Tume huru ya uchaguzi, amri tata za ma-DC, RC madai sugu bungeni

Saturday April 20 2019
pic tume

Dodoma. Tangu kuanza kwa mkutano wa Bejeti wa Bunge Aprili 2, mwaka huu moja kati ya mambo yanayozungumzwa mara nyingi na wabunge ni vitendo

vya wakuu wa mikoa na wilaya kuwaweka watu ndani kinyume na sheria na madai ya Tume huru ya uchaguzi.

Masuala hayo ambayo yamekuwa ni kilio cha muda mrefu, safari hii yameibuka katika mjadala wa Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na baadaye yakajirudia katika bajeti ya Ofisi ya Rais, (Utumishi na Utawala Bora) na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Kana kwamba haitoshi, pamoja na majibu yanayotolewa na mawaziri, vilevile yameibuka katika Wizara ya Katiba na Sheria.

Baada ya wabunge kuzungumzia masuala hayo kwa kina, Serikali imekuwa ikitoa majibu ambayo baadhi yameonekana kuwagusa wabunge kwa namna moja au nyingine, wa chama tawala na upinzani japokuwa mengine yameonekana ya kisiasa na si suluhisho la tatizo husika.

Mabadiliko ya Katiba

Advertisement

Katika hoja ya kutaka mabadiliko ya Katiba, yameibuka mambo mawili; ama kuendeleza mchakato wa Katiba Mpya kwa kupigwa kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa au kufanya marekebisho ya Katiba ya sasa ili kupata Tume huru ya uchaguzi kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu 2020.

Katika mjadala wa bajeti hizo, kati ya wabunge watatu wa upinzani waliosimama kuzungumza, mmoja kati yao aligusia suala la Katiba Mpya na vitendo vya wakuu wa mikoa na wilaya kuwaweka watu ndani.

Katika Katiba suala linaloonekana kupata uzito ni Tume huru ya uchaguzi ambapo wabunge wamebainisha kuwa haki inaonekana kutotendeka chini ya tume ya sasa. Wametoa mifano lukuki, ikiwemo mawakala wa upinzani kuzuiwa kuingia vituoni wakati wa chaguzi ndogo, madai kuwa wasimamizi wa uchaguzi hutangaza watu ambao hawakushinda na masanduku ya kura kuporwa.

Mathalani, Katika hotuba ya maoni ya kambi rasmi ya upinzani bungeni kuhusu bajeti ya Ofisi ya waziri mkuu kwa mwaka wa fedha 2019/2020, waliitaka Serikali kupeleka bungeni muswada wa marekebisho ya Katiba kabla ya uchaguzi wa Serikali za mitaa ili kuwezesha kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi.

Kambi hiyo inayoongozwa na Freeman Mbowe, mwenyekiti wa Chadema, ilipendekeza kuundwa kwa Tume huru itakayoondoa mamlaka ya Rais ya kuteua mwenyekiti, makamu mwenyekiti na wajumbe wengine au wakurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Badala yake, kambi hiyo ilishauri wajumbe hao wateuliwe kwa utaratibu mwingine maalumu utakaowekwa kwa mujibu wa katiba hiyo.

Pia, ilishauri kuanzisha mfuko wa fedha wa Tume Huru ya Uchaguzi, jambo litakalohakikisha uwepo wa fedha za kuendesha shughuli za uchaguzi nchini wakati wote bila kutegemea huruma ya Serikali kuu na rasilimali watu. Na tatu ni kuondoa katazo la kushtaki au kupinga mahakamani uamuzi wa Tume ya Uchaguzi kuhusu uendeshaji wa uchaguzi.

Mbunge wa Tarime Mjini (Chadema), John Heche alilieleza Mwananchi kuwa wakurugenzi wa halmashauri walielezwa hadharani kuwa hawatarajiwi kumtangaza mpinzani kushinda, jambo linaloashiria uporaji wa kura.

“Kwa uzoefu wa chaguzi zilizofanyika huko nyuma hatukuwahi kuona hali tunayoiona sasa. Hivi sasa ni kawaida mnaweza kukusanya matokeo yenu na mkaona mmeshinda ila msimamizi wa uchaguzi anataja mshindi mwingine,” alidai Heche.

“Hivi sasa wapiga kura wanaweza kuwa wengi kuliko waliojiandikisha kupiga kura. Mawakala wanazuiwa vituoni. Haya mambo yanaweza kufanyika katika chaguzi ndogo ila yakifanyika uchaguzi mkuu hali itakuwa mbaya sana. Suluhisho ni kuleta mabadiliko ya Katiba bungeni ili turekebishe kifungu kuhusu Tume ya uchaguzi ili twende katika uchaguzi kwa amani,” alisema Heche.

Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi maarufu Sugu alisema, “mtu yeyote anayekataa kufanya jambo jema ujue ni mwovu. Kama hawaibi katika uchaguzi kwa nini hawataki kuondoa shari, tufanye mchakato wa kuwa na tume ambayo kila mtu akishindwa kunakuwa hakuna malalamiko.”

“Inatakiwa iwepo Tume huru ambayo mfumo wa uundwaji wake tutautengeneza sisi, mfano tume inaweza kuwa na wawakilishi kutoka kila chama.”

Hata hivyo, uongozi wa Tume ya uchaguzi umezungumzia suala hilo mara nyingi, ikisema iko huru na inafuata sheria, kanuni, taratibu na miongozo katika kusimamia uchaguzi.

Hata hivyo, mahitaji ya tume huru hayakuanza leo, hata Tume ya Jaji Francis Nyalali iliwahi kueleza kuwa “mwenyekiti na wajumbe wa tume ya uchaguzi sharti wachaguliwe na Bunge na Baraza la Wawakilishi”.

Rasimu ya Katiba ya Jaji Warioba na Katiba inayopendekezwa kwenye ibara za 190 na 211 zimeongelea kuhusu kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi na jinsi tume hiyo itakavyopatikana.

Pia, wakati Bunge lilipokaa kama kamati kupitisha bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria ya mwaka 2019/2020, Viti maalum (Chadema), Salome Makamba alishika shilingi ya waziri, akitaka majibu ya Serikali ni lini itaendeleza mchakato wa Katiba.

Wabunge wa upinzani waliunga mkono hoja hiyo na kupewa nafasi ya kuchangia, huku wenzao wa CCM wakiipinga na kukumbushia jinsi vyama vya upinzani vilivyosusia vikao vya Bunge Maalumu la Katiba na kuipinga Katiba Inayopendekezwa kwa madai kuwa imechakachuliwa.

“Lakini ukurasa wa 206 na 207 wa ilani ya CCM inasema wazi kuwa; ‘Ili kuendeleza utawala bora, demokrasia na uwajibikaji katika kipindi cha miaka mitano ijayo CCM itahakikisha inatekeleza yafuatayo, (g) kukamilisha mchakato wa kutunga katiba mpya na kuanza kuitekeleza kwa mujibu wa sheria ya mabadiliko ya katiba.”

Mbunge huyo alitaka Serikali kuwaeleza wananchi ni lini wataipata Katiba mpya.

Baada ya kauli hiyo mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge alimweleza Salome kuwa si lazima kila kilichopo katika ilani ya uchaguzi ya chama chochote cha siasa kutekelezwa.

Pia, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Profesa Adelardus Kilangi alisema, “Katiba ni dira na ndio mwongozo ila mchakato wa Katiba utaendelea kulingana na mazingira na mahitaji yatakavyoruhusu.”

Salome hakuridhika na na maelezo hayo lakini hata wabunge walipochangia hoja hiyo na kupigiwa kura za sauti haikupita baada ya mwenyekiti kuridhika na kura zilizosema hapana.

Wakuu wa mikoa, wilaya

Suala jingine moja ni la wakuu wa mikoa na wilaya kuwaweka watu ndani, hoja ambayo Serikali iliitolea ufafanuzi wa kina bungeni, ikibainisha kuwa si sahihi kwa watendaji hao kufanya mambo hayo.

“Ninamshukuru mwanasheria mkuu wa Serikali ametoa waraka kwa wote waliopewa mamlaka ya kuweka mtu ndani na mie kanipa nakala, akieleza mazingira ya mtu kuwekwa ndani,” alisema Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), George Mkuchika.

Akiwa anajibu hoja za wabunge walizozitoa katika mjadala wa bajeti hiyo Mkuchika alifafanua, “Moja awe ametenda kosa la jinai, na (mkuu wa wilaya, mkoa) uweke kwa maandishi kwa nini umemuweka ndani. Utawala bora unasema kesi ikiwa mahakamani hakuna mkuu wa wilaya au mkoa au waziri anayeweza kuisikiliza (nje).”

“Mahakama ya chini uamuzi wake unaweza kutenguliwa na mahakama ya juu, wengine wamejiingiza katika matatizo kwa mambo ambayo tayari yametolewa hukumu mahakamani.”

Mkuchika alisema wakuu wa wilaya na mikoa wanapotumia mamlaka yao kuweka mtu mahabusu kwa saa 24 na 48 wazingatie sheria ya tawala za mikoa ya mwaka 1997.

“Sheria hii inawapa mamlaka kuwaweka ndani watu pale inapothibitika anahatarisha amani. Nawaomba wabunge tusikilize sheria na nawaomba na huko walipo (wakuu wa wilaya na mikoa) wanisikilize,” alisema.

“Mtu anawekwa ndani kama amehatarisha amani, si watu wanadaiana madeni hawataki kulipa unawapeleka kwa mkuu wa mkoa. Hawa wanadaiana si kuhatarisha amani.”

Alisema viongozi hao wakitekeleza hatua kinyume na utaratibu wanaweza kuchukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kushtakiwa binafsi.

Advertisement