Nchi za Afrika Mashariki kubadilishana wataalamu wa Kiswahili

Tuesday April 16 2019

Katibu Mtendaji wa kamisheni hiyo, Profesa

Katibu Mtendaji wa kamisheni hiyo, Profesa Kenneth Simala 

By Gadi Solomon,Mwananchi [email protected]

Ili kuhakikisha utangamano kwa wananchi wa Jumuiya ya Mashariki unaimarika kupitia matumizi ya lugha ya Kiswahili, Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki (Kakama), imeanzisha mpango endelevu wa mafunzo wa kubadilishana wataalamu utakaowanufaisha wananchi wa nchi wanachama jumuiya hiyo.

Katibu Mtendaji wa kamisheni hiyo, Profesa Kenneth Simala alisema mpango huo wa kubadilisha wataalamu, umelenga kuwaunganisha wananchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kuleta utangamano.

Alisema mpango huo unawahusisha wanafunzi wa vyuo vikuu, wafanyakazi katika vyombo vya habari na wadau wanaofanya kazi kwenye taasisi zinazofungana na Kiswahili jambo ambalo litawaongeza ufanisi kwenye taaluma zao na kuongeza utangamano kwa wananchi wa jumuiya.

Alisema muombaji atafanya maombi ya kwenda nchi yoyote kujifunza katika taasisi inayohusiana na tasnia aliyopo alimradi tasnia hiyo iwe na uhusiano na lugha ya Kiswahili.

Anasema tayari wameshazungumza na baadhi ya taasisi za vyombo vya habari kuwapokea waombaji watakaohitaji nafasi ya kwenda kujifunza.

Hapa nchini wameshazungumza na wadau kutoka Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) na Kenya wamewasiliana na KTN ili waweze kuwapokea waombaji.

“Natoa wito kwa vyombo vya habari na taasisi zingine kuwapokea waombaji watakaochaguliwa na kamisheni ili kwenda kutangamana na wenzao wa Jumuiya ya Afrika Mashariki,” anasema Profesa Simala.

Wadau wauzungumzia mpango

Mhadhiri wa Kiswahili Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Titus Mpemba anasema mpango wa kubadilishana wataalamu unaoratibiwa na Kakama unatoa fursa kwa wadau kutagusana na kuwa na mitandao ya uhusiano pamoja na mawasiliano.

Anasema, Mtanzania akienda Rwanda ataweza kufahamiana na watu ambao awali hakuwa anawafahamu kabisa hapo awali. Kufahamiana huko kutawafungulia mianya ya kufanya na kufanya nao shughuli mbalimbali za kitaaluma kama vile utafiti na hata kupata mahali pa kwenda likizo kunoa bongo.

“Naona kwamba hiyo ni fursa nyingine kwa wanataaluma kuchangamana na watu wengine ambao wanaweza kuwaalika kwenye makongamano kuhusu Kiswahili, jambo ambalo kwa namna moja au nyingine litarahisisha wigo wa kuwa na wadau wa lugha kimataifa,’’ anasema na kuongeza kuwa mpango huo pia unaweza kuwa fursa nzuri ya kukuza soko la vitabu hasa vile vya kitaaluma.

Mpemba ambaye pia alikuwa alikuwa miongoni mwa walimu walioanzisha darasa la Kiswahili nchini Zimbabwe, anasema matarajio yake mpango huo uweke mkazo pia uandishi wa vitabu vya Kiswahili kutokana na kuwa na uhaba mkubwa wa vitabu hivyo shuleni, vyuoni hata ughaibuni.

Mathalani anasema kwenye kozi za uandishi, vitabu vinavyotumika ni vile ambavyo vimeandikwa kwa lugha ya Kiingereza huku athari za shughuli za ziara za kimasomo ni za muda mfupi kuliko maandiko ambayo yanadumu kwa muda mrefu.

Hata hivyo, Mpemba ana wasiwasi kama anavyosema: ‘’Nimekuwa najiuliza kuna vigezo vimetajwa kimojawapo ni mwanachama hai anayejihusisha na masuala ya maendeleo ya Kiswahili na Kamisheni ya Jumuiya ya Afrika Mashariki lakini hilo linapaswa kutolewa ufafanauzi ili watu wengi zaidi waweze kuulewa mpango hu.’’

Advertisement