Unavyoweza kufuga nyuki kisasa

Muktasari:

Katika makala haya, tutaangazia namna ambavyo unaweza kuwajengea nyuki nyumba, ili kuboresha mazingira yao ya uzalishaji na hatimaye kupata ufanisi zaidi.

Ufugaji wa nyuki ni kazi ambayo imekuwapo nchini kwa karne nyingi. Kwa walio wengi, ufugaji huu unahusisha matumizi ya mizinga inayoning’inizwa kwenye miti. Hata hivyo, ufugaji wa nyuki umechukua sura mpya na rahisi zaidi.

Shughuli ya ufugaji wa nyuki nchini Tanzania hasa katika mkoa wa Tabora ambao ni maarufu kwa uzalishaji wa asali, ilianza kutambulika rasmi tangu mwaka 1884, baada ya wakoloni kama Rebman na Craft kufika katika eneo hilo.

Katika kipindi hicho, jamii ya eneo hilo walikuwa wanafuga nyuki kwenye magome ya miti, vibuyu, vyungu, mapango, vichuguu na kwenye miamba. Baada ya muda, ufugaji ulipiga hatua kidogo na watu wengi wakawa wanafuga kwa kutumia mizinga iliyochongwa kutoka kwenye magogo ya miti. Ufugaji wa aina hii umedumu kwa karne nyingi nchini Tanzania.

Kutokana na mahitaji na ongezeko la matumizi ya bidhaa za nyuki, kulifanyika tafiti mbalimbali ambazo ziliweza kuboresha ufugaji wa nyuki, kwa kuwa na mizinga ya kisasa ambayo imewezesha uzalishaji wa asali kuwa mkubwa na kuongeza pato la wafugaji tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

Tafiti hazikuishia kwenye kuboresha mizinga tu, ila siku hadi siku kunavumbuliwa namna bora zaidi za kuimarisha uzalishaji wa nyuki.

Katika makala haya, tutaangazia namna ambavyo unaweza kuwajengea nyuki nyumba, ili kuboresha mazingira yao ya uzalishaji na hatimaye kupata ufanisi zaidi.

Nyumba ya nyuki

Hii ni aina mpya ya ufugaji wa nyuki ambayo unaweza kujenga kibanda au nyumba kisha kuweka mizinga kwa idadi unayohitaji.

Kwa nini kibanda? Ni muhimu kufuga nyuki kwenye kibanda au kwenye nyumba, kwa sababu inasaidia kudhibiti wizi wa mizinga pamoja na wanyama wanaokula asali na kudhuru nyuki.

Pili, inarahisisha utunzaji wa mizinga na kuwafanya nyuki wasihame kwenda sehemu nyingine.

Inasaidia watu wengi kujifunza namna nzuri ya ufugaji wa nyuki, ikiwa ni pamoja na watoto, jambo ambalo linafanya shughuli hii kuwa endelevu.

Pia, ufugaji wa aina hii unasaidia kuwakinga nyuki dhidi ya majanga kama vile moto na mafuriko, na inawaepusha nyuki na usumbufu unaoweza kuwafanya wasizalishe kwa kiwango kinachotakiwa.

Faida nyingine ni kuwa uzalishaji unaongezeka. Hii ni kwa sababu mizinga inayotumika ni ile ya kibiashara. Mzinga mmoja unaweza kupata asali kilo 30 sawa na lita 20.

Aina ya nyumba

Unaweza kujenga nyumba yenye upana wa futi tatu na urefu wa futi tisa. Nyumba hii inaweza kuchukua mizinga 50. Halikadhalika, unaweza kujenga kibanda chenye ukubwa sawa na huo.

Eneo linalofaa

Ili kuwa na ufanisi mzuri, nyumba hii inafaa kujengwa nje kidogo ya makazi ya watu, kusiwe na mifugo karibu na iwe sehemu ambayo watoto hawawezi kufika.

Pia isiwe karibu na njia ambayo watu wanapita mara kwa mara. Kusiwe na aina ya mimea ambayo nyuki hawapendi na kusiwe na maji karibu.

Mavuno

Baada ya kujenga nyumba, kuweka mizinga na nyuki kuingia, unaweza kuvuna kwa mara ya kwanza baada ya miezi mitatu.

Utaweza kupata mavuno mazuri endapo utavuna kabla nyuki na wadudu wengine hawajaanza kula asali.

Ni muhimu kuhakikisha kuwa wadudu waharibifu kama vile sisimizi, mende na wengineo wanadhibitiwa ili wasiathiri uzalishaji wa asali.

Hakikisha unavuna kitaalamu ili kuepuka upotevu wa asali. Ikiwa nyuki watatunzwa vizuri na kwenye mazingira mazuri, unaweza kuvuna asali mara tatu kwa mwaka.

Katika mzinga mpya, nyuki wana uwezo wa kutengeneza masega kwa siku tatu na kuanza uzalishaji wa asali.

Makala haya kwa hisani ya mtandao wa mkulima mbunifu