Breaking News

Unavyoweza kufaidika kwa kumiliki ekari moja

Saturday May 18 2019

 

By Asna Kaniki, Mwananchi

Ni moja wala sio zaidi. Wala huhitaji maelfu ya ekari. Ni ekari moja pekee inayoweza kukutoa kimaisha.

Hili linawezekana vipi? Hilo ni eneo kubwa kwa mkulima makini na mbunifu.

Sasa tumeshatoka katika zama zile za mkulima kuwa na maelfu ya ekari, huku nyingi zikibaki kuwa mapori.

Kilimo cha kisasa kinahitaji eneo dogo lakini mkulima anaweza kutumia eneo hilo kuendesha mradi wenye tija.

Makala haya yanatazama eneo la ukubwa wa ekari moja na namna mkulima anavyoweza kufaidika.

Katika ekari moja, utalima na kufuga. Hiki kinaitwa kilimo mseto. Na sio kilimo mseto pekee, hata ufugaji, upo pia ufugaji mseto.

Advertisement

Makala haya yanakupa mwanga na njia inayokuonyesha namna unavyoweza kutumia eneo la ekari moja pekee kufanya mradi wa maana wa kilimo. Ekari moja inatosha kuwa ajira yako na pengine ikakutoa kimaisha. Kivipi?

Pangilia shamba lako

Hili ndilo jambo muhimu kulifanya wewe mwenyewe lakini pia hata kwa kumtumia mtaalamu wa kilimo, inawezekana kulipangilia shamba lako.

Muhimu ni kile unachotaka kufanya katika shamba lako. Ikiwa ni kilimo jiulize cha aina gani na kama ni ufugaji ni ule wa aina gani.

Tambua kuwa katika eneo la ekari moja, ikiwa litapangiliwa vizuri, mkulima anaweza kuwa na eneo la bustani za mazao kadhaa, eneo la kufuga jamii ya ndege kama kuku, bata, eneo la kufuga wanyama kama ng’ombe na pia eneo kwa ajili ya ufugaji wa samaki.

Haya yote yanaweza kufanyika ikiwa ekari hiyo utaigawa katika vipande. Kwa mfano, ikiwa una eneo lenye ukubwa wa mita 70 kwa 70, upo uwezekano wa kutoa vipande takriban 12 vya ukubwa wa mita 20, huku kila kipande kikiwa mahususi kwa ajili ya uzalishaji fulani.

Kilimo mseto

Eneo la ekari moja linatosha kabisa kwa mkulima makini kufanya aina zaidi ya moja ya kilimo.

Unaweza kuwa na mazao ya kudumu ya jamii ya miti kama vile miti ya matunda.

Hii inaweza kukupa matunda lakini pia ikasaidia kutoa kivuli kwa mifugo mingine.

Lakini kikubwa zaidi ni kuwa eneo hili unaweza kulitumia kwa ajili ya bustani za aina mbalimbali.

Ufugaji mseto

Eneo la ukubwa wa ekari moja linaweza pia kutumika kwa ajili ya ufugaji mseto.

Huu ni ufugaji unaojumuisha samaki, ndege kama jamii ya kuku na wanyama. Shughuli za shamba zinazoenda sambamba na ufugaji ni pamoja na kilimo cha mazao mbalimbali kama vile mboga mboga,.

Faida za ufugaji huu ni pamoja na kuongeza ufanisi, mavuno na hatimaye faida inayopatikana inakuwa kubwa.

Badili fikra

Si wakati tena wa kufikiri kuwa unaweza kulima kwa kuwa na kiasi kikubwa cha ardhi.

Ekari moja inatosha. Fuata mwongozo huu utengeneze fedha kupitia kilimo na ufugaji.

Hizi ndizo sekta ambazo wengi sasa wanazichangamkia kupata kipato maishani. Unasubiri nini tafuta sasa ekari moja yako.

Advertisement