SADC yajipa vipaumbele kutokomeza VVU ifikapo 2030

Monday August 12 2019

 

By Herieth Makwetta, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Sekretarieti  ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) imesema imeamua kuongeza kasi ya kutokomeza virusi vya ukimwi ifikapo mwaka 2030 kwa kuja na mpango mkakati maalum.

Imesema kufikia mwaka 2030 asilimia 95 ya wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi (VVU) wawe wanafahamu hali zao, asilimia 95 ya wanaofahamu wapate matibabu na asilimia 95 ya wanaopata tiba wapunguze kiwango cha virusi.

Hayo yamesema leo Jumatatu Agosti 12, 2019 na Mkurugenzi wa jamii na maendeleo ya watu kutoka SADC, Duduzile Simelane wakati akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam nchini Tanzania.

Amesema hatua hiyo imefuatia baada ya mpango wa 2020 ambao ulilenga asilimia 90 ya wanaoishi na VVU wawe wanafahamu hali zao, asilimia 90 wapate matibabu na asilimia 90 ya wanaopata tiba wapunguze kiwango cha virusi na kupunguza maambukizi kwa asilimia 75.

“Mpango huu umefanywa kupitia maendeleo ya SADC, kupitia mpango huu kutakuwa na programu mbalimbali ikiwemo kuwalenga watu ambao wapo hatarini zaidi, kuhakikisha kunakuwa na matibabu ya hiari ya tohara kwa wanaume, usambazaji wa kondomu na uimarishwaji wa vifaa tiba hasa vipimo vya vvu na kinga zingine,” amesema Simalane.

Amesema tayari mipango ya awali kuhusu namna ya kuanza utekelezaji huo imeanza kwa Taasisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia masuala ya virusi vya ukimwi (UNAIDS) kutoka fedha kwa ajili ya afya na VVU kwa kusudi la kusaidia nchi wanachama kuweza kufikia malengo waliyojiwekea.

Advertisement

Advertisement