TUONGEE KIUME: Watoto wetu hawajui…

Kama mwanaume kuna wakati unagundua ulitua kwenye mti usiokufaa; yule uliyemuamini mwanzo kwamba akiwa mmiliki msaidizi maskani kwako nyumba itakuwa ni edeni ndogo anakwenda ndivyo sivyo, tofauti na matarajio.

Huenda yeye ndiye aliyekuwa chanzo cha mambo kuharibika au pengine wewe ndiye unayestahili kubeba huo msalaba, kwenu haijalishi, kwa sasa wote mko ‘bize’ kuangalia namna ya kuutua huu mzigo ambao labda mwanzo, kila mmoja aliamini anaweza kuubeba na kupita nao katika kila hali.

Tunapofikia hapa wengi huona njia pekee ya kurejesha amani iliyopotea kwenye maisha yetu ni kutengana, kugawana ustaarabu kila mmoja achukue hamsini zake na bila kufahamu hapa ndipo tunapokosea.

Kuachana ikiwa ndiyo suluhisho la kwanza kwenye matatizo makubwa ya familia huko ni kupotoka, ni kupotoka kwa sababu tunawapoteza watoto wetu kwa namna fulani na kuzipoteza roho za upendo walizozijenga juu yetu tangu watufahamu.

Watoto hawajui kama kuna kipindi hufikia uhusiano wa baba na mama unashindwa kufanya kazi, hivyo kinachotakiwa kufuata hapo ni kuachana tu.

Watoto wetu si watu wanaoamini kwamba kuna uwezekano wa kupata furaha kwa mama mwingine, furaha pekee na ya kweli wanayoijua ni ile inayotokana na baba mzazi, mama mzazi na wao kuishi nyumba moja, kula pamoja, kutazama TV pamoja, kwenda kumtembelea shangazi kila mwisho wa wiki na kila kitu si vinginevyo.

Kuachana hakujawahi kuwafurahisha watoto wetu kwa namna yoyote ile hata kama wanaona waziwazi kwamba mmoja wa wazazi hayuko sawa labda baba analewa sana kiasi cha kuwadhalilisha hata wao huko kwa majirani.

Au mama kuwa na tabia za ajabu zenye kuwafedhehesha. Wenyewe wanaweza kuchukia, hata wakafikia hatua ya kuropoka kwamba kwa nini baba na mama msiachane tu, lakini kuwa makini hii huwa haitoki moyoni kwa maana sawa na kile unachokisikia.

Unaposikia mtoto anasema maneno ya hivyo basi elewa anachomaanisha ni kwamba, kwa nini baba na mama msiweke pembeni, mwenye tatizo ajirekebishe ili maisha yarudi kama zamani... Hiki ndicho wanamaanisha.

Hatusemi kutengana ni ‘dhambi kubwa kuliko’, hapana, kuna hatua inafikia huoni kama kuna uwezekano wa ndoa au familia kuendelea kuwa kitu kimoja na chenye amani ni lazima utengano uwepo.

Lakini ni vyema kabla watu hawajafikia uamuzi wa kutengana wakaangalia maisha ya watoto wao yatakavyokuwa na kuangalia maisha si kwa maana ya kwamba watakavyolipia ada ya shule na mahitaji mengine muhimu hapana, kuwaangalia watoto maana yake ni kutazama watakuwa na maisha ya furaha na amani kiasi gani pindi agano la ndoa yenu likivunjika.

Watoto wetu hawajui kama kuna sababu ya kumfanya baba na mama watengane, tuangalie mara mbilimbili uamuzi huu kabla hatujaukaribisha katika maisha yetu.