Msikilize Naibu Waziri Waitara akisemacho kuhusu zawadi kwa Rais Magufuli

Muktasari:

Naibu Waziri wa Tamisemi, Mwita Waitara amesema zawadi ambayo Watanzania  wanatakiwa kumpa Rais John Magufuli ni kuunga mkono juhudi zake za kuiletea nchi maendeleo.

Same. Naibu Waziri wa Tamisemi, Mwita Waitara amesema zawadi ambayo Watanzania  wanatakiwa kumpa Rais John Magufuli ni kuunga mkono juhudi zake za kuiletea nchi maendeleo.

Waitara ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Julai 19, 2019, alipokuwa akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, mgeni rasmi akiwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Waitara amesema ni vema Watanzania wakamuunga mkono Rais Magufuli pia  katika uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa na ule Mkuu, ili aweze kuwapata viongozi ambao akiwatuma kazi watakwenda kutumikia bila shaka.

“Niwaombe Watanzania wa Same na wote nchini, tumpatie zawadi kubwa Rais, Makamu wake na Waziri Mkuu, kwa kwenda kuwachagua viongozi safi ambao watatenda yale yanayokusudiwa na serikali hii.

“Mkichagua madiwani wa CCM viongozi wakija watakuwa pamoja, mkichagua wabunge wa CCM  viongozi wakija watakuwa pamoja, haya mambo mjifunze ili kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa na uchaguzi Mkuu ujao tuzungumze lugha moja.

Akizungumza na watumishi hao, Waziri Mkuu Majaliwa amesema popote walipo lazima watambue kuwa wanafanya kazi zao kwa mujibu wa Serikali iliyopo madarakani.

“Uwapo wenu hapa lazima mtambue mnatekeleza matakwa  ya Serikali iliyoko madarakani, na Serikali hii haimvumilii mtu asiyefanya kazi,” amesema Majaliwa.