Mchungaji Msigwa aitaka Serikali ya Tanzania kufikiri matokeo kuliko uamuzi

Thursday April 11 2019
msigwa pic

Dodoma. Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa amesema matokeo ya uamuzi unaofanywa na Serikali ni muhimu kuliko uamuzi husika, kutolea mfano jinsi sheria na mambo mbalimbali yanayopitishwa bungeni na maeneo mengine inavyoibua hali ya sintofahamu nchini.

Mchungaji Msigwa ametoa kauli hiyo jana jioni Jumatano Aprili 10, 2019 bungeni jijini Dodoma katika mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora) kwa mwaka wa fedha 2019/2020.

Amesema tangu Serikali hii iingie madarakani imefanya uamuzi mkubwa katika mambo matatu na mengine madogo yasiyopungua 10.

“Serikali ilifanya uamuzi kuhusu kikokotoo, korosho, muswada wa habari, muswada wa takwimu, kutofanya kazi na CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali), muswada wa vyama vya siasa, Stiegler’s Gorge (mradi wa kuzalisha umeme wa Rufiji), reli ya kisasa (SGR), ununuzi wa ndege na kuhamia Dodoma,” amesema Mchungaji Msigwa na kuongeza:

“Moja ya sifa ya viongozi duniani ni kufanya uamuzi sina tatizo na hilo, lakini tunapaswa kujua kama taifa matokeo ya uamuzi tunaofanya ni ya muhimu zaidi kuliko uamuzi tunaoufanya. Hatuishi kwa uamuzi tunaoufanya dakika moja, tunaishi kwa matokeo ya uamuzi tunaoufanya.”

Amesema kabla ya kufanya uamuzi watu wenye busara na hekima lazima wajifunze kwa kufanya utafiti, kupitia taarifa za kihistoria na kutazama wengine wamefanya uamuzi gani katika mambo wanayokwenda kuyafanya.

Advertisement

“Tukienda kwenye kikokotoo (utaratibu wa ulipaji mafao kwa watumishi wa umma), Jenista (Mhagama-Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu) anahusika. Mlikuja hapa  na nyimbo nyingi kuhusu kikokotoo,” amesema Msigwa na kuongeza:

“Na kwa mujibu wa taratibu ili sheria ije bungeni inapitia hatua mbalimbali, inaanza kwenye wizara husika, makatibu, baraza la mawaziri, wadau na inakuja bungeni. Baada ya kufanya uamuzi wa kikokotoo na kupitisha kwa mbwembwe nyingi baada ya miezi mitatu mkaweka u-turn (mkageuka).”

Sakata la kikokotoo lilizimwa na Rais John Magufuli baada ya kurejesha utaratibu wa zamani wa ulipaji wa mafao kwa watumishi wa umma kutokana na utaratibu mpya kuibua sintofahamu.

“Swali la kujiuliza, kama kupitia hatua zote hizi ndani ya miezi kadhaa mkaanza kukipinga kikokotoo. Rais kateua maprofesa, madokta, wenye shahada wanaoweza kuona vitu vina hoja na wabunge tukaimba ngonjera nyingi bila kuangalia matokeo tunaitumbukiza nchi kwenye matatizo,” amesema mbunge huyo.

Amebainisha kuwa hata sakata la korosho pia lilianzia bungeni na hoja kupitishwa na kuhoji: “Baada ya muda mfupi tunaambiwa kangomba hawana makosa. Nyinyi ambao mnasema mko fiti kuiongoza nchi hii huwa mnafikiria kuhusu matokeo ya uamuzi mnaoufanya?”

Kuhusu muswada wa habari amesema: “Hivi  mawaziri hawakuwa wakijua kuwa unakinzana na Jumuiya ya Afrika Mashariki, baraza zima la mawaziri mlileta hapa. Haya mkapitisha azimio la kutofanya kazi na CAG, leo vitabu vyake vipo hapa vikiwa na saini yake.

“Swali langu kwenu, mnapofanya uamuzi huo mnafanya utafiti, maprofesa mpo hapa huwa mnafanya utafiti?”

Amesema Rais John Magufuli katika ziara zake amekuwa akizungumzia masuala mbalimbali yanayosimamiwa na wizara.

“Huwa anazungumzia kuhusu wizara zote isipokuwa wizara ya Ulinzi, tulikosoa utaratibu wa kodi haufai leo Rais anasema kuhusu hilo, tulisema mnafukuza wawekezaji leo Rais analalamika wawekezaji wanakimbia,” amesema Msigwa.

Mbunge huyo amebainisha kuwa Tanzania inahitaji watu wenye akili nyingi, si kama naibu Waziri wa Tamisemi, Mwita Waitara anayedai kuwa mara nyingi akizungumza hudhani yupo katika mkutano wa siasa.

“Hatuwezi kuleta mabadiliko kwa tabia kama za Waitara  ambaye kila saa anadhani tupo katika mkutano wa siasa. Changamoto tulizonazo zinahitaji akili kubwa tuonyesheni nini mnafanya,” amesisitiza Msigwa.

Advertisement