TUONGEE KIUME: Unachotakiwa kumfanya mkeo mwenye tabia ya kujizeesha

Sunday November 24 2019

 

By Kelvin kagambo

Mara ya kwanza ulipokutana na mkeo alikuwa malaika. Alikuwa ni mwanamke mzuri zaidi ya unavyoweza kuelezea. Alikuwa ni mwanamke anayeweza kubeba sifa zote tamu na bado akabaki na nafasi ya kupokea zingine, hakika alikuwa ni ndoto yako na uliona fahari kutembea naye kwenye sherehe zote za harusi ukimtambulisha kwa washikaji na ndugu zako bila wasiwasi.

Kipindi kile ulikuwa unamuona kama Miss Tanzania, binti wa mfalme, staa wa Bongo Movie, alikuwa ameiva kama embe dodo katikati ya msimu wake kwa kumuangalia tu ulikuwa na kila sababu ya kumteua kuwa mkeo.

Lakini ulipomuoa tu vitu vikaanza kwenda tofauti, wimbo wenu wa mahaba ukaanza kuimbwa nje, mke wako akajisahau kwamba mwanamke ni maua, pambo machoni mwa mumewe.

Akaanza kuishi kwa kutojijali, kujizeesha na kweli akazeeka.

Kutwa anashinda amejifunga kanga ya kifua, kichwa kina manywele kama ‘mwendawazimu’, ngozi yake haijui mafuta, hajui manukato mazuri yaani kazeeka.

Wakati huo wewe ukienda kazini unakutana na kina Shanteel, wanawake wanaochukia kuzeeka ukiwatazama hivi ni kama kivutio cha utalii.

Advertisement

Sasa ukilinganisha haya unayoyaona nje na mkeo wa zamani ni pilau na mlenda, vitu viwili tofauti. Na usipokuwa makini sana unaweza kujikuta unacheza mechi za ugenini kwa sababu hiyo tu.

Tufanyeje?

Ongea na mkeo

Kwanza kabisa ongea na mkeo. Wanawake wanadanganywa au wanajidanganya kwamba uzuri wa mwanamke si urembo ni akili na tabia, lakini ndani ya mioyo yetu wanaume tunafahamu huo si ukweli wanaume wote tunapenda wanawake wazuri kwa mwonekano, wenye akili na tabia nzuri. Ukitutolea kitu kimoja kati ya hayo hatuishi kwa furaha sana.

Sasa kaa chini zungumza na mkeo ukweli wa jinsi unavyojisikia, mueleze jinsi gani unavyotamani kumuona hazeeki, mueleze jinsi unavyosikia raha ukimtazama akiwa amevaa magauni mazuri yaliyo kwenye fasheni, jinsi unavyopenda ukisikia ananukia na akisuka nywele za Kimasai na mitindo mingine ya kuvutia.

Mwambie asijidanganye kwamba mwanamke ni akili ya maisha kila senti ni lazima iende kwenye kununua mchanga wa kufyatua tofali za nyumba mnayojenga Makongo juu hapana, mwambie ukweli kwamba hukumuoa aje kuwa msimamizi wa miradi ya ujenzi, bali aje kuwa mke. Mkumbushe kuwa mke ni uwaridi kwa mume, uwaridi kwako, lazima apendeze.

Mnunulie unavyovipenda

Waswahili wanasema binamu yako akiwa anakuka kikwapa usimwambie kwa mdomo, nenda dukani, mnunulie pafyumu, mpelekee kama zawadi fanya kwa kurudia ataelewa unachomaanisha.

Fanya hivyo kwa mkeo pia, nenda dukani mnunulie mabegi ya kike, magauni, manukato, mawigi mazuri na kila kitu unachopenda kumuona akiwa nacho matokeo yake utayashangaa.

Wanawake wote ni wazuri wakiamua kuonekana hivyo, kwa hiyo Shanteel wa kazini kwako kwao sio mzuri kwa sababu ni mzuri kuliko mke wako, hapana, ni mzuri kwa sababu ameamua tu awe mzuri.

Advertisement