Lowassa arejea CCM, asindikizwa na Rostam

Rais John Magufuli akizungumza na Edward Lowasa (wa pili kushoto) katika Ofisi za CCM zilizopo Mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam jana, baada ya waziri huyo mkuu wa zamani kutangaza kurejea CCM. Kulia ni Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally na kushoto ni Mfanyabiashara Rostam Aziz. Picha na Ikulu

Muktasari:

  • Katibu wa NEC anayehusika na siasa na uhusiano wa kimataifa, Kanali Ngemela Lubinga aliliambia Mwananchi kuwa Lowassa alikwenda ofisi hizo akiwa kwenye gari aina ya Range Rover iliyokuwa ikiendeshwa na Rostam, ambaye alikuwa mbunge wa Igunga.

Dar es Salaam. Edward Lowassa, aliyeweka rekodi ya kuwa mgombea urais wa upinzani aliyepata kura nyingi, amerejea CCM akisema “nimerudi nyumbani”.

Kauli hiyo aliiitoa nje ya majengo ya ofisi za makao makuu ya CCM, akiwa mbele ya viongozi wa juu wa CCM wakiongozwa na Rais John Magufuli pamoja na mfanyabiashara maarufu, Rostam Aziz, aliyewahi kutangaza kujiondoa kwenye siasa.

“Bwana Yesu asifiwe, salaam alleikum. Sina mengi ya kusema; nimerudi nyumbani,” alisema Lowassa mbele ya umati wa watu waliokuwa nje ya ofisi hizo zilizopo Lumumba.

Kauli yake ni tofauti na wanachama wengine waliotoka upinzani, ambao wamekuwa wakieleza udhaifu wa vyama vyao na kusifu uongozi wa CCM na Serikali.

Lowassa maarufu kwa jina la “mamvi” kutokana na nywele zake kujaa mvi, alipambana vikali na Rais Magufuli wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na kufanikiwa kupata kura milioni 6.07 ambazo ni takriban mara tatu ya kura ambazo wagombea wa upinzani walikuwa wakipata tangu mwaka 1995.

Katibu wa NEC anayehusika na siasa na uhusiano wa kimataifa, Kanali Ngemela Lubinga aliliambia Mwananchi kuwa Lowassa alikwenda ofisi hizo akiwa kwenye gari aina ya Range Rover iliyokuwa ikiendeshwa na Rostam, ambaye alikuwa mbunge wa Igunga.

“Alisema anakuja nyumbani alikotoka kujenga nchi,” alisema Kanali Lubinga.

Alisema walimpokea nje ya ofisi hizo za CCM ili kila mwananchi aone kuwa amerudi alikotoka.

“Amesindikizwa na Rostam na mjiandae kumpokea na yeye kwenye siasa, ” alisema Kanali Lubinga.

Rais Magufuli alimkaribisha Lowasaa kwa kusema maendeleo hayana chama na alimmwagia sifa waziri huyo mkuu wa Serikali ya Awamu ya Nne kwamba ni mstaarabu kwa kuangalia kampeni zake za mwaka 2015.

“Mimi na Lowassa hatukufanya kampeni za kutukanana, zilikuwa kampeni za kistaarabu,” alisema.

Lowassa aliwahi kujitokeza kugombea urais mwaka 1995, lakini baadaye akatangaza kumuunga mkono Jakaya Kikwete, ambaye alishindwa katika kura za maoni na Benjamin Mkapa.

Hakujitokeza mwaka 2005 badala yake akawa nguzo ya ushindi wa Kikwete, kabla ya kuchukua fomu mwaka 2015 lakini akakatwa jina na Kamati Kuu, hali iliyosababisha Halmashauri Kuu kugawanyika, baadhi ya wajumbe wakiimba “tuna imani na Lowassa” mwanzoni mwa mkutano.

Alihamia Chadema, ambayo ilimpa fursa ya kuendeleza ndoto yake ya urais, akiungwa mkono na vyama vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi.

Tangu ashindwe uchaguzi amekuwa mkimya, lakini mwaka jana alistua ulimwengu wa siasa alipoenda Ikulu na kufanya mazungumzo na Rais Magufuli na baadaye kusifia uongozi wake.

Baadaye aliwaambia waandishi kuwa Rais alijaribu kumshawishi arejee CCM.

Sumaye ashtushwa

Tukio la Lowassa kurejea CCM lilionekana kama lilitarajiwa na uongozi wa juu uliokusanyika kumlaki, na haukuwa wa ajabu pia kwa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Frederick Sumaye.

“Mimi haunipi shida. Mtu akiamua kuhama chama kwenda kingine ni uamuzi wake,” alisema Sumaye, ambaye sasa ni mwenyekiti wa Kanda ya Pwani na mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema.

Lakini akasema hayuko njiani kumfuata Lowassa.

“Kama kaamua acha aende, sisi tutaendelea kujenga chama na hicho unachokisema cha kuhama ni ndoto ambayo haipo,” alisema Sumaye akijibu swali kama naye ana mpango huo.

Naye katibu mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji alisema kuondoka Lowassa hakutaweza kukiteteresha chama hicho.

“Tunamtakia maisha mema huko aendapo. Yeye ni mtu mzima anajua anachokifanya,” alisema Dk Mashinji.

Lakini mwenyekiti wa CUF, ambaye alijivua madaraka yake mwaka 2015 kupinga Lowassa kugombea urais kwa mgongo wa vyama vya upinzani, Profesa Ibrahim Lipumba alikuwa na maneno makali baada ya kupata taarifa hizo, akisema alishajua ingawaje hakufahamu ni siku gani.

Profesa Lipumba alisema kila wakati aliwaeleza Watanzania kuwa wagombea wa nafasi ya urais wa CCM ni wawili na si Magufuli pekee kama watu walivyodhani, kwani Lowassa naye alikuwa mgombea wa CCM kupitia upinzani.

“Leo imedhihirika. Hata alipokuja yule mganga wa Nigeria (nabii TB Joshua), kukutana nao kwa nyakati tofauti niliwahi kusema suala hili. Leo Watanzania watakuwa mashahidi kwa Lowassa kurejea,” alisema Lipumba

“Lowassa amerudi CCM bila aibu wakati (mwenyekiti wa Chadema, Freeman) Mbowe bado yupo gerezani. Hakufikiria wenzake anawaachaje.”

Naye mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema kwanza “ni haki yake kikatiba kuhama chama na kujiunga na chama kingine.

“Tunampongeza kwa kazi nzuri aliyoifanya katika siasa za upinzani. Tatu, upinzani si uadui na nne namtakia kila la kheri huko aendako,” alisema mbunge huyo wa Vunjo.

Wakati Mbatia akieleza hayo, katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad alisema kitendo cha Lowassa kurejea CCM ni pigo kwa upinzani kwa kuwa alikuwa nguzo muhimu kwenye siasa za upinzani.

“Tuliobaki tutazidisha ari ya kujiimarisha na kujenga nguvu zaidi ya kupambana na watawala,” alisema Maalim Seif.

Safari ya Lowassa

Lowassa na wenzake 33 walikatwa katika mbio za urais za CCM Julai 10, 2015 baada ya Kamati ya Maadili ya CCM kuona hawana sifa ya kugombea urais.

Uamuzi huo ulisababisha wajumbe watatu wa Kamati Kuu, Dk Emmanuel Nchimbi, Sophia Simba na Adam Kimbisa kuwaambia waandishi wa habari kuwa wanapinga kitendo hicho kwa kuwa hakikufuata Katiba ya CCM.

Wakati mkutano mkuu ukipitisha jina la mgombea urais wa chama hicho, Lowassa na wafuasi wake walikuwa kwenye mipango ya kutangaza kuhama chama. Julai 27, 2015 kwenye hoteli ya Bahari Beach, Lowassa alikwenda kwenye mkutano wa Kamati Kuu ya Chadema na kujiunga na chama hicho na aliteuliwa kuwa mgombea wa Ukawa.

Akizungumza kwenye mkutano huo baada ya kujiunga Chadema, Lowassa alimshukuru mke wake na wanafamilia katika kipindi kigumu walichokuwa nacho wakati huo, pia wanaCCM waliomuunga mkono na kumdhamini.

“Kilichotokea Dodoma, ni kupora madaraka ya Kamati Kuu, Waswahili wanasema kubaka madaraka. Chuki na roho mbaya zilitawala licha ya mimi kuwa mgombea mwenye ushawishi,” alisema.

Kurejea CCM kulibashiriwa

Uamuzi wa kurejea CCM unaonekana kama wa ghafla, lakini tetesi zilishaanza muda mrefu, lakini Novemba 17, 2017 akiwa jijini Arusha alikanusha tetesi hizo.

“Huu ni uongo wa kutunga. Wamekuwa wakitunga vitu vingi juu yangu. Mimi sina mpango wa kurejea CCM,” Lowassa aliiambia Mwananchi.

Alisema uongo mwingine ambao unasambazwa ni kuwa Serikali imezuia watu kumtembelea nyumbani kwake jambo ambalo anaamini ni maneno yanayotungwa. Pia, Desema 7, 2018, Lowassa alizungumzia tena taarifa za kurejea CCM akisisitiza hana mpango, hajafikiria wala hajapanga kuondoka chama hicho kikuu cha upinzani.

“Sina mpango wa kuondoka Chadema, sijapanga wala sijafikiria kuondoka Chadema,” alisema Lowassa alipofanya mahojiano maalumu na Mwananchi ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana.

Lowassa alizungumza na Mwananchi baada ya viongozi wa chama hicho kumtaka ajitokeze kuweka wazi msimamo wake.