Ulinzi mkali kuelekea hukumu ya rufaa ya kina Mbowe

Polisi wakiwa wameimarisha ulinzi katika viwanja vya Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam leo

Muktasari:

Leo Alhamisi, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam itasoma hukumu ya rufaa ya dhamana ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na mhazini wa Bawacha, Esther Matiko

Dar es Salaam. Bado saa moja na dakika kadhaa kufikia muda wa hukumu ya rufaa ya dhamana ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na mhazini wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Esther Matiko, lakini pilikapilika za maandalizi ya usomaji wa hukumu hiyo zimeshapamba moto.

Hukumu hiyo inatarajiwa kusomwa na Jaji Sam Rumanyika leo Alhamisi Machi 7, 2019 muda wa saa saba mchana huu lakini maandalizi ya hukumu hiyo yameanza mapema hususan suala la ulinzi.

Hali ya ulinzi mahakamani hapa imeimarishwa sana kwani kuna askari wengi sana waliotanda sehemu mbalimbali za Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Mwananchi limefika mahakamani hapo saa 4:40 asubuhi na kukuta askari wengi na magari yao ya doria na gari la maji ya kuwasha huku kundi jingine la askari 12 likifanya doria kwa kutembeatembea ng’ambo ya pili ya barabara ya Kivukoni eneo iliko Mahakama Kuu.

Wanachama, wafuasi na wapenzi cha Chadema wanaendelea kuwasili mahakamani hapa kwa ajili ya kufuatilia hukumu hiyo ili kujua hatima ya viongozi wao hao.

Mbowe na Matiko walikata rufaa Mahakama Kuu wakipinga uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwafutia dhamana, kwa sababu za kushindwa kufika mahakamani hapo bila sababu za msingi kwa ajili ya kesi yao ya jinai inayowakabili mahakamani hapo wao na viongozi wengine saba wa chama hicho.

Walifutiwa dhamana hiyo na aliyekuwa Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri Novemba 23, 2018 lakini siku hiyohiyo kupitia kwa wakili wao Peter Kibatala walikata rufaa Mahakama Kuu chini ya hati ya dharura sana wakipinga uamuzi huo.

Rufaa hiyo ilisikilizwa jana na Jaji Rumanyika ambaye baada ya kusikiliza hoja za pande zote alipanga kutoa hukumu yake leo mchana huu.

Endelea kufuatilia Mwananchi kujua kinachojiri