Ukusanyaji wa mapato, watendaji wafunguka

Wednesday December 12 2018
pic mapato

Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Deusdedit Kakoko

Dar es Salaam. Baada ya Rais John Magufuli kuzitaja mamlaka kadhaa kuchangia kudumaza mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini hivyo kuzorotesha ukusanyaji mapato, mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Deusdedit Kakoko amesema wadau wake wa karibu wanawapunguzia kasi ya ufanisi.

Akizungumza jana na Mwananchi, Kakoko alisema TPA inatekeleza maagizo ya Rais lakini akazitaka taasisi nyingine zinazohusika bandarini hapo kuboresha utendaji wao.

Katika Bandari ya Dar es Salaam, alisema zipo taasisi 36 za umma na wizara saba jambo ambalo limekuwa likikawiza utoaji wa shehena kwenye bandari hiyo.

Alisema endapo kila mmoja atatekeleza wajibu wake kwa wakati, TPA haiwezi kuzuia mzigo kutoka bandarini kwa kuwa wafanyabiashara ni wadau muhimu wa uchumi wa Taifa.

Alisema tayari hatua zimeanza kuchukuliwa ikiwamo kuzifungia kampuni za uwakala wa forodha zinazochelewesha utoaji wa mizigo kwa makusudi. “Kila mtu akimaliza siku hiyohiyo sisi tunatoa mzigo,” alisema Kakoko.

Licha ya TPA, Rais Magufuli alilitaka Jeshi la Polisi kurekebisha tabia za baadhi ya askari wake ya kuyasimamisha magari yanayoenda nje ya nchi kwa muda mrefu bila sababu.

Advertisement

Vilevile, aliitaka TRA na Wizara ya Fedha na Mipango kubuni vyanzo vipya vya mapato na kuongeza idadi ya walipakodi huku akiliagiza Shirika la Reli (TRC), kuharakisha usafirishaji wa mizigo hasa iendayo nje ya nchi.

Rais Magufuli aliitaka Wizara ya Fedha pamoja na TRA kushirikiana katika kuongeza wigo wa mapato na kubuni vyanzo vipya vya mapato.

Akizungumzia agizo hilo, mkuu wa kitengo cha mawasiliano wa Wizara ya Fedha na Mipango, Benny Mwaipaja alisema watatekeleza maagizo hayo huku akiwataka wananchi kushirikiana na Serikali.

“Tutayafanyia kazi maelekezo yote. Jana kikao kiliendelea kupanga mkakati wa namna ya kufanya. Cha msingi Watanzania walipe kodi na wadai risiti pale wanapofanya ununuzi,” alisema Mwaipaja.

Alisema utayari wa wananchi kulipa kodi utaisaidia Serikali kukamilisha miradi mikubwa ikiwamo ya ujenzi wa reli ya kisasa (SGR).

Msemaji wa Jeshi la Polisi, Ahmed Msangi alisema wanafuatilia maeneo yote nchini na kutoa maelekezo kwa askari.

“Tutafuatilia haya maeneo na kutoa maelekezo ili usafarishaji ufanyike kwa ufanisi zaidi,” alisema Msangi.

Advertisement