Taharuki yatanda ofisi za Clouds kifo cha Kibonde

Muktasari:

Kifo cha Kibonde kimetonesha kidonda kibichi katika kampuni ya Clouds Media Group baada ya kuondokewa na watu wawili muhimu ndani ya kipindi kifupi 

Dar/Mwanza.  Kila mfanyakazi katika viunga vya ofisi za Clouds Media Group anaonekana kukumbwa na fadhaa. Ni ngumu kuamini kuwa ndani ya siku 10 wamepokea taarifa za msiba wa watu wawili muhimu kwao.

Mtangazaji Ephraim Kibonde amefariki siku nane baada ya Mkurugenzi wa vipindi na uzalishaji wa kampuni hiyo, Ruge Mutahaba kufariki Februari 26, 2019.

Katika ofisi za Clouds Media group, wafanyakazi wameonekana wamekaa kimafungu sehemu ya kuegesha  magari kila mmoja akiwa na simanzi na wengine wakilia.

Mbali na wafanyakazi, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe naye amefika katika ofisi hizo kuzungumza na wafanyakazi hao ili kujua taratibu zinazofuata.

Wengine waliofika katika ofisi hizo ni watangazaji wa E FM, Maulidi Kitenge, Gerald Hando na Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara.

Ofisa uhusiano wa Clouds Media Group, Saimon Simalenga aliyekuwapo eneo hilo amesema kwa sasa hawezi kusema lolote mpaka watakapokutana na viongozi wengine wa kampuni.

 

Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dk Thomas Rutachunzibwa amesema Kibonde amefariki dunia akiwa njiani kupelekwa katika hospitali ya Rufaa ya Bugando.

Dk Rutachunzibwa imesema Kibonde aliugua ghafla akiwa kwenye mazishi ya Ruge ndipo alipelekwa hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Kagera kisha hospitali ya Uhuru jijini Mwanza.

"Umauti umemkuta leo saa 11:30 alfajiri wakati akipelekwa hospitali ya Rufaa ya Bugando, hivyo hospitali ya Bugando imepokea mwili," amesema

Endeela kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi