Serikali ya Tanzania yawatangazia neema wakulima wa pamba

Muktasari:

Serikali ya Tanzania imesema itahakikisha wakulima wa pamba hawauziwi dawa feki kwa lengo la kuwasaidia kuingia hasara kwa kununua dawa zisizoua wadudu.

Tabora. Serikali ya Tanzania imeahidi kufanya udhibiti wa dawa feki za kuulia wadudu katika zao la pamba kwa lengo la kuwanusuru wakulima wasipate hasara.

Akizungumza na wakazi wa kijiji cha Mwabakima leo Jumatatu Julai 15, 2019 Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Serikali inafahamu kuna dawa feki zinauzwa na wakulima wanazinunua ambazo haziwasaidii kwa vile haziuwi wadudu.

Amesema kutokana na hali hiyo, Serikali italisimamia eneo hilo kwa lengo la kuwalinda wakulima wasinunue dawa isiyowasaidia.

"Nawaomba wakulima suala hili mliachie Serikali iweze kudhibiti hali hiyo," amesema

Amewahakikishia wakulima wa pamba kuwa Serikali itahakikisha dawa zinazotumika ziwe ni zile zinazoua wadudu na sio vinginevyo na kwamba haitawaangusha wakulima hao.

Ameeleza wameimarisha Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na kuimarisha chuo cha Ukiriguru na kuwaondoa wasiwasi kuwa hali itakuwa nzuri.