Uchaguzi Serikali za mitaa nchini Tanzania kugharimu Sh82 bilioni

Naibu Waziri wa Tamisemi, Mwita Waitara akijibu maswali bungeni katika kikao cha 44 cha mkutano wa Bunge la Bajeti, jijini Dodoma, leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Ikiwa imebaki miezi mitano kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa Serikali za mitaa Oktoba 2019,  Serikali ya Tanzania imesema itatumia Sh82.9 bilioni katika uchaguzi huo.


Dodoma. Serikali ya Tanzania imesema uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika Oktoba, 2019 utagharimu Sh82.9 bilioni huku ikivitoa hofu vyama vya upinzani kuwa utakuwa huru na wa haki.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano Juni 12, 2019 bungeni jijini Dodoma na naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mwita Waitara wakati akijibu swali la mbunge wa Mtambile (CUF), Masoud Abdallah Salim aliyetaka kujua kuhusu maandalizi ya uchaguzi huo.

Katika majibu yake Waitara amesema Serikali imekamilisha maandalizi ya kanuni za uchaguzi zitakazotumika kuendesha uchaguzi huo na kutangaza katika gazeti la Serikali (GN) la Aprili 26, 2019

“Serikali imehakiki maeneo ya utawala na kufanya mafunzo na mikutano kwa wadau wa uchaguzi huo. Pia Serikali inaendelea na maandalizi ya ununuzi wa vifaa vya uchaguzi na imetenga Sh82.9 bilioni kwa ajili ya kuendesha uchaguzi huo,” amesema Waitara.

Katika swali  lake la nyongeza Salim alitaka kujua kauli ya Serikali kuelekea uchaguzi huo kutokana na yaliyojitokeza katika chaguzi zilizopita ambako wagombea wa upinzani walizuiwa kugombea kwa madai kuwa hawana sifa.

Mbunge huyo amesema mkoani Morogoro CCM wameanza kampeni ya Morogoro ya kijani na kufananisha jambo hilo na kuanza kampeni mapema.

Akijibu swali hilo Mwita amesema, “Uchaguzi utakuwa huru na haki na majina ya wapiga kura yatabandikwa vituoni. Nadhani wapinzani mna hofu kwa kuwa mnajua CCM ipo katika nafasi nzuri ya kushinda kutokana na mambo mazuri yanayofanywa na Rais John Magufuli.”

Kuhusu kampeni za Morogoro ya kijani, Waitara amesema huo ni makakati wa chama hicho kupata taarifa za wanachama wake na kwamba hata Chadema nao wana mikutano ya Chadema ni Msingi kwa ajili ya kukutana na wanachama wao.

Mbunge wa Konde (CUF), Khatib Said Haji  naye aliuliza swali la nyongeza akibainisha kuwa CCM ina mbinu nyingi katika uchaguzi na kuhoji kama moja ya mbinu hizo ni wakurugenzi  kutokuwepo ofisini wakati wagombea wa upinzani wakirudisha fomu.

“Mbinu za CCM ni ushindi safi sidhani kama wakurugenzi wanakimbia na ninajua kuwa wagombea wa CCM walikuwa na sifa na kimsingi hakuna mtu aliyekwenda mahakamani na kusema wakurugenzi walikimbia,” amesema Waitara.