Profesa Lipumba apitishwa kugombea uenyekiti CUF

Wajumbe wanaowania nafasi ya Mwenyekiti Taifa wa Chama Cha Wananchi Cuf, kutoka kushoto  ni  Zuberi Mwinyi, Profesa Ibrahim Lipumba na  Diana Simba wakionyesha namba zao za kupigiwa kura na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa saba wa Chama hicho unaoendelea leo jijini Dar es Salaam. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

  • Baraza Kuu la Chama cha Wananchi (CUF) leo Jumatano limepitisha majina matatu ya wagombea nafasi ya uenyekiti wa CUF akiwamo Profesa Ibrahim Lipumba.

Dar es salaam. Baraza Kuu la Chama cha Wananchi (CUF) limewapitisha wanachama watatu wa chama hicho akiwamo Profesa Ibrahim Lipumba kugombea nafasi ya uenyekiti wa chama hicho.

Akizungumza kwenye mkutano wa saba wa chama hicho leo Jumatano Machi 13, 2019 Profesa Lipumba amesema kwa sababu ni miongoni mwa wagombea wa nafasi ya uenyekiti hawezi kuwa mwenyekiti wa kikao hicho.

Amesema kwa mujibu wa katiba, kanuni na taratibu za chama hicho kikao kipendekeze mwenyekiti wa muda.

Aliwauliza wanachama kwa ujumla wao wanamtaka nani awe mwenyekiti wa muda wakajibu. ‘Milambo Yusuph Kamili’ hivyo akamtangaza kuwa ndiyo mwenyekiti wa muda wa kikao hicho.

Awali, Profesa Lipumba ametoa ufafanuzi wa uchaguzi utakavyofanyika kuwa wataanza na kumchagua  mwenyekiti wa taifa, akifuatia makamu mwenyekiti Zanzibar na kumalizia na makamu mwenyekiti Tanzania Bara.

Pamoja na Profesa Lipumba wengine kwenye kinyang’anyiro hicho ni Diana Daudi Simba na Zuberi Mwinyi Hamisi. Mkutano huo umehudhuriwa na wajumbe 798.

Naye Mkurugenzi wa habari wa CUF, Abdul Kambaya amesema kinachoendelea sasa hivi ni kuchagua wajumbe watakaoshiriki uchaguzi huo.

Kambaya amesema hali ya leo katika mkutano huo itakuwa nzuri tofauti na ilivyokuwa jana. Pia amesema kutakuwepo na ulinzi wa askari ambao watakuwa wamevaa nguo za kiraia ili kuhakikisha hali ya usalama inakuwapo.

Endelea kufuatilia Mwananchi kujua kinachojiri kwenye mkutano huo