Dar imekithiri siasa kuliko vitendo vya maendeleo

Saturday January 18 2020

 

By Luqman Maloto

Tayari tupo mwaka 2020. Imebaki miezi tisa kufanyika uchaguzi mkuu, hivyo kuhitimisha muhula wa uongozi wa 2015 mpaka 2020. Mwaka wa mwisho wa muhula umeambata na kioja cha umeya wa Jiji la Dar es Salaam na huenda vikaja vioja vingine kama hivyo.

Wajumbe (madiwani) wa CCM walikusudia kumng’oa Meya wa Jiji, Isaya Mwita. Mvutano mpaka nusura ngumi zichukue nafasi. Kura zikapigwa lakini zikapungua kufikia theluthi mbili ambazo ndizo zingetosha kumwondosha Mwita.

Wakati kura hazikutosha, Mwita alinyang’anywa gari, akafungiwa ofisi. Wao wakahesabu wamemng’oa. Kuna watu wanaweza kudhani kufanya hivyo ni kumkomoa Mwita au chama chake, Chadema, lakini vurugu hizo ni kuliumiza Jiji la Dar es Salaam na wakazi wake.

Kumnyang’anya meya gari na kumfungia ofisi ni kumfanya ashindwe kutimiza wajibu wake. Matokeo yake shughuli za halmashauri zinazorota. Wanaoumia ni wananchi.

Tukio la Mwita kuondolewa madarakani na fujo zilizoambana na tukio hilo, ni moja ya vipimo kuwa kipindi cha kuanzia mwaka 2015 mpaka 2020, kilitekwa zaidi na minyukano ya kisiasa kuliko mipango na utekelezaji wa maendeleo.

Unaweza kuwaza; moja ya sababu ya kutaka kumwondoa Mwita ofisini ni eti gari la meya kupata ajali. Mwita anaendeshwa na dereva wa halmashauri. Kweli abiria awajibishwe kwa ajali ya gari lililoendeshwa na mwingine?

Advertisement

Mengine sitaki kuingia, lakini hiyo ni kuonyesha kuwa suala la Mwita kuondolewa madarakani lilijaa siasa. Madiwani wa CCM badala ya kushirikiana na Mwita ili kufanikisha maendeleo ya Jiji la Dar es Salaam, wao wapo kwenye mikakati ya kumng’oa. Kuna maendeleo hapo?

Dar es Salaam ambayo miaka yote mvua ikinyesha nyingi jiji halipitiki, barabara zinafungwa kwa sababu ya miundombinu mibovu, vyama vya siasa vinapambana kushindania madaraka. Jiji linazidi kubaki nyuma. Ikumbukwe, hata Mwita kuingia Ofisi ya Meya, ulitokea mvutano mkubwa.

Lipo tatizo la kutoachiana nafasi ya kisiasa kati ya vyama tawala na wapinzani. Hali hii inasababishwa na vyama kuoneana wivu. Uchaguzi unakwisha, kila upande unakuwa umevuna stahiki yake. Hata hivyo chuki na kuoneana gere za kisiasa zinadumu miaka na miaka.

Binafsi naamini kuwa Mungu ni sababu ya kila kinachojiri duniani, hivyo hawezi kupatikana kiongozi kama Mungu hajataka. Kwa mantiki hiyo, nidhamu ya kwanza ya kimaisha ni kutambua uwepo wa kiongozi na kumheshimu kwa nafasi yake.

Kumtambua na kumheshimu kiongozi kwa nafasi yake ni ufunguo wa nafsi yako kuwa na mawazo chanya juu yake hata kama hukubaliani naye. Ukishatambua ni kiongozi, mpe thamani yake.

Unapompa thamani kiongozi, basi atakapofanya vizuri utamsifia hata kama mnapishana kiitikadi, maana hafanyi kwa ajili yake bali kwa umma.

Unapomsahihisha kiongozi ili afanye vizuri au unapomsifia anapofanya vema, usitazame kwa jicho la kumjenga yeye, bali fikiria kwa jicho la ujenzi wa nchi. Anapoitwa kiongozi maana yake amebeba matarajio kwa kipindi husika.

Suala la maendeleo ya nchi na huduma kwa raia ni muhimu kuliko tofauti za kiitikadi na matamanio ya madaraka. Viongozi waliopo wanaposhindwa kufanya vizuri haitakiwi iwe kicheko kwa baadhi ya watu, bali kilio kwa taifa zima. Maana ni hasara ya taifa zima si waliopo madarakani peke yao.

Tunahitaji nchi isonge mbele, kwa hiyo ni vizuri wenye ridhaa ya kuongoza wawe wanapewa nafasi ili watekeleze yaliyomo kwenye ilani zao. Kuendekeza wivu wa kisiasa husababisha vizingiti na mwingiliano usio na sababu.

Vizingiti hivyo si maslahi ya wananchi bali vyama. Taifa haliwezi kunufaika kwa wenye vyama kutetea masilahi ya vyama vyao kuliko ya wananchi. Siasa za vyama vingi hazikuwekwa ili kuwepo na misuguano ya aina hiyo.

Vyama vingi vipo kwa ajili ya kushindana kwa hoja kuhusu namna bora ya kuwaongoza wananchi. Wapigakura wanasikiliza vyama na wagombea, kisha wanaamua upande wanaoridhika nao.

Ni vizuri kwamba wakati wale ambao wamepewa nafasi wanapokuwa kazini wanatakiwa kuungwa mkono, kusahihishwa wanapokwenda nje ya mstari kwa lengo la kujenga nchi moja. Hizo ndiyo siasa.

Wivu unaoumiza wananchi

Rais John Magufuli anapotekeleza wajibu wake, kama kuna mahali labda amekosea, haitakiwi wapinzani washangilie, bali watoe hoja zenye kumsahihisha vizuri zaidi. Maana nchi inajengwa kwa ushirikiano mkubwa wa wananchi, chama tawala, wapinzani na hata wasio na vyama.

Kama wapinzani wanapokosoa wanaonekana kuwa hawana nia njema kwa Serikali, matokeo yake ndio kunakuwa na mvutano wa pande mbili, wakati nyumba inayojengwa ni moja.

Siasa za kugombea fito zimekithiri Afrika. Ni nadra kuona mshikamano wa kisiasa kati ya utawala na upinzani. Nyakati zote watu huwaza uchaguzi.

Zipo nchi, viongozi waliopo madarakani huhakikisha upinzani unakufa ili kuwa na wakati mzuri wa vyama tawala kufanya siasa bila kusumbuliwa na presha za wapinzani.

Uwepo wa vyama vya upinzani ni chachu ya vyama tawala kuwajibika zaidi. Kwamba watawala wanaona wakichezea nafasi waliyonayo wananchi watawaweka pembeni na kuchagua wapinzani.

Kwa maana hiyo, badala ya vyama vya siasa kujikita katika kuoneana wivu au hata kuharibiana katika utendaji, vinapaswa kutambua nafasi. Kila upande uheshimu nafasi ya mwenzake.

Nini ambacho wananchi wanataka? Utawala tu au na vyama vya upinzani? Msingi wa kwanza upo hapo.

Wananchi kwa maendeleo yao hawahitaji wivu wa kisiasa kati ya utawala na vyama vya upinzani, isipokuwa wangependa kuona kunakuwa na mchanyato wa hoja za kujenga nchi.

Kati ya chama chenye mamlaka ya kuongoza Serikali Kuu na vingine vyenye kuongoza Serikali za Mitaa, haitakiwi kuwepo kwa misuguano. Mathalan, Serikali Kuu itumie nguvu kupokonya baadhi ya mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuzikomoa.

Wananchi kwa ajili ya maendeleo yao, wangependa kuona kila upande unaachwa utimize wajibu wake. Serikali Kuu itimize matarajio ya wananchi kupitia mamlaka zake, vilevile halmashauri zifanye kazi bora katika maeneo yao. Hivyo ndivyo wananchi wanataka.

Jiji la Dar es Salaam badala ya kugombana, wajitathmini. Miaka mitano inaisha, miundombinu ni mahututi kama walivyoikuta.

Advertisement