Mbunifu wa teknolojia anayebadili maisha ya wasichana

Friday February 21 2020

 

By Julius Mnganga, Mwananchi [email protected]

Wengi hulalamika kuhusu wasichana nchini wanavyonyimwa nafasi ya kusoma ila ni wachache wanaochukua hatua.

Miongoni mwa wasiolalamika ila wanawasaidia ni Caroline Ekyarisiima, mwanzilishi wa Shirika Lisilo la Kiserikali la Apps and Girls alilolisajili Machi 2014. Hadi sasa anasema limewafundisha zaidi ya wasichana 6,000.

Caroline ni mhitimu wa sayansi ya kompyuta ambaye kwa miaka minne aliajiriwa kama mhadhiri msaidizi wa Chuo Kikuu cha Kampala (KIU) kilichopo jijini Dar es Salaam.

“Kwenye kila darasa nililokuwa nafundisha kulikuwa na idadi ndogo sana ya wasichana. Hivyo nikaona kuna haja ya kuwajengea uwezo,” anasema Caroline.

Baada ya kubaini hilo, mama huyu wa watoto watatu anasema alichukua hatua. Mwanzoni, mwa mwak 2013 alianza kuwafundisha wasichana sebuleni kwake. “Ni vitu vya kawaida vya ubunifu wa kutumia kompyuta mfano kutengeneza katuni, programu za simu za mkononi, tovuti hata kutatua changamoto mbalimbali zilizopo kwenye jamii,” anasema.

Alianza kwa kutoa tangazo na akapata watu 30 ambao wengi walikuwa ni wafanyakazi ambao halikuwa lengo lake. Yeye alikusudia kuwahamasisha mabinti wadogo zaidi hivyo akaanza kuwatafuta wanafunzi.

Advertisement

Wasichana hao anasema walikuwa wanaenda nyumbani kwake eneo la Mzambarauni, Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam alikokuwa anaishi.

Kadri idadi ya wasichana ilivyoongezeka, kukawa na changamoto ya rasilimali za kufundishia na mahitaji mengine.

Mwaka 2014 anasema kampuni ya mawasiliano ya Tigo ilikuwa na shindano la kuwatafuta wabunifu wanaotatua changamoto za jamii hivyo akaamua kushiriki na kuibuka mshindi.

Anasema shindano hilo lilikuwa linaitwa Tigo Digital Change Maker na aliposhinda alipata Dola 25,000 za Marekani.

Alipopata fedha hizo alianza kwenda shule tofauti za sekondari kuanzisha ‘coding clubs’ (vikundi vya wanafunzi wanaotengeneza programu za kompyuta). Wanafunzi aliowalenga zaidi ni wale wanaoamua wasome mchepuo upi, kuanzia kidato cha pili na cha tatu.

“Tulianzisha klabu tisa mwaka 2014 lakini baada ya kuwapa mafunzo tukaona wanabaki na ujuzi wasioweza kuutumia hivyo tukaanzisha utaratibu wa kuwajengea uwezo wa kijasiriamali ili waweze kuyaendeleza mawazo yao kibiashara,” anasema.

Mwaka uliofuata walianzisha mashindano ambayo wanafunzi walishindanisha mawazo yao. Washiriki 30 walijitokea na klabu zikafika 15.

Caroline ni aina ya wajasiriamali wasiokata tamaa akiwa amejengewa uwezo zaidi mwaka 2016 aliposhiriki program ya Young African Leaders Innitiative (Yali) iliyoanzishwa na Rais mstaafu wa Marekani, Barrack Obama ili kuwajengea uwezo wabunifu, viongozi na wajasiriamali wa Afrika.

Alipotoka Marekani, anasema mwishoni mwa mwaka huo alihama sebuleni na kutafuta ofisi wakati huo klabu za wanafunzi zikiwa zimefika 28 na wakaanza kuwajengea uwezo walimu wa kompyuta pia. “Mwaka 2017 tukishirikiana na ubalozi wa Marekani nchini, tulijipanga vizuri zaidi,” anasema.

Mafanikio

Miaka saba ya kuwajengea uwezo wasichana haijapita bure. Ndani ya kipindi hicho, App and Girls inayo mafanikio inayojivunia ambayo ni chachu ya kusonga mbele.

Caroline anasema kati ya washiriki wa mashindano ya mwaka 2015 mmoja alitengeneza mfumo unaokusanya manyanyaso wayapatayo wanafunzi wanaotumia usafiri wa umma ambao alipoujaribu alipokea zaidi ya maoni 1,000.

Aliupeleka mfumo huo kushindana Tume ya Taifa ya Sayansi (Costech) na akashinda Dola 5,000 kuuendeleza. Alipohitimu kidato cha nne alipata fursa kwenda Marekani na Finland na akawa mmoja wa vijana 20 wanaoleta mabadiliko duniani.

Alipotoka huko alipewa ufadhili kusoma kidato cha tano na sita nchini Afrika Kusini na sasa amepata udhamini wa Mastercard kwenda kusoma chuo kikuu Uingereza.

Mwaka huo pia alikuwepo mwingine aliyetengeneza mfumo wa kuwasaidia wanawake wenye fistula. Kabla hajamaliza kidato cha nne aliwafikia wanawake 300 waliotibiwa Hospitali ya CCBRT.

“Wakishatibiwa hupewa mtaji kidogo kuanzisha biashara. Naye amepata ufadhili na ataenda kusoma Kenya,” anasema Caroline.

Katika kituo chake cha mafunzo ya ubunifu kilichopo Mwananyamala, Dar es Salaam ana washiriki wa mwaka 2018 wanaoendelea kuboresha program zao kwa udhamini wa Shirika la Elimu na Watoto la Umoja wa Mataifa (Unicef).

Mwaka 2018 Unicef walikuwa na shindano la ‘Generations Unlimited’ lililofanyika katika nchi 15 Tanzania ikiwamo. “Walihitajika watu watano lakini hapa kwetu walitoka wanne, mmoja alitoka Iringa. Walikuwepo washiriki wa vyuo vikuu pia lakini hawakushinda,” anasema.

Mwaka 2017 walianza kufundisha utengenezaji wa roboti na timu ya vijana watano ilienda kushiriki mashindano ya dunia Washington, Marekani, wenzao walienda Mexico na wengine Dubai.

“Hawa wote ni wasichana wa kawaida kutoka familia za chini. Ninaye binti mmoja hapa ambaye ni mjumbe wa bodi wa taasisi ya utafiti mjini Morogoro,” anasema.

Wasichana waliofeli

Baada ya kujihusisha sana na wanafunzi walio shuleni, Caroline anasema waligundua wapo wanaolazimika kuacha shule kutokana na sababu mbalimbali hivyo mwaka jana wakaanzisha program maalum ijulikanayo kama Jovia.

Program hiyo inawahusisha walioacha shule kwa kukosa ada, waliolazimishwa kuolewa au wafanyao kazi za ndani. Wasichana hao hufundishwa kwa miezi sita kwa udhamini wa taasisi ya South African Innovation Support (SAIS) iliyo chini ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc).

Mabinti hao, anasema wanafundishwa utengenezaji program za kompyuta na simu za mkononi, katuni mjongeo (animations), tovuti na program zinazoweza kutatua changamoto kwenye jamii.

“Wakihitimu tunawatafutia kazi au wawekezaji wa kuendeleza program walizozitengeneza. Wanashindana na wahitimu wa chuo kikuu na kuwashinda,” anasema.

Anatoa mfano wa msichana mmoja aliyebuni mfumo unaotoa taarifa kuhusu lishe ya watoto na wagonjwa. Program hiyo inamuelekeza mzazi chakula cha kumpa mtoto kulingana na umri alionao.

Na kuna msichana aliyetoroka kuozeshwa akaacha shule anasema amebuni mfumo wa kuuza vyakula. Ukiagiza, utapewa bei na ukikubali unaletewa. “Kuna wanawake wawili wanaotoa huduma hiyo mpaka sasa,” anasema.

Kuna binti aliyetengeneza mfumo unaotambua muda wa matumizi ya dawa lakini kwa kuwa ni suala linalohusisha Serikali, wanaendelea kuwasiliana na mamlaka husika kupata ruhusa ya kuuingiza sokoni.

Mradi wa Jovia unatekelezwa pia Kajiado nchini Kenya kwa wasichana wa Kimasai na Bukavu huko Jamhuri ya Demokrasi ya Kongo (DRC) kwenye jamii inayokabiliwa na mapigano.

“Mwaka 2019 ilikuwa awamu ya kwanza, sasa tunapokea wengine. Tumeshatoa tangazo la kutafuta wasichana wengine,” anasema.

Ushindi

Caroline hawajengei tu uwezo wa kujiamini mabinti anaowafundisha. Yeye pia ni mfano. Kila inapotokea fursa, anashindana na mara nyingi anashinda.

Ukiacha mwaka 2014 aliposhinda ufadhili wa Tigo, mwaka jana alishinda Euro 100,000 kutoka SAIS zinazotumika kutoa mafunzo ya Jovia.

Akiwa na vijana 10 aliowaajiri na vibarua 15 ameshinda pia nafasi ya kuwafundisha wanafunzi wa shule 61 zilizofungiwa intaneti na kupewa kompyuta na Tigo.

Kuhakikisha wasichana wanapata maarifa yaliyokusudiwa, katika shule zote za umma ambako kuna miundombinu ya intaneti, anashauri walimu wapewe mafunzo yatakayowawezesha kuitumia.

Advertisement