Zitto: Wananchi Pemba ongezeni nguvu ya kudai mabadiliko

Muktasari:

Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amesema wakati umefika kwa wananchi wa Pemba kuongeza nguvu ya kudai mabadiliko ili kujikwamua kiuchumi.

Pemba. Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amesema wakati umefika kwa wananchi wa Pemba kuongeza nguvu ya kudai mabadiliko ili kujikwamua kiuchumi.

Mbunge huyo wa Kigoma Mjini ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Machi 23, 2019 kisiwani Pemba wakati akizungumza na waliokuwa wanachama wa CUF, ambao sasa wamejiunga na ACT.

Akizungumza katika Wilaya ya Mkoani, Zitto amesema

hali ya maisha ya wananchi wa Pemba ni duni jambo ambalo linapaswa kutazamwa kwa macho mawili na umakini.

Amesema hali hiyo inaweza kubadilika ikiwa watakuwa kitu kimoja na kuunga mkono harakati za ACT.

Amebainisha kuwa hata Ilani ya Uchaguzi ya ACT ya mwaka 2015, iliweka bayana kuunga mkono Rasimu ya Katiba ya Jaji Joseph Warioba wakiamini kuwa suluhisho la kuleta usawa kwa pande zote mbili za muungano za Tanganyika na Zanzibar.

“Pemba ina matatizo mengi lakini kubwa ni ugumu wa maisha,” amesema Zitto.

Kiongozi huyo amesema kwa sasa wanaratibu mkakati maalumu wa kushuka kwenye matawi yote ya chama chao kwa ajili ya kuzungumza na kuwapa misimamo wanachama ili uongozi bora usimame kuanzia kwenye matawi.