Polisi watoa sababu za askari wake kutumia nguvu kumdhibiti dereva

Muktasari:

  • Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Songwe, Yusuph Sarungi leo Jumatatu amezungumzia tukio la askari wa usalama barabarani kutumia nguvu kumdhibiti dereva wa gari mkoani Songwe.

Mbozi:  Jeshi la Polisi mkoani Songwe limeeleza sababu ya askari wa usalama barabarani kumshambulia dereva kwa kumpiga kuwa alitumia lugha ya matusi na kutotii amri ya kumtaka atoe ushirikiano kwa wanausalama hao ambao walikuwa wakifanya kazi kwa kushirikiana na maofisatoka Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchikavu (Sumatra).

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani hapa Yusuph Sarungi amewaambia waandishi wa habari leo Jumatatu Januari 14, 2019 kuwa tukio hilo lilitokea juzi Jumamosi Januari 12, 2019 saa 2:30 asubuhi katika eneo la Transforma, halmashauri ya mji wa Tunduma wilayani Momba wakati askari hao wakishirikiana na maofisa toka Sumatra wakiwa kwenye ukaguzi wa magari mbalimbali.

Amesema dereva huyo Mawazo Jairos (29) mkazi wa Mbeya aliyekuwa akiendesha gari aina ya Mistubishi Fuso lenye namba za usajili T842 AAC, baada ya kusimamishwa alianza kutoa lugha za kashifa na matusi kwa askari na maofisa wa Sumatra.

Kamanda huyo amesema Jairos aliliondoa gari bila ya kuruhusiwa kwa kupitia barabara ya vumbi hali iliyolazimu askari hao kumfuatilia na kumkamata tena katika eneo la Makambini ambapo walimzuia tena.

Sarungi amesema dereva huyo aliteremka kwenye gari kwa jazba huku akiendelea kutoa matusi na kumshambulia askari ambapo hata hivyo askari hao walifanikiwa kumdhibiti hali iliyofanya apige kelele kuomba msaada.

Amesema wananchi walifika lakini wakati wananchi wanamsaidia dereva huyo alifanikiwa kuwatoka na kwenda kwenye gari kisha kuchukua panga kuwatishia askari hao na kufanikiwa kuondoa gari eneo la tukio hadi alipokamatwa tena katika mji wa Vwawa.

Kamanda Sarungi aliongeza kuwa askari polisi hao walikuwa wanatimiza wajibu wao wa kazi kwa kumdhibiti dereva huyo kwa vile sheria inawaruhusu kutumia nguvu za kadri ili kumdhibiti mhalifu.