VIDEO: Ndugai alianzisha tena Bungeni

Friday May 17 2019

Dodoma. Mbunge wa Shinyanga Mjini (CCM), Stephen Masele ameibua sintofahamu baada ya kutuhumiwa kugonganisha “mihimili ya nchi na kufanya mambo ya hovyohovyo”na hivyo kusababisha Spika Job Ndugai amuamuru arejee nchini kutoka Afrika Kusini anakohudhuria vikao vya Bunge la Afrika (PAP).

Ndugai, ambaye katika siku za karibuni amekuwa akionyesha ukali dhidi ya wabunge na watu wengine wa nje, alitoa tamko hilo jana baada ya dua ya kuliombea Bunge na Taifa na kuamsha mjadala ndani na nje ya chombo hicho cha kutunga sheria.

Jana bungeni baada ya kumalizika kwa dua ya kuliombea Bunge na Taifa, Spika Ndugai alisimama kutoa taarifa akisema Masele ambaye anahudhuria vikao vya Bunge la Afrika (PAP) nchini Afrika Kusini, amefanya vitendo vya utovu wa kinidhamu.

Akianza kutoa taarifa hiyo, Ndugai alianza kutaja mabunge ambayo Bunge la Tanzania lina wawakilishi wake ambayo ni PAP, Sadc (Sadc PF), African Carribbean Pacific-Europe (ACPEU) na maziwa makuu.

“Wawakilishi hawa tumekuwa tukiwachagua watuwakilishe katika mabunge hayo, nao wamekuwa wakifanya kazi nzuri,” alisema Ndugai.

“Lakini katika uwakilishi wa Bunge la Afrika kumejitokeza matatizo makubwa, hasa kwa Mheshimiwa Stephen Masele. Kuna matatizo makubwa sana ya kinidhamu ambayo nisingependa kuyafafanua leo humu kiasi cha kutosha.

Advertisement

“Lakini tumelazimika kumtafuta Mheshimiwa Masele kumrudisha nyumbani kuanzia Jumatatu, badala yake amekuwa akigoma.

“Hata jana kwenye Bunge hilo clip zinaonyesha zimerushwa baada ya kumwandikia arudi nyumbani ili aje ahudhurie kikao cha maadili hapa, (ameonekana) akilihutubia Bunge lile akisema japo ameitwa na Spika, Waziri Mkuu amemwambia adisregard (apuuze) wito wa Spika na aendelee na mambo yake kule, kitu ambacho ni uongo na kutudhalilisha kama nchi.”

Ndugai alimtuhumu Masele kuwa ni “kiongozi ambaye amekuwa akifanya mambo ya hovyohovyo na ndio maana tumemwita kidogo kwenye Kamati ya Maadili (ili) atufafanuliwe, huenda labda yuko sahihi, lakini kwa mtazamo wetu amekuwa akifanya mambo ambayo ni hatari”.

Ndugai alitaja baadhi ya mambo hayo kuwa ni kugonganisha mihimili ya nchi.

“Anapeleka kwenye muhimili wa Serikali, juu kabisa, maneno mengi ya uongo na ushahidi upo. Ni kiongozi ambaye amejisahau, hajui hata anatafuta kitu gani, ukiacha hizo vurugu ambazo hivi sasa zinaendelea kwenye Bunge ambalo analiongoza, ni kubwa. Hizo hazituhusu.”

“Sasa kwa kuwa tumekuwa tukimwita tangu Jumatatu hataki kurudi, kwa niaba yenu na kwa mamlaka niliyo nayo basi, nimemwandikia barua rais wa PAP ya kusitisha uwakilishi tuliompatia Mheshimiwa Masele katika Bunge la PAP hadi hapo Kamadi ya Maadili na Madaraka ya Bunge itakapokamilisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yake na kukamilisha taarifa yake.”

Ndugai alisema Masele, ambaye alikuwa naibu waziri wa Wizara ya Nishati na Madini katika utawala uliopita, atahojiwa pia na kamati ya maadili ya CCM.

Licha ya agizo la Spika Ndugai la jana asubuhi, Masele, ambaye ni makamu wa rais wa PAP, aliendelea kuongoza vikao vya Bunge hilo.

Ndugai alisema PAP ina vurugu ambazo hakuzitaja, lakini Bunge hilo limepitisha hoja ya kuunda kamati ya kuchunguza tuhuma za unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya rais wake, Roger Nkodo Dang.

Mbali na unyanyasaji wa kijinsia, Dang pia anatuhumiwa kwa upendeleo na matumizi mabaya ya madaraka.

Alipoulizwa na Mwananchi jana, Masele alisema hawezi kusema lolote kwa kuwa hajamsikiliza Ndugai kutokana na kuwa nje ya nchi.

Lakini mbunge mwingine wa PAP, David Silinde, aliiambia Mwananchi akiwa Afrika Kusini kuwa, “Masele hana kosa” na akipinga taarifa ya Ndugai.

“Wiki iliyopita watumishi wa ofisi hii ya PAP hapa Afrika Kusini waligoma kwa sababu walidai kuna unyanyasaji wa kijinsia, upendeleo kwa baadhi ya watumishi unaofanywa na Rais wa PAP,” alisema.

Alisema wanawake kumi walijitokeza kudai kuwa walinyanyaswa kijinsia na Rais, hivyo rais alitakiwa kukaa kando na kikao kikawa kinaendeshwa na Masele ambaye ni Makamu wa Rais.

Alisema Masele kuitikia wito wa kurejea nchini ilikuwa vigumu ndipo alipowasiliana na Waziri Mkuu na kueleza kilichojiri.

“Mimi nitasimama na Masele na hili nitakuwa nalieleza, kwa sababu hakuna utovu wowote alioufanya na kama ameufanya kwa nini asishughulikiwe na kamati za PAP hadi aitwe nyumbani?” alihoji Silinde.

Alisema nchi anayotoka Dang, Cameroon inaweza kutafsiri tukio la Bunge hilo kuwa Tanzania inaendesha siasa chafu PAP hivyo inaweza kuwa sababu ya Spika Ndugai kuagiza Masele arejea nchini.

Advertisement