Zitto kwenda kumkingia kifua CAG mahakamani

Muktasari:

  • Sakata la CAG na Spika wa Bunge limechukua sura mpya baada ya wabunge kueleza nia ya kulifikisha mahakamani.

Dar es Salaam. Sakata la Spika wa Bunge, Job Ndugai kumuita Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad mbele ya kamati ya maadili limechukua sura mpya baada ya wabunge kujipanga kulifikisha suala hilo mahakamani.

Kiongozi wa Chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe kupitia ukurasa wake wa Twitter    amesema wanalipeleka suala hilo katika ngazi ya mahakama ili kuomba kinga ya CAG, Profesa Mussa Assad. 

Amesema wameona ni muhimu kulifikisha suala hilo mahakamani ili kupinga uamuzi wa Spika Ndugai. 

“Baada ya kushauriana na wanasheria na wabunge tumeona ni muhimu sana kwa maslahi mapana ya nchi yetu kulinda Katiba yetu.”

“Baadhi ya wabunge kutoka vyama vyote tumeamua kwenda mahakamani kuomba tafsiri ya kinga ya CAG kwa mujibu wa Katiba na mamlaka ya Spika kutoa wito kwa CAG,” ameandika Zitto.

Zitto ni mmoja wa wabunge ambao wamekuwa mstari wa mbele kupinga uamuzi wa Spika Ndugai ulipotolewa jana Jumatatu kwa madai kwamba unavunja Katiba na kuingilia uhuru wa Ofisi ya CAG.

Baadhi ya wachangiaji kwenye mtandao huo wameonyesha kuvutiwa na uamuzi huo kwa madai utalinda heshima ya CAG.

Simmy Kyetra ameandika “Kwa hili nawapongeza naona mmeamua kufanya siasa kwa hoja.”

Mwingine Mai Mai ameandika “Good to go but don't politicize it tuweke uzalendo Kwanza na kuweka rekodi sawa. Mambo ya namna hii ingekuwa vizuri kuwa na mahakama ya katiba,” ameandika.

Enock Nkaina amesema, “I second this opinion. Sasa maarifa kama haya tunayapata kwa viongozi wachache sana sio wale wa ndio mzee,”.

Ramadhan Idd ameandika “Hata mimi ninajiuliza hivi Ndugai anaijua Katiba kweli?, haiwezekani na wala haingii akilini kwa Ndugai kumhoji mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali,” ameandika.