Sylivia Kaindoa muuguzi jasiri aliyegeuka mlezi wodini

Muktasari:

Kaindoa anakumbuka zaidi kwamba Renata alifikishwa katika kituo cha matunzo ya watoto njiti maarufu ‘Kangaroo Mother Care’ (KMC) kilichopo katika Hospitali hiyo wakati akiwa na umri wa siku moja kwa ajili ya huduma kubwa zaidi ya kitaalamu mwaka 2018.

Mbali na kuhudumia wagonjwa katika kitengo cha huduma ya mama, baba na mtoto (RCH) katika Hospitali ya Mugana, Sylivia Kaindoa anasimamia malezi ya mtoto aliyetelekezwa (Renata) ambaye mama yake alifariki mara baada ya kujifungua akiwa na ujauzito wa miezi nane.

Kaindoa muuguzi mwenye umri wa miaka 38 mama wa watoto wawili anayeishi Mugana, mji mdogo uliopo mkoani Kagera anasema Renata, ambaye sasa ana mwaka mmoja, alizaliwa njiti akiwa na uzito wa kilogramu 1.8.

Kwa kawaida mtoto akizaliwa chini ya uzito wa kilogramu 2.5 huhesabiwa amezaliwa chini ya uzito wa kawaida. Watoto wenye uzito wa chini ya kilogramu 1.5 wakati wa kuzaliwa huchukuliwa kuwa chini ya uzito wa kawaida.

Kaindoa anakumbuka zaidi kwamba Renata alifikishwa katika kituo cha matunzo ya watoto njiti maarufu ‘Kangaroo Mother Care’ (KMC) kilichopo katika Hospitali hiyo wakati akiwa na umri wa siku moja kwa ajili ya huduma kubwa zaidi ya kitaalamu mwaka 2018.

“Mama wa Renata alijifungulia nyumbani na kufariki kutokana na kutokwa na damu nyingi,” anasema Kaindoa.

Anaongeza: “Renata aliletwa hapa kwenye kituo cha KMC na baba yake ambaye alijitambulisha kwa jina moja pekee kama Richard (36) kutoka kijiji cha Bugorora.”

Anasema alimuacha hapo akiwa katika huduma ya kangaroo na alipokuwa na umri wa wiki mbili, Renata alitelekezwa hospitalini hapo na baba yake wa kumzaa kutokana na hali yake ilivyokuwa, tangu wakati huo Kaindoa amemtunza kama mwanaye wa kumzaa.

“Baba yake alituambia kwamba alikuwa anarudi kijijini ili kukutana na ndugu zake na aliahidi kuwa atarudi baada ya siku kadhaa lakini tangu wakati huo, hakuwahi kuonekana tena,” anasimulia Kaindoa.

Kwa mujibu wa Kaindoa, Renata ni mtoto wa sita katika familia hiyo akielezea kuwa kifo cha mama yake huenda kilisababishwa na huduma hafifu za uzazi wa mpango.

“Fikiria katika umri huo mdogo, tayari alishazaa watoto watano. Nadhani kifo chake kinahusishwa na kutokuwa na mipango mizuri ya uzazi wa mpango, “ anasema Kaindoa wakati wa ziara ya hivi karibuni hospitalini hapo.

Yeye ni miongoni mwa wataalamu wa afya katika Mkoa wa Kagera ambao walipewa mafunzo na kuwezeshwa kwa vifaa na njia za kisasa za utoaji wa huduma za afya chini ya Mradi wa Afya ya Mama na Mtoto (MCSP) uliogharimu Dola32 milioni za kimarekani na kutekelezwa na shirika la Jhpiego, chini ya ufadhili wa USAID.

Maisha ya Renata yaanza

Baada ya Renata kutimiza umri wa mwezi mmoja na wiki mbili, aliondolewa kutoka kwenye kitengo cha huduma maalumu za dharura (NICU) na kupelekwa kwenye wodi ya kawaida hospitalini hapo kwa ajili ya huduma maalumu zaidi. Wakati huo alikuwa na uzito wa kilogramu 2.5.

Baada ya hatua hiyo, Renata alianza kuongezeka uzito wa karibu gramu 112 hadi 200 kwa wiki mpaka alipofikisha miezi minne. Faida ya uzito huu kwake ni kubwa kwani kwa kawaida watoto wadogo huongezeka chini ya gramu tano kila siku lakini kuna wakati hufikia ongezeko la hadi gramu 20 kila siku kwa baadhi yao. Renata alihitaji matunzo ikiwemo uangalizi wa karibu, chakula, mavazi na hata malazi, lakini aliendelea kuishi wodini chini ya uangalizi wa Kaindoa.

Akizungumzia gharama za kila siku ambazo anajitahidi kuhakikisha kwamba Renata anapata mahitaji muhimu ya kila siku, ikiwemo chakula na nguo, Kaindoa anasema kwamba hutumia angalau Sh5,000 kwa siku ili kufidia gharama za kila siku kwa chakula na pampers.

“Baadhi ya fedha hutumiwa kuwezesha gharama nyingine za kufua na kununua nguo. Lakini wakati mwingine wasamaria wema hujitokeza na kuleta nguo kwa ajili yake,” anasema Kaindoa.

Kwa sasa, Renata ana uzito wa kilogramu 8.7 na anaishi katika jengo la hospitali, kwenye ofisi ya wauguzi katika kitengo cha afya ya mama, baba na mtoto ndipo kitanda cha Renata kilipo.

“Wakati mimi nikiwa kazini, wauguzi wengine waliosajiliwa hospitali wanamtunza. Amekuwa mmoja wa wafanyakazi wa hospitali, kila mtu anafurahi kuwa naye kwa miaka mingi ijayo, “anasema Kaindoa. Anaongeza: “Yeye atakulia hapa na labda atakuwa mmoja wetu (muuguzi) kwa sababu anatumia muda nasi tangu asubuhi hadi usiku kila siku. Nina hakika atapenda kuwa muuguzi atakapokua. “

Akizungumzia ongezeko la haraka la watoto wachanga wanaozaliwa kabla ya muda wao nchini, Kaindoa alibainisha kuwa hospitali hiyo imepokea watoto zaidi ya 150 kabla ya kuanzishwa kwa kituo cha KMC hospitalini hapo.

Akizungumzia matokeo mazuri ya mradi wa MCSP, Kaindoa anasisitiza kuwa idadi ya vifo vya watoto wachanga imepungua katika kanda yao.

Mkurugenzi wa Mradi wa MCSP, John George anasema kuanzishwa kwa vituo hivyo kumewasaidia wataalamu wa afya katika kanda hiyo kuhudhuria mafunzo ya kupunguza vifo vya watoto wachanga wanaozaliwa kabla ya muda wao.

“Lengo ni kuhakikisha angalau watoto wachanga 1000 wanaozaliwa kabla ya muda wao wanahudhuria hospitali ikilinganishwa na 500 waliohudhuria hapo awali,” George anasema.

Kwa mujibu wa Kaindoa, mwaka wa 2018 watoto 70 wachanga waliozaliwa kabla ya muda walizaliwa katika hospitali ya Mugana, wawili pekee ndiyo walifariki.

Kituo cha KMC katika Hospitali ya Mugana ni kati ya vituo 25 vilivyoanzishwa na kufadhiliwa na Jhpiego chini ya mradi wa MCSP kwa lengo la kukabiliana na vifo vya uzazi katika mikoa ya Mara na Kagera.

Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni zilizotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) zilionyesha kuwa kila mwaka, watoto milioni 15 wanazaliwa kabla ya muda wao (kabla ya wiki 37 za kukua kwa mimba), na idadi hii inaongezeka.

Ulimwenguni, kuzaliwa kabla ya muda (njiti) na uharibifu wa hali ya hewa ni sababu zizoongoza kwa vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano. Na katika karibu nchi zote zilizo na takwimu za kuaminika, kiwango cha kuzaliwa kabla ya muda kinaongezeka.

Pia, tofauti za viwango vya maisha katika suala la uzazi salama ulimwenguni pote ni sawa. Katika mazingira ya kipato cha chini, nusu ya watoto waliozaliwa au chini ya wiki 32 (miezi 2 mapema) hufa kutokana na ukosefu wa huduma inayofaa, kama vile joto, kunyonyesha na huduma ya msingi ya maambukizi na matatizo ya kupumua.

Wakati kwa nchi za kipato cha juu, karibu watoto wote hawa wanaishi jambo linalochangiwa na matumizi ya kisasa ya teknolojia .

Hata hivyo lishe bora, kuepika matumizi ya tumbaku, dawa, mama kuwa karibu na huduma za faya na vipimo vya fetasi ikiwa ni pamoja na matumizi ya ultrasound itasaidia kubaini tatizo mapema.