Mapambano kukomesha vifo vya uzazi bado yanahitajika

Kila mtu ana wajibu wa kushiriki vita ya kukomesha vifo vya wajawazito na watoto vitokanavyo na uzazi usio salama.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani (Unicef), Tanzania ni nchi ya tisa, kati ya kumi zinazoongoza katika vifo vya watoto.

Mtaalamu wa mawasiliano kutoka Unicef, Tahseen Lama anasema Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na wadau, imefanya vizuri katika miaka 10 iliyopita ya kuokoa vifo vya mama na mtoto, hasa katika eneo la chanjo.

Usia Nkoma ambaye pia ni mtaalamu wa mawasiliano wa Unicef, anasema licha ya jitihada kubwa zinazofanywa, zikiwamo za ujenzi wa hospitali, zahanati, vituo vya afya, vifaa tiba na vitendea kazi zikiwamo gari za kubebea wagonjwa, bado jitihada za makusudi kwa kila mmoja zinahitajika, kwa kubeba ajenda ya kupunguza ‘vifo vya wajawazito na watoto wachanga’ katika kila vikao vyao.

Jambo linalotia moyo, Nkoma anasema ajenda ya kupunguza vifo hivi inawezekana ikiwa kila mtu anashiriki katika kampeni hii.

Ili kuendana sambamba na mikakati ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ya kutaka kila mtu ashiriki katika kampeni ya ‘Jiongeze Tuwavushe Salama’ Kampuni ya True Vision Production (TVP), kwa kushirikiana na Unicef Tanzania na Wizara ya Afya, waliandaa semina kwa wahariri, viongozi wa dini na waandishi wa habari ili kutoa elimu na kuhamasisha jitihada za kupunguza vifo vya wajawazito na watoto nchini.

Nkoma anawataka waandishi kutumia kalamu zao kuchochea habari zinazowahusu wajamzito na mtoto mchanga ili kupunguza vifo vyao visivyo vya lazima.

“Kwa kufanya hivyo, watunga sera na watendaji watachukua hatua za haraka. Mbali na vyombo vya habari mnavyoviongoza na waumini wenu, pia nawaomba mtumie akaunti zenu binafsi za mitandao ya jamii kuwa sehemu ya kampeni ya kuzuia vifo zinavyotokea hapa nchini.”

Nkoma anasema kutokana na takwimu kuonyesha vifo vipo juu, Unicef Tanzania inashirikiana na wadau , ikiwemo serikali, taasisi na mashirika katika kuhakikisha mama na mtoto wanavuka salama katika kipindi cha uzazi.

“Ndio maana tunashiriki katika kusaidia uboreshwaji wa huduma za afya, vifaa tiba na kutoa misaada ya magari ya kubebea wagonjwa (ambulances) katika kukabili vifo hivi, ambazo sasa inapaswa kuwa ajenda ya kitaifa,”anasema Nkoma.

Kwa mujibu wa takwimu za Serikali, katika kila vizazi hai 100,000 wajawazito 556 hufariki dunia wakati wa kujifungua, lengo likiwa ni kufikisha vifo 292 mwaka 2020.

Agnes Mgaya, Kaimu Mratibu wa Huduma ya Afya ya Mama na Mtoto Mkoa wa Dar es Salaam, anataja sababu zinazosababisha vifo vitokanavyo na uzazi nchini kuwa ni kutokwa na damu nyingi kabla, wakati na baada ya kujifungua, kifafa cha mimba, kuharibika kwa mimba, uchungu pingamizi, uambukizo, upungufu wa damu, Ukimwi na Malaria.

Mgaya anasema elimu ya afya ya uzazi ni muhimu ikatolewa kwa mjamzito na mwenza wake ili kuhudhuria kliniki kabla na baada ya kujifungua.

Mgaya anasema mjamzito anatakiwa kuhudhuria kliniki si chini ya mara nne, au zaidi ya hapo pale atakapotakiwa na wataalam wa afya kulingana na hali yake.

“Lakini, wengi wanahudhuria kliniki mwanzoni tu (tofauti na inavyotakiwa), wanawake wajawazito wanaohudhuria kliniki mara nne kama inavyotakiwa ni asilimia 50 tu, lengo ni kuwashawishi walau wafikie asilimia 80 ifikapo mwakani, kama malengo ya kampeni ya ‘Jiongeze Tuwavushe Salama’ yanavyosema.”

Mgaya anatoa sababu ya mahudhurio hafifu kliniki kuwa ni umbali wa baadhi ya vituo vya afya, hali duni ya miasha, ukosefu wa elimu ya afya ya uzazi, mila na desturi potofu zinazochochea wanawake kukosa uamuzi wakisubiri waume au wake zao waamue.

Orsolina Tolage kutoka kitengo cha elimu kwa umma (Wizara ya Afya), anasema wanahabari wana wajibu wa kuelimisha jamii, kutumia kalamu zao kuelezea umuhimu wa kwenda kliniki wakati wa ujauzito na baada ya kujifungua.

“Muhimu ni kuhakikisha ndani ya siku 42 baada ya kujifungua, mama aendelee kuwa chini ya uangalizi wa wataalamu wa afya ili wakabiliane na changamoto zinazoweza kujitokeza kama vile kifafa cha mimba,’ anasema Tolage.

Wanahabari wazungumza

Mhariri, Lilian Timbuka amewataka waandishi kufuatilia kwa karibu masuala yanayohusu afya ya wajawazito na watoto ili kuibua hoja zitakazosaidia kupunguza vifo vyao.

Mhariri mwingine, Neville Meena ameshauri kuwe na mafunzo ya mara kwa mara kwa wadau wa habari, wauguzi na madaktari ikiwa sehemu ya kukumbushana wajibu wa kumsaidia mjamzito na mtoto mchanga.

Mmoja wa wakongwe katika tasnia ya habari, Theophil Makunga anasema takwimu za vifo vya wajawazito na watoto zinatisha, hivyo ni muhimu waandishi wakatumia kalamu zao kuhakikisha vifo hivyo havitokei. “Wajibu wa waandishi siyo tu kuandika habari mbaya, bali pia wana wajibu wa kuandika habari zinazohusu maendeleo ya jamii na kutoa suluhisho la matatizo yanayojitokeza ili hatua zichukuliwe na jamii, watendaji na watunga sera,” anasema.

Kampeni ya Jiongeze Tuwavushe Salama ni ya Taifa na ilizinduliwa na makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan mjini Dodoma, Novemba mwaka jana. Lengo ni kuchukua hatua za kuzuia vifo vya mama na mtoto nchini.