Breaking News

NDANI YA BOKSI: Mondi dizaini kama katuzoea sana hivi...

Sunday January 12 2020

 

Miaka kumi iliyopita Mondi aliingia rasmi kwenye ‘gemu’ la ushindani. Ni kama alikuwa anakuja na kupita kama wengi walivyopita. Kwa mwonekano wake, kile alichoimba na yote yaliyoendelea mwanzo wa safari yake. Ulihitaji akili flani ya kiwendawazimu kuamini kuwa angekuwa pale alipo leo. ‘Nenda Kamwambie’ ndo ngoma yake kubwa ya kwanza. Kwa ile ngoma unaanzaje kutabiri kuwa yule cha upepo (kimbaumbau) Atakuja kuwa huyu unayemuona leo? Ilikuwa ngumu.

Mungu angetupa uwezo wa kujua mbele ya mtu angeanza kuombwa ajira miaka 10 iliyopita. Huyu dogo ndo maana halisi ya msela mchakarikaji. Dogo anasaka pesa kwa kasi kuliko kuandika mashairi ukipiga hesabu za haraka mkwanja anaoingiza kwa sasa hauendeni na anachofanya kwenye muziki.

Ashajivua kabisa akili na hulka za Tandale. Ni yule yule kimwili na rangi si akili. Mondi wa sasa anaandika zaidi sahihi yake kwenye ‘cheki’ kuliko mashairi ya ngoma zake.

Huku alikofikia wengi hawakufika. Sugu na Profesa Jay hawakufika kwa wakati wao ingawa wao ndo mabingwa waonyesha njia hii anayopita Mondi. Na wao si kwamba hawakutaka au walikuwa wazembe hapana! Mazingira hayakuwa rafiki.

Muziki na tuzo mbalimbali, kila siku yeye tu tunamuona. Kifupi hii leo kumlinganisha na mwingine unahitaji roho ya kijasiri iliyokosa aibu, haya, soni na staha. Dogo yuko juu mno. Niliwahi kuandika hapa. Kwamba neno Bongofleva linafutwa na Wasafi. Wao ndo wanaosikika zaidi ya neno Bongofleva.

Hiki kitu hakina afya kwa muziki wetu. Lakini afanyaje kama wengine wako ‘bize’ kulelewa na totozi? Wamemuacha peke yake afanye atakalo, apendalo na analotamani. Ndio maana wenye akili tulifurahia Konde Boy kusepa WCB. Bongofleva ni muhimu kuliko WCB.

Advertisement

Furaha yetu si kuondoka kwake WCB. Maana WCB ilipofikia hata Mondi akisepa itabaki kuwa na nguvu. Furaha yetu ni kuona WCB zinakuwepo nyingi. Haivutii mtu mmoja tu kumiliki kila kitu kwenye ‘indastri’. Ili ujue Mondi yuko mbali imebidi mbavu yake moja (Harmo) ijitenge na kiwiliwili chake kwenda kuleta ushindani nje ya WCB. Hii si picha nzuri kwa taswira ya muziki na sanaa.

Hii ina maana waliokuwa nje ya WCB walishindwa kuleta ‘bato’ lenye kujenga. Sasa tuzo za ndani zimekufa kifo cha mende, zimebaki za kimataifa tu ambazo Nandy alifurukuta kidogo akabeba moja huko Nigeria, lakini hakukuwa na mwendelezo. Lakini sasa Mondi kaachwa atambe. Na anatamba kweli, kila ‘dili’ kubwa la shoo anatazamwa yeye kwanza. Ukimfuatilia vizuri nyendo zake utagundua hakuna uchawi bora duniani kama juhudi. Huu uchawi utauona kwenye kichwa cha Mondi, miguu ya kina Samatta na Msuva.

Tunguri haziwezi kukupa kiboya mchongo mkubwa kama ule wa kutumbuiza tuzo za CAF. Wakati Sadio Mane anabeba tuzo ya mchezaji bora Afrika jukwaani alikuwepo Mondi akiburudisha akili kubwa zenye rangi mchanganyiko toka mataifa mbalimbali.

Tulizoea kuwaona kina Koffi Olomide, Yoùssur Ndur, Angelina Kidjo, Oliver Mtukudzi (RIP) wakipewa haya mashavu. Wakati ndoto ya Mondi ilikuwa kutumbuiza jukwaa la Fiesta kukaa ‘back stage’ na Ferouz, kuhug na FA, kupeana namba na Lady Jaydee, kupiga stori na TID na Chillah, leo hii juhudi zake zimepelekea awe na Fiesta yake (Wasafi Festival). Kutoka ndoto ya kukaa ‘back stage’ na Ferouz hadi kumpa nafasi Ferouz kupanda jukwaani na kumlipa. Kwa lugha ya wahuni wa soka wangesema ‘Come Back’ ya hatari. Mondi ndo maana halisi ya upepo wa kisulisuli. Amekuja kama upepo, akabeba kila kitu.

Dogo kila siku utadhani ndo anatoka kisanii. Hasira za ‘gemu la muziki’ hazijawahi kuisha kichwani mwake utadhani liliua ndugu zake na kumtenganisha nao. Kumbe kishaona maisha ndo haya na pesa ipo hapa hataki kupoteza pointi na kamwe hataki kuwa nyuma ya wenzake. Kwa mwanamuziki mwingine angemdharau Harmonize kijana aliyemtoa mwenyewe. Dogo anayeiga swaga na sauti yake. Kwa nini amuhofie? Amemzidi pesa, umri, ukubwa wa jina, wingi wa marafiki mpaka idadi ya madem na watoto. Lakini Mondi hajatazama yote hayo kakaza kama kawaida. Na ukiangalia mchezo unavyoenda unaona kabisa anaheshimu uwepo wa Konde Boy. Hiki kitu alikikosa Alikiba. Wakati Mondi anahaha kuwa kama Ali.

Mwenyewe alikuwa anadharau ni kama alipuuza uwepo na juhudi za Mondi kutaka kuwa kama yeye. Angetumia fujo za Mondi kama kichocheo cha kukaza kwenye ‘gemu’. Hii leo tungekuwa tunaongea lugha nyingine. Yeye Kiba akaacha mashabiki ndo wapambane na presha za Mondi. Nini kinaendelea sasa? Mondi alianza kwa kutamani kuwa Kiba akawa anaandika ngoma kama ‘Ukimuona’, ‘Kizaizai’, ‘Mawazo’, ‘Nitarejea’, ‘Mbagala’, ‘Nenda Kamwambie’ hazikuwa nyimbo za polepole. Mondi alisoma kinachofanywa na wasanii aliotamani kuwa kama wao, akaona wana udhaifu wa kutawala jukwaa. Hapo ndipo alipopiga bao. Uwepo wa Mose Iyobo kando yake haikuwa bahati mbaya alijua umuhimu wake katika juhudi za kuwa juu.

Kutoka ndoto ya kuwa kama wao hadi juhudi zikamkutanisha na Davido shughuli ikaishia hapo. Upinzani ukabaki kwenye mitaa ya Kino na Ilala kama si Kimara. Mondi akawa mkubwa anayepata taabu na kelele za mashabiki kuliko muziki wa wasanii waliotangulia na kuwa na majina kabla ya ujio wake. Waliacha lango wazi wakiishi Kimwinyi.

Walichelewa kuelewa akili kubwa ya biashara ya muziki kwenye kichwa cha Mondi. Kama utakuwa unawafuatilia wasanii walioanza kabla ya Mondi wanafanya vitu ambavyo alishavifanya huko nyuma. Kulikuwa na waimbaji wazuri, yeye akawa mtumbuizaji mzuri sasa wanajitahidi na wao wawe watumbuizaji huku wakijaribu kuimba laivu. Tukiwa wakweli Mondi wa sasa si yule wa hapo nyuma. Yule ambayo fujo zake za jukwaani zilimpa wakati mgumu Kifesi kupata picha zake. Mondi alikuwa mnyama jukwaani, alikuwa katili sana jukwaani. Huyu wa sasa sawa, ila Mondi yule alikuwa sawa zaidi. Wakati zamani Mondi alikaza studio. Alitisha kwenye kichupa na kuleta balaa jukwaani. Mondi wa sasa anatisha kwenye kichupa analegeza studio kwa kuimba vitu vyepesi sana. Hili la kuimba vitu vyepesi vyepesi yuko sahihi, muziki wa sasa ndo unataka mambo hayo. Mondi wa sasa ni ‘intaneshino’ hawaimbii watu wa Kawe na Tegeta muziki wake unaenda kwenye vichwa vinavyohitaji fleva zaidi ya ujumbe. Yes! Lakini pamoja na yote hayo Mondi wa sasa katuzoea ameshatuchukulia poa washikaji. ‘Intaneshino’ sawa lakini kuna kitu tunakosa kutoka kwake. Mondi yule wa ‘kolabo’ la hatari na Mose Iyobo kiasi cha staili zao kuwavuruga watoto Uswahilini. Tunataka kuona Ngololo lingine. Si hizi za mikato ya kufanana sana na wadwanzi wa Lagos. Imekuwa ‘tuu machi’ ziwepo nyimbo kwa ajili ya kimataifa na ziwepo ‘Ukimuona’ kwa ajili yetu wakazi wa Kijitonyama. Mondi wa sasa anafanya ‘vesi’ nyepesi. Anatupia mitandaoni picha nyepesi. Ana skendo nyepesi sana. Hata jukwaani hasa akitutumbuiza sisi kawa mwepesi sana. Mondi usituzoee kihivyo. Hebu kuwa muungwana kidogo. Piga ngoma zako kwa ajili ya watu wa Ethiopia na kwingine kama Togo lakini kuna mikato yetu ile ya ‘Nataka Kulewa’. Zile za ‘Sikomi’ ambazo wenyewe tunazijua na unaowachana kwenye ‘vesi’ tunaishi nao kitaa. Ukiwa ‘homu’ usitupigie ‘shoo’ za ‘kiloko’ sana huku ndiko ulikoanzia kupata mkwanja uliomlipa Davido ili ugonge naye lile ‘kolabo’ la karne. Piga madude kama yale ya kutua na helkopta pale Dar Live. Na sisi tunataka burudani zile zilizofanya Kifesi akupige picha ukiwa umebinuka sarakasi jukwaani kwa mkono mmoja. Mondi usituzoee kihivyo sisi.

Advertisement