Masabeda: Sekondari ya kata na ufaulu unaozitingisha shule kongwe

Muktasari:

Ni shule ambayo wazazi wamejitambua, walimu wanawajibika na wanafunzi wamekubali kujifunza

Pata picha ya shule ya kata ikiwa nafasi ya tatu kimkoa, ya tisa kitaifa kwa orodha ya shule za Serikali na ya 251 kati ya shule 3488 zote nchini. Hivi ndivyo ulivyokuwa ufaulu wa shule ya sekondari Masabeda iliyopo mkoani Manyara katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2018.

Katika matokeo hayo, hapakuwepo mwanafunzi aliyepata daraja sifuri ambalo ni maarufu kwa wanafunzi wengi wa shule za kata.

Wenyeji wa kata ya Bashnet mkoani Manyara wanaiita shule ya kimataifa, lakini kwa taratibu za kiserikali bado ni shule ya kata.

Jina la kimataifa limekuja baada ya shule hiyo pekee katika kata ya Bashnet kufanya vizuri katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne kwa miaka minne mfululizo.

Hata hivyo, ufaulu wa Masabeda haujaja kirahisi. Ushirikiano baina ya walimu, wazazi, viongozi na wanafunzi umeipaisha shule hiyo hadi kufikia hatua ya kupigiwa mfano.

Ni shule inayosadifu ukweli kuwa kama jamii itaamua kuwekeza vilivyo shule za kata zinaweza kuwa mkombozi kwa watoto wa Kitanzania.

Mchango wa shule hiyo katika kata ya Bashnet umekuwa mkubwa kwa wanafunzi ambao wengi wanatoka familia za kawaida tena zile za vijijini.

Mafanikio ya Masabeda yamewasukuma wakazi wa vijiji vya kata hiyo hasa wanawake kuja na salamu isemayo: ‘Mwanamke na mtoto chuo kikuu’ wakimaanisha kuwa watoto wao wengi hasa wasichana wameanza kujiunga na kidato cha tano na wengine wamepata sifa ya kujiunga na vyuo vikuu.

Mwenyekiti wa bodi ya shule, Theodori Bilauri anasema ndani ya miaka miwili shule hiyo imewezesha vijana zaidi ya 70 kujiunga kidato cha tano.

‘’Kuwa na wanafunzi 74 wanaoenda masomo ya juu kama stashahada ya udaktari wa binadamu ualimu na udaktari wa mifugo na kidato cha tano, kati ya 85 si kazi ndogo kutoka shule ya kata,’’ anasema

Anaongeza: “Shule haina maabara iliyokamilika isipokuwa jengo moja tu lililokamilika lakini hakuna vifaa vya maabara.

Walimu wanapanga nje ya shule, hakuna umeme ambao ungepunguza gharama ya uchapaji mitihani na mazoezi ambayo kwa masabeda ni sawa na sala.’’

Wakazi wengi wa Bashnet wanaamini kuwa ufaulu wa wanafunzi katika shule hiyo ya kata ni wa kuipigia kengele Serikali kuwa inaweza inaweza kutegemea shule zake kuboresha elimu, badala ya wananchi kuingia gharama ya kuwalipia ada katika shule binafsi.

‘’Tumetoa mikono na mioyo yetu kwa uongozi na walimu wote. Hatubakizi chochote kwa kuwasaidia wanapohitaji msaada ulio ndani na hata nje ya uwezo wetu wote. Tutafanikisha tu,” ni kauli yake mzazi Priscus Tlaqsi huku akiungwa mkono na Raphael Amsi.

Wakati baadhi ya watu wakizibeza shule za kata kwa hoja ya kuwa ni zao la matamko ya kisiasa, kwa wakazi wa Bashnet shule hiyo kwao ni mkombozi; ndio maana wameamua kujitoa kwa hali na mali. Hata lilipotoka agizo la wazazi kutotoa michango ikiwa ii utekelezaji wa mpango wa elimu bure, jamii ya Bashnet haikukubali kuona watoto wao wakikosa elimu bora kwa sababu ya michango. Wamekuwa wakiendelea kuchangia gharama za chakula, mitihani na nyinginezo.

Mafanikio kitaaluma

Katika matokeo ya mwaka 2018, wanafunzi 13 walipata daraja la kwanza. daraja la pili wanafunzi 38. Wanafunzi 23 walipata daraja laa tatu, huku daraja la nne likiwa na wanafunzi 11.

Shule hiyo pia imepata ufaulu mkubwa katika masomo ya sayansi huku wasichana wakiongoza kwa kupata daraja la kwanza hadi la tatu.

Kwa mfano, kati ya wanafunzi 45 waliofanya mtihani wa Fizikia ni moja tu aliyefeli, Huku 34 wakipata alama C. Wanafunzi tisa walipata alama A katika somo la Biolojia, 21 wakipata B na wanafunzi 48 wakipata alama C. Alama D walipata wanafunzi sita na hakuna aliyefeli.

Hata somo la Kemia ambalo halikuwa na mwalimu kwa zaidi ya miaka mitatu, wanafunzi walifanya vizuri. Huwezi kuamini kuwa ufaulu huo wa kushangaza umekuja shule ikiwa na mwalimu mmoja mmoja kwa kila somo la sayansi na pia ukosefu wa vifaa vya mazoezi.

‘’Hatuna vifaaa kabisa vya maabara. Tunatumia maji ya ndoo, tunatumia meko za China au kibatari badala ya bunsen burner ya gesi. Pamoja na hayo yote tunafanya mitihani ya vitendo halisi na siyo mbadala,’’ anasema mwalimu pekee wa Biolojia shuleni hapo, January Malley.

Kwa ufaulu huo anasema kati ya wanafunzi 74 walioenda masomo ya juu, 60 wameenda shule na vyuo vya sayansi kama udaktari wa binadamu na mifugo, na kidato cha tano wakisoma tahasusi za PCB, PCM na nyingine.”

Malley anasema kuwa amegundua kuwa walimu wanapokuwa karibu na wanafunzi, hata wanafunzi wazito kiakili na wazembe wanajituma.

‘’Wanafunzi wa Masabeda wako karibu na walimu wao na wanapendana. Hata tukiwaadhibu wanafunzi hawalalamiki. Tumekuwa kama wazazi wao. Wazazi wanachangia mitihani na mazoezi na kila mwezi tunatoa majibu hadharani na kutangaza wa mwanzo na wa mwisho,’’ anasema.

Siri ya mafanikio

Mkuu wa shule, Lucas Qwaray anasema: ‘’Ushirikiano mzuri kati ya walimu, wazazi, wanafunzi Serikali na uhusianio baina ya watumishi na wahudumu shuleni ni siri kubwa ya mafanikio. Kila mtu anatekeleza wajibu wake na wanategemeana. Walimu hushindana kupasisha watoto ikiwamo hata mazoezi ya kila mwezi.”

Ofisa elimu wa Mkoa wa Manyara, Arnold Msuya anasema hakuna uchawi kwa Masabed kufanya vizuri zaidi ya wanafunzi kujifunza kwa bidii na kuzingatia maelekezo ya walimu.

‘’ Wazazi, walezi, wanafunzi na walimu wa shule hiyo wametimiza wajibu wao ipasavyo kuhakikisha wanafunzi wanasoma na kufaulu, licha ya ukweli kuwa wapo eneo la pembezoni,’’ anasema.

Wanafunzi wasifu

Mwanafunzi Alberto Sherwin anayesoma kidato cha tano katika Shule ya Njombe High School ni mmoja wa wahitimu wa Masabeda, anayesema shule hiyo ni ya kipekee na anaona tofauti kubwa na shule anayosoma sasa.

‘’Huko Njombe sisi likizo, wikiendi, sikukuu ni mapumziko. Hatujazoea hayo Masabeda, walimu wa Masabeda wana nidhamu sana na wanaonekana kama walimu na kuheshimiwa na wazazi na jamii yote.

Hii ndiyo Masabeda shule iliyojengwa kwa nguvu za wazazi mwaka 2008. Licha ya uhaba wa walimu hasa wa sayansi na Hisabati huku ikiwa na maabara moja na hata tatizo la maji shuleni, shule hiyo bado inasonga mbele ikizipiga kumbo shule nyingi kongwe nchini.

Kinachovutia zaidi ni kuwa mafanikio haya yote yamepatikana shule ikiwa chini ya uongozi wa mwalimu mwenye diploma ya ualimu. Kwa sasa mwalimu huyo amewekwa kando kumpisha mwenzake mwenye elimu ya chuo kikuu ikiwa ni utekelezaji wa agizo la kila shule ya sekondari kuongozwa na mwalimu mwenye shahada.

Nyongeza kwa hisani ya mwalimu Jacob Qorro