Breaking News

USHAURI WA DAKTARI: Fahamu chanzo cha kuziba mirija ya uzazi

Sunday December 15 2019Dk Shita Samwel

Dk Shita Samwel 

Kuziba kwa mirija ya uzazi ni moja ya sababu inayochangia ugumba kwa wanawake, mirija hii hujulikana kitabibu kama Fallopian tube ndiyo inayounganisha kokwa za kike (ovary) na nyumba ya uzazi.

Kila mwezi katikati ya mzunguko wa hedhi kijiyai huchoropoka na kusafiri kutoka katika kokwa za kike kupitia katika mirija ya uzazi na kwenda katika nyumba ya uzazi.

Endapo mbegu ya kiume itarutubisha kijiyai cha kike katika mirija muunganiko huo husafiri na kujipachika katika tando nyororo za nyumba ya uzazi kwa ajili ya kupiga hatua za ukuaji (mimba).

Kama mirija hii itazibwa kwa namna yoyote ile ina maana kuwa mbegu za kiume zitashindwa kwenda kurutubisha kijiyai cha kike.

Ni kawaida pia mirija kuziba na kuacha kipenyo hivyo mbegu ya kiume hupita na kupandikiza kijiyai lakini baadaye hushindwa kusafiri kwenda katika nyumba ya uzazi kwa ajili ya mimba kukua.

Zipo sababu mbalimbali ambazo zinachangia mara kwa mara kujitokeza kwa tatizo hili ikiwamo uwepo wa kovu, maambukizi na kukandamizwa na tishu za maeneo ya kiunoni.

Advertisement

Maambukizi ya bakteria katika viungo vilivyopo ndani ya kiuno ikiwamo nyumba ya uzazi hushambuliwa na kusababisha makovu ndani ya mirija ya uzazi.

Makovu hayo kutokana na maumbile yake huweza kusababisha kijiyai kukwama. Uwepo wa tatizo la tishu za tando laini za nyumba ya uzazi kujirundika eneo lisilo lake ikiwamo katika mirija ya uzazi husababisha kuziba, tatizo lijulikanalo kitabibu kama Endometriosis.

Vile vile tishu hizo huweza kujipachika nje ya nyumba ya uzazi na kubanana na mirija hiyo na hatimaye kuiziba.

Magonjwa yanayoenea kwa njia ya kujamiiana ikiwamo kisonono (Gonorrhea) na klamidia hushambulia maeneo ya viungo vya uzazi hivyo kuchangia tatizo hili.

Kuwahi kufanyiwa upasuaji baada ya mimba kutunga na kukua katika mirija badala ya nyumba ya uzazi (Ectopic Pregnancy) upasuaji huu huweza kuacha kovu katika mirija.

Uvimbe wa Fibroid unaweza kuwa mkubwa na kuziba katika mirija hiyo hasa mahala ulipojichimbia katika nyumba ya uzazi.

Kuwahi kufanyiwa upasuaji wa nyumba ya uzazi hasa katika mirija yenyewe inaweza kusababisha kushikamana na tishu za tumbo na mirija hiyo kuziba.

Mambo mengine hatarishi ni pamoja na vimelea kushambulia katika nyumba ya uzazi, kuharibika kwa mimba mara kwa mara na kujifungulia maeneo yasiyo salama.

Vile vile uvamizi wa maambukizi ya bakteria mwilini, kupasuka kwa kidole tumbo, kusafishwa nyumba ya uzazi na vifaa visivyo safi na salama na upasuaji wa maeneo ya pango la tumbo.

Mambo mengine yanayochangia tatizo hili ingawa kwa uchache ni pamoja na matumizi ya vidonge vya uzazi wa mpango, ajali au majeraha maeneo ya kiuno.

Madhara ya kuziba ni pamoja na mimba kutungwa na kukua katika mirija tatizo linaloitwa Ectopic Pregnancy, hutokea baada ya mbegu za kiume kupita katika upenyo wa mrija ulioziba kwa kiasi. Madhara makubwa ni pale mirija yote miwili inapokuwa imeziba bila kuacha upenyo wowote hivyo mbegu ya kiume hushindwa kupita kwenda kuungana na kijiyai cha kike. Matokeo ya hali ni kupata ugumba kwa wanawake.


Advertisement