Tanzania yashinda kwa hifadhi bora duniani

Friday February 28 2020

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Israel. Wakati ikichuana na Kenya pamoja na Afrika Kusini, Tanzania imeibuka kidedea kwa kuwa na hifadhi zenye mvuto zaidi duniani.

Tanzania imeshinda tuzo hiyo ambayo ni sehemu ya tuzo za Outlook Travellers Awards (Olta) zinazoandaliwa na Jarida la Outlook Travellers la nchini India.

Akipokea tuzo hiyo, balozi wa Tanzania nchini India, Baraka Luvanda amesema tuzo hiyo itaongeza imani ya watalii watakaovutiwa kuja Tanzania kujionea wanyama tofauti waliopo kwenye mbuga za nchini.

“Tunaamini tuzo hii pamoja na habari za jarida la Outlook Traveller watu wengi watapata taarifa za uhakika kuhusu ubora wa vivutio vilivyopo Tanzania...vinavyoongoza kwa mvuto,” alisema Balozi Luvanda katika taarifa iliyowekwa kwenye ukurasa wa tovuti ya ubalozi.

Pamoja na tuzo hiyo, alisema Tanzania haitabweteka bali itaendelea kuvitangaza vivutio vyake hasa kwenye masoko mapya.

Jarida la Outlook Travel limejikita katika kuchapisha taarifa za mafanikio ya sekta ya utalii ili kuongeza hamasa kwa wananchi kutembelea vivutio vilivyopo maeneo tofauti ulimwenguni pamoja na mchango wake kwenye pato la Taifa.

Advertisement

Jarida hilo linashirikiana na bodi za utalii kutoka mataifa tofauti duniani na husomwa na zaidi ya watu 575,000.

Advertisement