Gari la Zari lilivyomponza Q.Boy WCB

Sunday February 23 2020

 

By Nasra Abdallah, Mwananchi. [email protected]

Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) iliyopo chini ya msanii anayefanya vizuri kwa sasa ndani na nje ya nchi, Naseeb Abdul maarufu kwa jina la Diamond, haikuja tu kama uyoga unaojiotea porini.

Kuna watu walikaa na kubuni jina na lebo hiyo, mmoja wapo ni msanii Q Boy Msafi. Msanii huyo anasema kuwa alikutana na Diamond kwa mara ya kwanza mwaka 2010 Diamond alipokwenda kwa mara ya kwanza kufanya shoo nchini Afrika Kusini.

Anasema wakati huo yeye alikuwa huko akifanya kazi ya ubunifu wa mavazi, alimtafuta na walipokutana wakajikuta wanajuana na wazazi wao wanatoka Kigoma, ila walipotezana kwa sababu ya changamoto za maisha.

“Diamond alikuwa analala kwangu kwa kipindi alichokuwa Afrika Kusini, katika mazungumzo tukakubaliana kufanya kazi pamoja.

“Kuanzia hapo nikawa ninamvalisha na tuliwahi kutoa wimbo wa pamoja tuliouweka Facebook kwa sababu mambo ya Instagram na Youtube ilikuwa hayajashika kasi kama sasa, ulikuwa unaitwa ‘Party ya kigeni’.”

Anasema “Nilikuta lebo inaitwa Wasafi Classic Bongo nikaibadili na kuipa jina la Wasafi Classic Baby ili kuweza kusajili kila jinsi ya msanii, majina ya awali niliona kama linawafunga kusajili msanii kutoka mahali pengine nje ya Tanzania,” anasema.

Advertisement

Anasema baadaye Kifesi ndiyo akachora picha ya lebo hiyo kwa sababu alikuwa ndiye mpiga picha wa kwanza wa Diamond na kipindi hicho wasanii waliokuwepo katika lebo hiyo mbali na Diamond na yeye, alikuwepo Harmonize, Queen Darleen na Rayvanny.

Kuhusu kutofautina na WCB hadi kuondoka ni baada ya kwenda kinyume na malengo ya kampuni.

Anasema alikuwa akifanya kazi na WCB kama mtoto wa nyumbani, mwaka 2017 alijisahau kwamba lebo hiyo tayari ina uongozi na inafanya kazi kwa sheria na taratibu walizojiwekea.

Moja ya kosa alilofanya ni kutumia gari la aliyekuwa mpenzi na mzazi mwenzie Diamond, Zari kwa kuruhusu watu kupiga picha na kutangaza biashara zao.

Japo hakujua kama huyo mtu alidhamiria kutangaza hiyo biashara yake, jambo lililomfanya kubananishwa na uongozi akiulizwa amepewa shilingi ngapi hadi kuruhusu mtu kujitangaza na gari hilo.

Katika tangazo hilo, mtu huyo alienda mbali na kuandika kwenye mitandao kuwa ‘Mama Diamond amepita eneo hilo kuchukua bidhaa wewe unasubiri nini?”.

“Pia nilikuwa nikiwasapoti baadhi ya wasanii bila kushirikisha uongozi, jambo ambalo walihofia huenda baadaye wasanii hao wakajitangaza wamesajiliwa WCB halafu ikawachafulia jina lao.

“Japo yote nilikuwa nayafanya kwa mapenzi yangu, sikujua kuwa ina athari kwa lebo kwani kila kitu nilikuwa nachukulia poa,” anasema.

Baada ya kukutwa na makosa mbalimbali yakiwemo hayo, uongozi ulimtaka apumzike wiki mbili lakini alipotafuatwa na waandishi kuhojiwa kisa cha kufukuzwa kwake WCB.

Anasema alijikuta akiropoka na kulaumu uongozi kumfukuza licha ya mchango wake katika lebo hiyo.

“Lakini katika hili nilijifunza kwamba hata kama umetendewa ubaya na mtu au watu, inakuhitaji kuchukua muda kutafakari kosa ulilolifanya japo malalamiko mengine niliyokuwa nayatoa yalikuwa na ukweli lakini haikuwa wakati sahihi kusema,” anasema.

Kuanzia hapo akaamua kuendelea na maisha yake ikiwemo kurudi Afrika Kusini kuendelea na shughuli za ubunifu mavazi.

Hata hivyo anasema pamoja na yote anashukuru katika kutimiza miaka 10 ya Diamond katika muziki alikumbukwa kwa kualikwa.

Anasema kwa sasa wapo vizuri na wamekuwa wakishauriana mambo mbalimbali jambo ambalo pia Meneja wa WCB, Babu Tale anakiri na kuongeza kuwa hata makosa aliyoyaeleza baadhi yana ukweli likiwemo hilo la gari ya Zari.

Advertisement