Waislamu Tanzania watakiwa kuzingatia kauli mbiu ya Mufti Zubeir

Muktasari:

Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) limekuja na kauli mbiu ya jitambue, acha mazoea na badilika katika kuhakikisha waumini wao wanafikia maendeleo wanayotarajia.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) Hamis Mataka amewataka Waislam kutumia kauli mbiu ya Mufti Abubakar Zubeir ya jitambue, acha mazoea na badilika katika kujipatia maendeleo.

Amesema mtu yeyote anayejitambua atamtambua Mwenyezi Mungu na kuwa na hofu naye.

Sheikh Mtaka amesema hayo wakati akishukuru hotuba ya Waziri wa Tamisemi, Seleiman Jafo baada ya kuzungumza katika  Baraza la Eid-El-Adh’aa lililofanyika leo Jumatatu Agosti 12, 2019 Chanika jijini Dar es Salaam.

Pamoja na mambo mengine, Bakwata pia wamefanya dua maalum kwa ajili ya kumuombea Rais wa Tanzania, John Magufuli.

Akizungumza kwenye baraza hilo, Mataka amesema Waislamu Tanzania wanaweza kujipatia maendeleo kupitia michango yao wenyewe kwa kutumia kauli hiyo ya Mufti Zuberi.

“Kujitambua, kubadilika na kuacha mazoea maana yake ni kwamba kumbe Waislamu wa nchi hii kupitia Bakwata wanaweza kujipatia maendeleo kupitia michango yao,” amesema Sheikh Mataka.

Amewataka Waislam kuuanza mwaka mpya wa Kiislam ujao kwa  kupokea mpango wa kupata maendeleo kupitia michango yao.

Awali, Waziri Jafo amesema kauli mbiu ya jitambue, acha mazoea na badilika ndiyo ambayo inatumiwa na Serikali ya awamu ya tano ya Rais John Pombe Magufuli.

Jafo amesema yapo matokeo mabaya ya kumkufuru Mungu na kuwataka Watanzania kumshukuru Mungu kwa neema ya amani iliyopo Tanzania.

“Mungu ametoa majibu ya wazi kuwa ukishukuru unaongezewa, Mungu ametupatia neema Watanzania hivyo tushukuru,” amesema kiongozi huyo wa Tamisemi.

Amempongeza Mufti Zuberi kwa kuwaunganisha Waislamu na kuwataka viongozi wengine wa dini kuendelea kuwaunganisha Watanzania wote huku ajenda kubwa ikiwa amani na utulivu.

Mufti Zuberi amesema katika utendaji kazi wa baraza hilo, kauli ya jitambue, acha mazoea na badilika ndiyo inayotumika kwa sasa huku akiwashauri Waislamu kuwa kitu kimoja kwa kuacha migogoro na migongano.

Amesema msemaji wa Waislamu wote Tanzania ni Bakwata na kuwakumbusha waumini wa dini hiyo kuheshimu baraza hilo.