Spika apangua kamati katikati ya sakata la CAG

Dar es Salaam. Spika wa Bunge, Job Ndugai amefanya mabadiliko kwa kuwahamisha wajumbe wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na ile ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), ikiwa ni siku chache kabla ya CAG, Profesa Mussa Assad kufika mbele ya chombo hicho cha kutunga sheria.

Kamati hizo ndizo zinahusika na uchambuzi wa ripoti ya ukaguzi ya CAG-mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali, lakini ofisi ya Bunge imesema mabadiliko hayo ni ya kawaida.

Profesa Assad anatakiwa kufika mbele ya Kamati ya Maadili na Hadhi ya Bunge Januari 21 kujieleza kuhusu kauli aliyoitoa nchini Marekani kuwa Bunge halitekelezi majukumu yake kama inavyotakiwa, ikiwa ni pamoja na kuhoji udhaifu unaobainishwa kwenye ripoti zake.

Katika mabadiliko hayo, mbunge wa Chadema, Naghenjwa Kaboyoka, ambaye ni mwenyekiti wa PAC, amepelekwa Kamati ya Miundombinu, wakati makamu wake, Aeshi Hilaly (CCM amepelekwa Kamati ya Viwanda na Biashara.

Mbunge wa CUF, Vedasto Ngombale Mwiru ambaye ni mwenyekiti wa LAAC) aliiambia Mwananchi jana kuwa hata wajumbe wa kamati yake wamepangwa katika kamati nyingine.

“Kamati ni za Spika. Kwa nini amefanya hivi mimi sijui,” alisema Ngomale Mwiru ambaye ni mbunge wa Kilwa Kaskazini.

Mwananchi ilipotaka kujua watawasilishaje taarifa ya LAAC bungeni, Mwiru alisema: “Hata sisi hatujui kwa kuwa wiki ya kwanza ilikuwa tukutane na halmashauri, wiki nyingine tuandae taarifa, sasa kwa hali hii sijui ngoja tuone itakavyokuwa.”

Mmoja wa wajumbe wa PAC Anatropia Theonest (Chadema) alisema kuwa pamoja na ratiba hiyo kutolewa na Bunge wajumbe wa kamati yake wameshindwa kukutana na badala yake kila mmoja ilimlazimu kuripoti katika kamati mpya aliyopangiwa.

“Hizi taarifa tumeanza kuzipata juzi, zimevuruga utaratibu wetu wote. Sisi kama kamati tulishaandaa ripoti yetu ambayo tulipanga kuiwasilisha katika mkutano huu, ina maana sasa hatuwezi kukutana tena.”

Mkurugenzi wa Huduma za Kamati za Bunge, Athuman Hussein alithibitisha taarifa hizo akisema ni mabadiliko ya kawaida. “Kwani wameondolewa ubunge wao? Kamati bado zipo palepale. Utaratibu ni kwamba kila mbunge anapaswa kuwa katika kamati kwa hiyo ni mabadiliko ya kawaida,” alisema mkurugenzi huyo.

Juhudi za kumpata Ndugai kuzungumzia mabadiliko hayo hazikufanikiwa, lakini wiki iliyopita wakati Mwananchi ilipotaka ufafanuzi wa masuala ambayo CAG ameyeka kwenye ripoti zake kuonyesha Bunge halikuyahoji, Spika alisema hawezi kuzungumza kwa sasa hadi hapo Profesas Assad atakapohojiwa na kamati.

Uamuzi wa kufanya mabadiliko hayo unaweza kuzuia ripoti hizo kujadiliwa hadi baada ya Januari 21, muda ambao Ndugai alisema ataeleza kwa ushahidi jinsi chombo chake kinavyotimiza wajibu wake. Awali ofisi ya Bunge ilitoa ratiba ikionyesha kuwa Mkutano wa 14 umepangwa kuanza Januari 29, na kwamba utatanguliwa na vikao vya kamati, kuanzia januari 14 hadi 27, isipokuwa kwa PAC, LAAC) na Bajeti zitakazoanza Januari 7, 2019.

PAC ilitakiwa ikutane katika Jengo jipya la utawala na wajumbe wake walipaswa kuwasili Jumapili na siku inayofauata wangepokea maelezo ya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) kuhusu miradi iliyokaguliwa na itakayotembelewa na kamati kwa ukaguzi.

Kamati hiyo pia ilipaswa kusafiri jijini Dar es Salaam wakiwa na CAG, Mhasibu Mkuu wa Serikali, Msajili wa Hazina, Kurugenzi ya Usimamizi wa Mali za Serikali (DGAM) pamoja na Kamishina wa Bajeti (CB)

Jijini Dar es Salaam kamati hiyo ingetembelea jengo la tatu la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, mradi wa umeme wa gesi wa Kinyerezi II, miradi ya Shirika la Nyumba (NHC), Bohari ya Dawa (MSD), Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) na kurejea Dodoma ambako wangepata ufafanuzi wa kina wa taarifa za ukaguzi za hesabu za Serikali.

Kamati hiyo ilipaswa pia kuchambua na kujadili taarifa ya hesabu zilizokaguliwa za Shirika la Madini la Taifa (Stamico), kukagua miradi ya Wakala wa Majengo (TBA).

Shughuli nyingine ni kupitia rasimu ya taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya kamati kuhusu uchambuzi wa taarifa ya CAG kuhusu hesabu za Serikali na mashirika ya umma za mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2017

LAAC pia ilipaswa kuanza vikao January 7, katika ukumbi huo ambako pamoja na mambo mengine wangefanya ziara ya kukagua miradi ya maendeleo kwa kutumia mbinu Expenditure Tracking katika Manispaa za zilizo katika Mkoa wa Dar es Salaam (Temeke, Ilala na Kinondoni) kwa mwaka wa fedha 2016/2017 lakini pia kupitia, kuhoji na kujadili hesabu zilizokaguliwa na CAG mwaka 2016/17.

Mjumbe mmoja PAC aachwa

Katika mabadiliko hayo wajumbe wote wa PAC wamepelekwa katika kamati mbalimbali isipokuwa Catherine Ruge Viti Maalumu (Chadema).

Wajumbe wengine wa PAC ni pamoja na Dk Hadji Mponda, Jamal Kassim Ali, Allan Kiula na Aysharose Matembe (Kamati ya Bajeti)

Wengine ni Felister Bura, Omar Kigua, Khadija Nassir Ali na Juma Hamad Omar (Uwekezaji wa Mitaji ya Umma)

Walikwenda Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira wapo pia Stanslaus Mabula, Ali Salim Khamis, Abdalah Haji Ali na Oliver Semuguruka. Wakati Kamati ya Miundombinu wapo pia Dk Shukuru Kawambwa, Mussa Bakari Mbarouk, Hussein Makungu, Hassan Massala na Rhoda Kumchela,

Wajumbe waliopelekwa Kamati ya Katiba na Sheria ni pamoja na Livingstone Lusinde, Anatropia Theonest, Kiswaga Destery na Rashid Shangazi wakati Kamati ya Kilimo, Maji na Mifugo yumo Ignas Malocha, Mariam Kisangi, Maida Abdalah , Josephine Chagula na Joyce Sokombi.

Mwenyekiti Laac azungumza

Alipoulizwa Mwenyekiti wa LAAC Ngomale Mwiru alisema ni kweli wajumbe wa kamati hiyo na yeye mwenyewe wamehamishwa.

“Kamati ni za Spika na mali ya Spika. Kwa nini amefanya hivi mimi sijui,” alisema

Ngomale Mwiru ambaye ni mbunge wa Kilwa Kaskazini (CUF) alipoulizwa hatua hiyo inatokana na nini alisema, “...Sababu CAG alitoa taarifa za kulidharau Bunge.”

Mwananchi lilipotaka kujua, watawasilishaje taarifa ya LAAC bungeni, Mwiru alisema, “Hata sisi hatujui kwani wiki ya kwanza ilikuwa tukutane na halmashauri, wiki nyingine tuandae taarifa, sasa kwa hali hii sijui ngoja tuone itakavyokuwa.”

Mmoja wa wajumbe wa PAC Anatropia Theonest (Chadema) alisema kuwa pamoja na ratiba hiyo kutolewa na Bunge wajumbe wa kamati yake wameshindwa kukutana na badala yake kila mmoja ilimlazimu kuripoti katika kamati mpya aliyopangiwa.

“Hizi taarifa tumeanza kuzipata juzi zimevuruga utaratibu wetu wote sisi kama kamati tulishaandaa ripoti yetu ambayo tulipanga kuiwasilisha katika mkutano huu inamana sasa hatuwezi kukutana tena.”

Kwa mujibu wa Annatropia waliokuwa viongozi wa kamati yake wamepanga kuwa na mkutano leo kuzungumzia muskatabari wa jambo hilo. Badaye jioni Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itikadi na Mambo ya Nje wa Chadema kupitia mitandao ya kijamii alitoa tangazo likionyesha Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni (KUB) watafanya mkutano na waandishi wa habari Katika hotel ya African dream jijini Dodoma.