Hivi hapa vipaumbele vya wadau bajeti ya elimu 2019/2020

Tuesday April 30 2019
pic vipaumbele

Jana Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amewasilisha bungeni mapendekezo ya matumizi na mapato ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2019/2020.

Ni hotuba ambayo wadau mbalimbali mbali wa elimu walikuwa wakiisubiri hasa wakitaraji kuona kama imegusia mambo wanayofikiri ni ya kipaumbele katika sekta ya elimu.

Wadau hao wamezungumza na Mwananchi wakielezea mambo ambayo wabunge wanapaswa kuyatilia maanani wakati wa mjadala wa hotuba hiyo unaotarajiwa kuanza leo bungeni jijini Dodoma.

Baadhi ya mambo muhimu yanayotajwa na wadau ni kuongezeka fedha za ruzuku kwenye elimu bila malipo, maslahi ya walimu, miundo mbinu shuleni na bajeti ya watoto wa kike.

Miundombinu shuleni

Mchambuzi wa bajeti kutoka Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) Godfrey Chambua anasema miundombinu shuleni ni kati ya vipaumbele muhimu 2019/2020.

Advertisement

Miundombinu hiyo ni pamoja na ujenzi wa madarasa ya kutosha, matundu vya vyoo kulimgana na uwiano wa kisera, upatikanaji wa maji, ujenzi wa hosteli na nyumba za walimu.

Mkurugenzi wa Shirika la Furaha Pamoja Foundation, John Paul anasema bajeti hiyo pia lazima izingatie miundombinu inayokidhi mahitaji ya wanafunzi wenye ulemavu.

“Mfano madarasani, lazima miundombinu iwezeshe wanafunzi wenye ulemavu kusoma bila wasiwasi wowote,” anasema na kuongeza:

“Watoto wasioona wana mahitaji tofauti na wasiosikia, wasio sikia wana mahitaji tofauti na walemavu wa viungo, kwa hiyo Serikali isisahau kundi hili muhimu hasa wakati huu tunapotekeleza sera ya elimu jumuishi.”

Anasema miundombinu imara shuleni lazima iende sambamna vifaa vya kujifunzia na kufundishia.

“Vitabu vya uhakika vinavyoendana na uwiano wa wanafunzi darasani ni jambo la msingi. Hata kama miundombinu itakuwa imara kama hakuna vitendea kazi ni bure,” anasisitiza Paul

Ujenzi wa hosteli

Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali linalojihusisha na Masuala ya Kisaikolojia kwa Watoto (REPPSI) Edwick Mapalala anasema lazima Serikali itenge bajeti kwa ajili ya ujenzi wa hosteli kwenye shule za kata ambazo zimeenea karibu kila kona ya nchi.

Anasema wakati wa kampeni yao ya kupambana na mimba shuleni walibaini wanafunzi wengi wanaishi kwenye vyumba vya kupanga ‘geto’ na wengine wanatembea umbali mrefu jambo ambalo ni hatari.

“Kwa hiyo wizara ione umuhimu wa kuhakikisha watoto wanaishi shuleni kuliko kwenye vyumba walivyopanga, kwa sababu huko ni hatari na nia yetu ni kuona wanasoma na kufikia ndoto zao. Bajeti ya kutosha kwenye eneo hili ni muhimu,” anasema Mapalala.

Maslahi ya walimu

Mapalala anasema eneo jingine muhimu ni kwenye maslahi ya walimu.

“Ili walimu waweza kufundisha watoto na kupunguza ukatili shuleni wanatakiwa kuboreshewa maslahi yao. Walau Serikali ione uwezekano wa kutenga bajeti kwa ajili ya motisha,” anasema.

Kwa upande wake, Paul anasema bajeti ikizingatia maslahi ya walimu wataweza kufundisha vizuri zaidi, kwa sababu hawatakuwa na msongo wa mawazo ya ugumu wa maisha.

“Akiwa darasani mwalimu atamuwaza mwanafunzi wake tu hato waza mambo mengine kwa hiyo maslahi ya walimu ni eneo nyeti,” anasisitiza.

Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TenMet) Cathleen Sekwao anasema jambo jingine muhimu katika bajeti hiyo ni kuwekeza katika elimu ya ualimu kwa kutumia mbinu za kisasa na jumuishi tena kwa lugha zote mbili yaani Kiswahili na Kiingereza.

Bajeti ya elimu ya watoto wa kike

Kwa sababu wasichana ndio waathirika wa mazingira duni shuleni, Chambua anakumbusha bajeti hiyo kujali suala la taulo za kike kwa wanafunzi wa ike.

Anasema kwa sababu baadhi yao hushindwa kumudu masomo siku za hedhi kwa kukosa vifaa hivyo, ni muhimu Serikali ione uwezekano wa wanafunzi wa kike kuzipata bure.

Pia, anasema wanafunzi wa kike lazima waandaliwe chumba maalum cha kujisitiri wakati wa hedhi tofauti na sasa ambapo wasichana wengi hutumia vyoo vya pamoja.

Ruzuku kwa wanafunzi

Paul anashauri fedha za ruzuku ya wanafunzi ziongezwe kutoka Sh10,000 ya mwanafunzi wa shule ya msingi sasa mpaka Sh15,000 hadi 20,000 na Sh50,000 kwa kila mwanafunzi wa sekondari badala ya Sh25,000 ya sasa. Anasema fedha za ruzuku zikitosheleza mahitaji shuleni kiwango cha kujifunza kitaongezeka.

Motisha kwa walimu

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa (UoI) Dk Jimson Sanga anasema motisha kwa walimu ina nguvu na inaweza kuongeza ufaulu kwa shule za umma.

Anasema wakati Srikali itakapotenga bajeti, isisahau suala la motisha kwa walimu hasa wakati huu wa elimu bila malipo.

“Kutokuwa na bajeti ya motisha kwa walimu katika shule za msingi na sekondari kunaweza kuchangia matokeo mabovu, walimu wakipata motisha watakuwa na ari ya kufundisha,” anasema Dk Sanga.

Anasema siri ya shule binafsi kufaulisha kwa kiwango cha juu ni mazingira mazuri ya kufundishia ikiwamo motisha kwa walimu.

“Tukitaka shule zetu za umma ziingie kumi bora lazima walimu wapewe kipaumbele na watakumbukwa kuanzia kwenye bajeti,” anasema .

Advertisement