Spika: Profesa Assad anampa wakati mgumu Rais

Spika wa Bunge Job Ndugai akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam jana, kuhusu ripoti ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali kwa mwaka 2017/18. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

 

  • Spika wa Bunge, Job Ndugai ameeleza kusitishwa kwake na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa kurudia tena neno udhaifu wa Bunge na amemtaka akamwone Rais ili wamalize mgogoro uliopo.

Dar es Salaam. Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amemshauri Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad akamwone Rais John Magufuli ili mzozo wake na Bunge uishe.

Kauli ya Spika inakuja wakati tayari Bunge limeshapitisha azimio la kutofanya kazi na Profesa Assad bali ofisi ya CAG.

Spika Ndugai aliyekuwa ziarani nchini Sweden wiki iliyopita ameyasema hayo leo Jumapili Aprili 14, 2019 akieleza kusikitishwa na hatua ya Profesa Assad kurudia neno udhaifu kwa Bunge alipotoa taarifa yake hivi karibuni.

"Zipo njia za kumaliza mambo kama haya, mojawapo aende kwa Rais akajieleze kwamba mimi nimepima nimeona nimekosea hapa na pale. Maana Rais ni sehemu yetu sisi (Bunge) hatuwezi kupitisha sheria bila yeye kupitisha mkono wake," alisema Ndugai.

Ameongeza kuwa hata bajeti inayojadiliwa na Bunge lazima ipitishwe na Rais. Amesema kwa kuwa Bunge limeshapitisha azimio la kutofanya kazi na Profesa Mussa Assad alitakiwa ajiuzulu.

"Kwa kuwa Bunge likishaaamua kuwa halifanyi kazi na mtu, ni uamuzi halali. Katika nchi zote Bunge likishakosa imani na wewe unajiuzulu," amesema.

Ameongeza, "Sasa hatumfundishi kazi Mussa Assad, anampa wakati mgumu Rais tu. Tutafanya kazi na ofisi ya wananchi."

Spika Ndugai amemsifu Profesa Assad kwa ujasiri wake huku akiufananisha na ujasiri wa mbwa kumtukana mtu anayemlisha.

"Unatukana hadi mkono unaokulisha, inahitaji ujasiri na jamaa ana ujasiri. Ila ni ujasiri ule wa mbwa anayemtukana anayemlisha," amesema.

Hata hivyo, Ndugai amesema hana chuki binafsi na Assad bali tatizo ni lugha tu aliyotumia ya kuliita Bunge dhaifu.