Simulizi chungu mauaji ya dada wa Bilionea Msuya

Muktasari:

  • Moja ya matukio yaliyovuta hisia za wengi na kuendelea kufuatiliwa kesi yake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ni mauaji ya Aneth Msuya, dada wa aliyekuwa mfanyabiashara maarufu na tajiri wa madini mkoani Arusha, Erasto Msuya, maarufu kama Bilionea Msuya. Aliuawa Mei 25, 2016, nyumbani kwake Kibada, Kigamboni, Dar es Salaam. Mauaji hayo yalitikisa kwa jinsi alivyouawa kinyama. Wanaotuhumiwa kuhusika nayo walikamatwa na kufikishwa Mahakama ya Kisutu ilikofunguliwa kesi ili kukamilisha hatua za awali na upelelezi ambao sasa umekamilika.

 

Mauaji ya Aneth Msuya ni moja ya matukio ya simanzi yaliyopata kutikisa jijini Dar es Salaam kutokana na namna alivyouawa kinyama na mtiririko wa matukio ya mashambulizi na mauaji katika familia yao.

Aneth, ambaye ni dada wa aliyekuwa mfanyabiashara maarufu na tajiri wa madini Mirerani mkoani Arusha, Erasto Msuya ‘Bilionea Msuya’, aliuawa Mei 25, 2016, nyumbani kwake Kibada, Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Mwanamama huyo aliuawa kinyama kwa kuchinjwa na mwili wake kuachwa uchi ikiwa ni miaka mitatu tangu kuuawa kwa kaka yake, Bilionea Msuya.

Simulizi hii inatokana na maelezo ya mashahidi wa upande wa mashitaka katika kesi inayowakabili washitakiwa wa kesi ya mauaji hayo.

Maelezo hayo yalisomwa na mawakili wa Serikali wakati jalada la kesi hiyo lilipofungwa rasmi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilikofunguliwa ili kukamilisha hatua za awali ikiwa ni pamoja na upelelezi. Baada ya hatua hizo kukamilika itahamishiwa Mahakama Kuu ambako ndiko itakakosikilizwa na kutolewa uamuzi.

Maelezo hayo ya mashahidi wa upande wa mashitaka yanawataja watuhumiwa wa mauaji hayo, sababu, mipango na namna yalivyotekelezwa.

Aneth ni nani

Aneth Simon Msuya, ambaye jina lake halisi alilopewa na wazazi wake ni Anathe alizaliwa Aprili 3, 1986 katika Hospitali ya Machame mkoani Kilimanjaro.

Baada ya kufikisha miaka sita alianza elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Msaleni, iliyopo mkoani Kilimanjaro ambako alihitimu. Baadaye alijiunga Shule ya Sekondari St Dorcas Seminary iliyopo Moshi.

Katika mtihani wa kidato cha nne alifanya vizuri kwa kupata daraja la kwanza (division one) ya alama nane (8). Kisha alijiunga na Shule ya Sekondari Lutheran Junior Seminary iliyopo Morogoro.

Katika mtihani wake wa kuhitimu kidato cha sita, pia Aneth alifanya vizuri kwani alipata daraja la kwanza kwa alama nne (4).

Alijiunga masomo ya elimu ya juu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) akichukua shahada ya uchumi, ambapo alihitimu shahada yake huku akifanya vema na kuwa mwanafunzi bora wa kwanza kwa kozi hiyo.

Kutokana na ufaulu wake huo mzuri alifanikiwa kupata ufadhili wa Wizara ya Fedha, ambayo ilimsomesha Shahada ya Uzamili ya Uchumi hapohapo UDSM na baada ya kuhitimu shahada hiyo aliajiriwa na Wizara ya Fedha.

Licha ya uwezo huo mkubwa wa kiakili aliokuwa nao Aneth, baadhi ya watu waliokuwa karibu naye wanaeleza hakuwa mtu mwenye kujivuna bali alikuwa mpole na hakuwa mzungumzaji sana.

Aneth alifunga ndoa mwaka 2011, na (Wilbard Kimario) na wakafanikiwa kupata mtoto mmoja wa kiume, lakini ndoa yao haikudumu kwani mwaka 2012, wawili hao waliachana.

Kwa mujibu wa watu waliokuwa karibu na marehemu Aneth, tangu wakati huo hadi mauti yanamfika, hawakuwahi kumuona Aneth akiwa na mwanaume wala kusikia ana uhusiano na mwanaume mwingine.

Kutokana na mauaji hayo, watu wawili walikamatwa kwa tuhuma za kuhusika nayo na hatimaye kupandishwa kizimbani na kusomewa shitaka moja la kumuua Aneth.

Washitakiwa hao ni Miriam Mrita (mshtakiwa wa kwanza), ambaye ni mke wa marehemu Bilionea Msuya, yaani wifi wa marehemu Aneth pamoja na mfanyabiashara Revocatus Muyella.

Kwa pamoja washitakiwa hao wanadaiwa kumuua kwa makusudi, Aneth Msuya kinyume na kifungu cha 196 cha Kanuni za Adhabu (Penal Code- PC) wakidaiwa kutenda kosa hilo, Mei 25, 2016 nyumbani kwa marehemu maeneo ya Kibada, Kigamboni, Dar e Salaam.

Kesi hiyo namba 5 ya mwaka 2016 ilifunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa ajili ya kukamilisha hatua za upelelezi kabla ya kuhamishiwa Mahakama Kuu ambayo ndiyo yenye mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.

Mahakamani hapo kesi hiyo ilikuwa ikisikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba. Waendesha mashtaka walikuwa Wakili wa Serikali Mwandamizi (SSA) Patrick Mwita na Wakili wa Serikali (SA) Faraj Nguka na washitakiwa wote wanatetewa na Wakili Peter Kibatala.

Baada ya upelelezi kukamilika, Novemba Mosi, 2018, washitakiwa hao walisomewa maelezo ya mashahidi watakaoitwa kutoa ushahidi upande wa mashitaka, kuthibitisha shitaka dhidi ya washtakiwa hao.

Hatua ya washitakiwa kusomewa maelezo ya mashahidi ndio lilikuwa hitimisho la majukumu ya Mahakama ya Kisutu, hivyo kesi hiyo ilifungwa rasmi mahakamani hapo na sasa itahamishiwa Mahakama Kuu kwa ajili ya usikilizwaji na uamuzi.

Mashahidi na vielelezo vitakavyotumika

Awali Wakili Mwita aliieleza Mahakama kuwa upande wa mashitaka utakuwa na mashahidi 45 na vielelezo zaidi ya 14 ambavyo vitatumika kujenga kesi, kuthibitisha mashitaka na hatia dhidi ya washitakiwa.

Miongoni mwa mashahidi hao ni mama mzazi wa Aneth, Ndesu Msuya, mfanyakazi wa ndani wa Aneth, Getrude Mafuru pamoja na majirani wa marehemu akiwemo mwanafunzi wa shule ya msingi.

Wengine ni polisi kutoka mkoani Arusha na Dar es Salaam akiwemo Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kinondoni na Mkuu wa Upelelezi Temeke, mchunguzi wa picha za kawaida na video kutoka jeshi la polisi na mtaalamu wa uchunguzi wa kijinai.

Vielelezo vitakavyowasilishwa mahakamani hapo na upande wa mashitaka ni pamoja na taarifa ya uchunguzi wa chanzo cha kifo, ramani ya eneo la tukio na taarifa ya uchunguzi wa vinasaba ( DNA) vya mshtakiwa wa pili.

Vingine ni maelezo ya onyo ya washtakiwa na maelezo ya ungamo ya mshitakiwa wa kwanza, Miriam; hati za ukamataji, ukaguzi na utambuzi wa magari ya kifahari; hati ya ukaguzi wa nyumba. Vilevile kuna hati za gwaride la utambuzi wa washitakiwa na za utambuzi wa magari pamoja na picha za magari yaliyokamatwa yakidaiwa kutumiwa na washitakiwa kwenye uhalifu.

Maelezo ya mashahidi

Baada ya kumaliza kutaja idadi na majina ya mashahidi pamoja na vielelezo, mawakili hao wa upande wa mashitaka walianza kuwasomea washtakiwa maelezo ya mashahidi wote wanaotarajiwa kutoa ushahidi katika kesi hiyo.

Mawakili hao waliwasomea washtakiwa maelezo ya mashahidi hatua kwa hatua, kwa kupokezana kila baada ya kusoma maelezo ya mashahidi kadhaa, kazi ambayo ilitumia takribani saa tano, kuanzia saa 5.15 asubuhi mpaka saa 9.55 alasiri, Alhamisi iliyopita

Pamoja na mambo mengine yaliyomo katika maelezo ya mashahidi hao, mawakili hao walidai mshitakiwa wa kwanza, Miriam alikiri kuhusika katika mauaji hayo na kueleza sababu na mpango wa namna walivyotekeleza mauaji

Mipango ya mauaji

Wakili Mwita alidai washtakiwa katika kutekeleza mauaji hayo walimtafuta mfanyakazi wa ndani wa Aneth.

Alidai Mei 5, 2016 , Miriam na mwenzake walienda Kibada alikokuwa akiishi Aneth na kwamba kabla ya kufika katika nyumba ya Aneth, alikutana na mfanyakazi huyo wa ndani wa Aneth, aitwaye Getrude Mafuru ambaye alikuwa anaenda dukani kununua karatasi za chooni (toilet paper).

Wakili Mwita alidai mshtakiwa Miriam alishusha kioo cha gari la kifahari lenye rangi ya bluu alimokuwamo na kumuita Getrude ambaye aliitikia wito na akamuuliza mahali Aneth alikokuwa akiishi. Alidai kuwa Getrude alimueleza kuwa Aneth anakaa nyumba iliyokuwa inafuata, kutoka walikokuwa wamesimama na kisha Miriam alimuahidi msichana huyo kuwa angepita kesho, kisha alipandisha kioo cha gari yake na kuondoka.

Siku iliyofuata, Wakili Mwita alidai Miriam alienda tena hadi karibu na nyumba aliyokuwa akiishi Aneth, ambapo alimuona Getrude akichota maji nyumba ya jirani na akamuita na msichana huyo alipomfikia, Miriam alimtaka apande katika gari hilo. Kwa mujibu wa maelezo hayo, Wakili Mwita alidai msichana huyo aliingia ndani ya gari hilo na Miriam akampatia simu ndogo yenye rangi nyeusi.

Mwita alidai kuwa wakati Getrude anapewa simu na Miriam, mshitakiwa wa pili yeye alikuwa amekaa nyuma huku akiwa amemuwekea Getrude bastola begani na kwamba Miriam alimwambia msichana huyo asimwangalie Muyella bali amwangalie yeye.

Wakili Mwita alidai Miriam alimweleza Getrude kuwa simu hiyo ni ya mawasiliano baina yao wawili huku akimweleza sio kwa ajili ya kumpigia mtu mwingine yeyote.

Alidai Getrude ambaye alikuwa analipwa mshahara wa Sh 60,000 alieleza kuwa sura ya Miriam alishawahi kuiona Moshi, kwa bibi yake yaani kwa mama yake marehemu Aneth, alikokuwa kabla ya kwenda kwa Aneth, na kwamba Miriam alikwenda nyumbani hapo na mumewe Erasto Msuya enzi za uhai wake.

Wakili Mwita aliendelea kudai kuwa Mei 23, 2016 saa tisa mchana, Miriam alimpigia Getrude na kumwambia anataka kuonana naye, huku akimwelekeza mahali alikokuwa.

Alidai kuwa Getrude alikwenda hadi mahali lilipokuwa limeegeshwa gari la washitakiwa hao, karibu na nyumba ya Aneth na kisha binti huyo aliingia katika gari hilo.

Wakili Mwita alidai Getrude akiwa ndani ya gari hilo aliiona pochi ya Miriam ikiwa imejaa hela zikiwa zimefungwa na mpira mwembamba, na Miriam akampa Sh 20,000.

Alidai baada ya kumpa fedha hizo, Miriam alimsisitiza Getrude aondoke nyumbani kwa Aneth kabla ya Mei 25, 2016 na kwamba simu hiyo aliyompa aitupe sehemu ambayo mtu mwingine hawezi kuiona.

Wakili Mwita alidai Mei 25, 2016 Getrude aliondoka nyumbani kwa Aneth na ufunguo wa geti aliupeleka kwa jirani yao, kisha akampigia simu Aneth kuwa ufunguo wa ndani upo chini ya kapeti la kufutia vumbi lililopo mlangoni na kwamba ufunguo wa getini upo kwa jirani yao.

Alidai Getrude aliondoka na kwenda Chanika kwa mchumba wake aitwaye Sabri Kombo, na kwamba wakati akiwa kwenye pantoni, aliitupa simu hiyo baharini na alipofika kwa mpenzi wake alimwelezea mambo aliyoambiwa na Miriam. Akiwa Chanika, Wakili Mwita alidai kuwa Getrude alipigiwa simu na bibi yake, yaani mama wa Aneth na kumweleza kuwa Aneth ameuawa kwa kukatwa koromeo.

Kwa upande wake Wakili Nguka alidai baada ya tukio, hilo timu ya askari wa upelelezi wakiongozwa na Mkuu wa Upelelezi Kinondoni, Mrakibu wa Polisi (SP) Richard Mwaisamba ilifika eneo la tukio na kukuta mlango wa nje ukiwa haujafungwa.

Alidai timu hiyo ilikuta mlango wa chumbani ukiwa umevunjwa kwa kutumia tofali na kwamba chini ya mlango kulikuwa na vumbi la matofali. Ndani ya chumba cha Aneth, Wakili Nguka alidai kuwa wapelelezi hao walikuta mwili wa Aneth ukiwa umekatwa koromeo ukiwa sakafuni, huku ukiwa uchi wa mnyama na mdomoni alikuwa amewekewa kitambaa.

Alidai pembeni mwa mwili wa Aneth, wapelelezi hao walikuta nguo ya ndani yenye rangi ya zambarau, kisu chenye damu na filimbi iliyokuwa karibu na kitanda. Kwenye kabati lililokutwa wazi walikuta hereni, cheni za dhahabu na simu.

Mshitakiwa adaiwa kukiri

Wakili Mwita alidai kuwa wakaguzi wa Polisi, Latifa Mohamed, ASP Jumanne Malangehe na Koplo Mwaka walienda Arusha kwa ajili ya kufanya mahojiano na upekuzi nyumbani kwa mshitakiwa Miriam.

Alidai Agosti 7, 2016 akihojiwa na wakaguzi hao, mshitakiwa huyo alikiri kuhusika kupanga mpango wa mauaji na aliwaelekeza maeneo walikokuwa wanapangia mpango huo. Alidai mbali na kukiri kosa hilo mbele ya askari hao ambao waliandika maelezo yake, pia mshitakiwa alikiri kutenda kosa hilo mbele ya Mlinzi wa Amani (Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo). Alidai wakaguzi hao wa polisi walirudi Dar es Salaam na Miriam, wakiongozana na wachunguzi wa picha za kawaida na za video kutoka makao makuu ya polisi na Miriam aliwapeleka sehemu ambayo walikuwa wanakutana na Getrude kwa ajili ya kufanikisha mauaji hayo.

Wakili Mwita alidai katika maelezo hayo ambayo mshitakiwa wa kwanza aliyatoa kwa askari na mbele ya Mlinzi wa Amani, alieleza kuwa aliamua kutenda kosa hilo kutokana na mgogoro wa mali za mumewe yaani Bilionea Msuya.

Pia, walidai kuwa mshtakiwa huyo aliamua kutenda kosa hilo kwa hasira kutokana na Aneth kumtumia picha za kukashfu umbile lake. Wakili Mwita alidai mshitakiwa alieleza kuwa Aneth alikuwa akimtumia picha za wanawake wenye maumbile makubwa mabaya, wenye matumbo makubwa, jambo ambalo lilimfanya apate hasira.

Alidai kwa mujibu wa maelezo yake, mshitakiwa Miriam baada ya kuchukizwa na kitendo cha wifi yake kumtumia picha hizo alizoziona kama za kumkashfu, aliamua kutafuta ushauri kwa mshitakiwa wa pili Muyella, ambaye alimshauri kuwa huyo dawa yake ni kumuua tu.

Wakili Mwita alidai baada ya ushauri huo wa mshitakiwa wa pili walikubaliana mshtakiwa wa kwanza amlipe mshitakiwa wa pili Sh20 milioni kwa ajili ya kazi hiyo.

Alidai washitakiwa hao baada ya makubaliano hayo ndipo walipopanga na kutekeleza mauaji hayo, na kwamba mshtakiwa wa kwanza alimlipa mshtakiwa wa pili Sh10 milioni kwanza wakiwa jijini Dar es Salaam na baada ya kutekeleza mauaji hayo, alimmalizia Sh10 milioni jijini Arusha.

Wakili Mwita aliieleza mahakama kuwa mshitakiwa wa pili baada ya kukamatwa na kuhojiwa alikubali kumfahamu mshitakiwa wa kwanza kuwa ni mfanyabiashara mwenzake na alikuwa akifahamiana na marehemu mumewe, lakini alikana kuhusika na mauaji hayo.

Licha ya kukana kuhusika katika mauaji hayo, Wakili Mwita aliieleza mahakama kuwa mshitakiwa huyo alitambuliwa na shahidi mmoja (ambaye ni shahidi muhimu kwenye kesi hiyo) kwenye gwaride la utambuzi. Kwa upande wake Wakili Nguka alidai Agosti 4, 2016 timu ya upelelezi kutoka Dar es Salama ilisafiri hadi Arusha kwa ajili ya kumkamata Miriam na walimkamata.

Wakili Nguka alidai Miriam alikamatwa akiwa katika klabu ya Tembo iliyopo Arusha kisha askari hao waliongozana na mshitakiwa huyo hadi nyumbani kwa mshtakiwa na kuanza upekuzi. Alidai katika upekuzi huo ulioanza saa saba mchana hadi saa 10 jioni, timu hiyo ya upekuzi ilichukua suti mbili ikiwemo ya rangi ya bluu na nyekundu, cheni za dhahabu na viatu jozi mbili.

Alidai Miriam alikiri kuhusika katika mauaji ya wifi yake kutokana na mgogoro wa kifamilia. Hata hivyo, kwa mujibu wa maelezo ya mashahidi hao, Miriam alipendekezwa na familia ya mumewe, Bilionea Msuya, na akateuliwa na mahakama kuwa msimamizi wa mirathi ya mumewe. Baadaye mshitakiwa huyo alilalamikiwa na ndugu wa marehemu kwa ufujaji wa mali na kwamba kutokana na kushindwa kuwasilisha mahakamani mrejesho wa usimamizi na mgawanyo wa mali hizo, mahakama iliamua kumuondoa katika usimamizi wa mirathi hiyo.

Kutokana na hali hiyo, mshtakiwa huyo aliomba ushauri wa mfanyabaishara aitwaye Muyella kuhusiana na mgogoro huo na kumueleza kuwa Aneth amekuwa akimuingilia katika mirathi na mali alizoachiwa na mume wake.

Kwa mujibu wa maelezo ya mashahidi hao, baada ya mahakama kumuondoa katika usimamizi wa mirathi, kikao cha familia kilimpendekeza dada mwingine wa marehemu Msuya pamoja na baba wa marehemu kuwa wasimamizi wa mirathi hiyo lakini mshtakiwa Miriam aliweka pingamizi.