Mjane aliyepania kujikomboa kwa kilimo cha kisasa

Muktasari:

Anasema kipato chake kinatokana na kilimo ambacho hata enzi za uhai wa mumewe aliyeitwa Gadalia John walikuwa wanashirikiana kulima mashamba wakipanda mazao ya aina mbalimbali lakini zaidi mahindi.

Julieth Sembuche ni mjane anayeishi katika kijiji cha Yameni kilichopo katika Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro. Ni miaka minne sasa tangu mumewe afariki dunia Machi mosi 2012 na kubadili kabisa mfumo wa maisha katika familia yake.

Anasema kipato chake kinatokana na kilimo ambacho hata enzi za uhai wa mumewe aliyeitwa Gadalia John walikuwa wanashirikiana kulima mashamba wakipanda mazao ya aina mbalimbali lakini zaidi mahindi.

“Wawili ni wawili huu msemo una maana kubwa kwangu kwa sababu nilikuja kuutambua maana yake baada ya mume wangu kufa kwani nilijikuta napoteza mwelekeo kwa muda, lakini nilikumbuka kusali hatimaye.

Sembuche anasema Pia hali ya hewa iliyojitokeza mwaka jana ilikuwa ni changamoto kubwa katika maisha yake.

“ Mimi nina watoto watatu wawili ndiyo wanafamilia zao mmoja naishi naye, mwaka jana nilijikuta nateswa na njaa kutokana, nilikunywa maji mengi na mapera, wakati mwingine wanangu walinitumia msaada lakini kwa sababu nao wana kipato kidogo ilikuwa ni msaada wa siku chache tu,” anasema Sembuche.

Anasema bahati nzuri baada ya kukumbana na changamoto hizo alipata nafasi ya kuwa miongoni mwa walima 40 katika kijiji chao waliochaguliwa kupata mafunzo ya kilimo bora, ambayo yaliotolewa na Usharika wa wajasiriamali wahitimu wa Chuo cha Kilimo cha Sokoine (Sugeco).

“Mafunzo hayo yaliweka nuru mpya kwenye maisha yangu, kwa sababu awali tulipokuwa tunalima na mume wangu enzi za uhai wake tulilima kienyeji, tulikuwa tunalima hata hekari mbili na kupanda mahindi lakini tunavuna magunia manane au kumi, lakini baada ya mafunzo hayo nimeona maajabu,” anasema.

Anamtaja mwalimu wake wa kilimo cha kisasa kuwa ni Baraka Messu ambaye ni Ofisa kilimo kutoka Sugeco, kwamba aliwaeleza pamoja na wakulima wenzake kuwa wanapaswa kulima kwa kuhakikisha wanapata faida na siyo kupoteza nguvu.

“Mwalimu Baraka alijaza ujasiri kwamba kilimo ni fedha na sivyo tulivyokifikiri awali, kwamba tunapaswa kuzingatia kanuni 10 za kilimo bora, ambazo ni kuandaa shamba mapema, kuwa na mbegu mbolea, kupanda kwa mstari, kuweka mbolea, kupalilia, kuweka dawa, kuvuna kwa wakati na kuhifadhi sehemu salama,” anasema.

Sembuche baada ya mafunzo hayo walipewa kilio 2.5 za mbegu bora ya mahindi lishe ambayo yana rangi ya njano, na kuelekezwa namna ya kupanda kwenye shamba lenye ukubwa wa robo ekari.

“Nikalima kwa kufuata maelekezo hayo, kwa hakika sasa nimeamini kilimo cha kisasa kina faida kwani nimevuna magunia saba ya mahindi hayo ambayo tumejulishwa hata bei yake sokoni ni tofauti na mahindi ya kawaida kwamba kilo ni kati ya Sh 1,800 hadi 2,000,” anasema.

Anabainisha kuwa amekusudia kuhifadhi baadhi ya mahindi hayo kwa akiba ya chakula na mengine anatarajia kuyauza ili kupata fedha atakazotumia katika kununua mbegu nyingine ya mahindi hayo pamoja na mbolea alime ekari zaidi ya tatu akiamini kwamba kilimo cha zao hilo kutamkomboa kiuchumi.