Makonda apiga marufuku wasiooga, kufua nguo kwenda mjini

Monday July 29 2019
pic makonda

Dar es Salaam. Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam nchini Tanzania, Paul Makonda amepiga marufuku watu wachafu kuonekana mitaani hasa wakati wa mkutano wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Makonda ameyasema hayo leo Jumatatu Julai 29,2019 wakati akizindua kampeni nyingine ya usafi wa jiji la Dar es Salaam ikiwa ni moja ya maandalizi ya mkutano wa 39 wa SADC unaotarajiwa kufanyika hapa nchini Agosti 17 na 18, 2019.

Amesema magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu yamekuwa changamoto kwa sababu ya ugumu wa mioyo ya watu kubadilika na kujenga tabia ya usafi kwenye makazi yao na miili yao wenyewe.

"Tabia ya kuna mjini bila kunyoosha nguo ni marufuku. Tabia ya kuja mjini hujaoga ni aibu. Watu wanatembea tu na chawa, kama huwezi kuwa msafi basi subiri mwezi huu upite."

"Kwa kipindi hiki tuvumiliane, kama hufui nguo, kama huogi, pumzika kidogo kuja mjini," amesema Makonda na kusisitiza kwamba hataki kumtia aibu Rais wa Tanzania John Magufuli mbele ya marais kutoka nchi 15 watakaokuwa hapa nchini.

Pia, Makonda ameagiza kwamba mtu yoyote mwenye gari atakayetupa takataka barabarani asitozwe faini badala yake apewe eneo la kufanya usafi. Amesema baadhi ya watu hao wana jeuri ya fedha, hivyo kwao faini siyo adhabu.

Advertisement

"Mtu mwenye gari akitupa takataka msimtoze faini, mshusheni kwenye gari, mpeni kipande cha kilomita moja cha barabara apige deki. Hawa watu fedha kwao siyo tatizo, sasa tunataka kuwaonyesha kwamba na sisi tuko serious na usafi wa jiji letu," amesema Makonda mbele ya maofisa afya na mazingira kutoka manispaa zote za Dar es Salaam.

Awali, mwenyekiti wa kamati ya usafi ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Sarah Msafiri amebainisha kwamba shughuli ya usafi itafanywa na vijana 130 wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na mgambo 300 katika maeneo mbalimbali ya jiji.

Amesema halmashauri za manispaa zilizopo jijini hapa zimetoa vifaa mbalimbali vya usafi vitakavyotumika katika shughuli hiyo ya usafi. Pia, amebainisha kwamba wakandarasi kwenye manispaa wametoa magari yao kusaidia shughuli hiyo ya usafi ambayo imeanza leo.

"Shughuli ya usafi itaanzia katika Uwanja wa Ndege, wengine watatawanyika kwenda maeneo mengine. Tutahakikisha jiji linakuwa safi kuelekea mkutano wa Sadc ambapo wageni mbalimbali watawasili," amesema Msafiri.

Advertisement