Jaji Warioba: Mwalimu Nyerere hakujikweza, alithamini utu, haki

Saturday October 12 2019

 

By Noor Shija, Mwananchi

Waziri mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba amesema Mwalimu Nyerere aliiishia maisha ya kawaida na alithamini utu na haki kwa wote.

Jaji Warioba ambaye aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati wa utawala wa Nyerere, alisema hayo wakati wa mahojiano na Mwananchi hivi karibuni kuhusu miaka 20 baada ya kifo chake.

“Kwenye Taasisi ya Mwalimu tunapenda zaidi kusherehekea maisha yake kuliko kumbukumbu za kifo chake. Huwa tunakumbuka siku yake ya kuzaliwa ya Aprili 13, 1922,” alisema Jaji Warioba ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere.

Alisema Mwalimu pamoja na nafasi kubwa aliyopewa katika jamii, bado alibaki mtu wa kawaida mwenye mawazo na mwelekeo wa mtu wa kawaida.

Jaji Warioba alisema Mwalimu alikuwa na imani ya utu wa binadamu, aliamini watu wote ni sawa kwamba kila mtu anastahili heshima.

“Alipochaguliwa kuwa Rais, wakati ule ilikuwa ni kawaida watu kumuita mtukufu Rais, lakini yeye alikataa kuitwa mtukufu Rais, akasema yeye si mtukufu, mtukufu ni Mungu, yeye ni binadamu na mwalimu wa kawaida. Ndio chanzo cha kumuita Mwalimu,” alisema Jaji Warioba.

Advertisement

Anasema pia mkewe Maria Nyerere walikuwa wakimuita ‘First Lady’, lakini alikataa na kusema huyu ni Mama Maria, ndio jina hilo limekua kama cheo.

Jaji Warioba alisema Mwalimu alikataa jina lake kukuzwa na alikataa habari zake kuwa kubwa kwenye vyombo vya habari.

“Vyombo vya habari ilikuwa ni kawaida iwe ni magazeti au redio, habari ya kwanza inahusu Rais. Yaani ilikuwa kwenye redio habari ya kwanza ni ‘Rais amesema nini’, magazeti ukurasa wa kwanza ilikuwa alichozungumza Rais.

“(Nyerere) Akasema hii si sawa. Siyo kila kitu ninachosema ni cha muhimu kuliko matukio mengine waliyosema wengine,” alisema Jaji Warioba akimnukuu Mwalimu Nyerere.

Pia, Jaji Warioba alisema Mwalimu alikataa jina lake kutumiwa kwa mambo mbalimbali, kama majina ya barabara, majengo. Alipokuwa Rais hakukuwa na barabara iliyokuwa inaitwa Nyerere.

Anasema Mwalimu hakupenda viongozi kuitwa muheshimiwa, aliamini Watanzania wote ni ndugu na alitaka waitane ndugu ikiwamo yeye kuitwa ndugu Rais.

“Wakati wake kumuita ndugu Rais ilikuwa jambo la kawaida. Mahusiano yake ni kweli alikuwa anafanya kazi na viongozi, lakini hakusahau marafiki zake wa kawaida na alikuwa anakutana nao. Anakutana na wazee na anacheza nao bao. Kwa mfano, Dosa Azizi alikuwa ni rafiki yake alikuwa anaweza kumkaribisha wakazungumza wenyewe tu kama marafiki pale Msasani,” alisema Jaji Warioba.

Jaji Warioba alisema Mwalimu Nyerere alikuwa anaamini haki kwa wote, hata katika maandiko yake alikuwa anasisitiza haki na ndiyo ulikuwa msingi kwenye mapambano ya kujikomboa kutoka kwa wakoloni.

Anasema Mwalimu katika kazi zake zote alitaka watu kushirikiana na kuwa pamoja. Kwake ilikuwa muhimu sana na ndiyo maana aliona muhimu ni kujenga Taifa kwanza na siyo kujenga nchi.

Anasema Mwalimu Nyerere baada ya kushika madaraka aliondoa matabaka yote ya kibaguzi yaliyowekwa na wakoloni.

Anasema pia kulikuwa na ubaguzi wa kikabila ambao aliuondoa, hata ikawa muhimu kuondoa machifu.

“Haikuwa kazi rahisi, ukiangalia Tanzania ni tofauti kabisa na jirani zetu. Tanzania ni Taifa. Hata wakijitokeza baadhi ya watu kutaka kuleta ukabila, kuna watu wanakemea, lakini kwenye mataifa mengine unakuta bado wanaendelea na ubaguzi wa kikabila,” alisema Jaji Warioba.

Jaji Warioba anasema Tanzania ina zaidi ya makabila 120, lakini Mwalimu Nyerere alitumia lugha ya Kiswahili kuyaunganisha makabila yote kwa kujenga, umoja, mshikamo na hadi sasa nchi ina amani.

Anasema pia Mwalimu Nyerere alikuwa anaamini utu wa binadamu na watu wote wako sawa. Mwelekeo wa maendeleo ilikuwa ni maendeleo kwa wote.

“Sasa hivi kuna jitihada kubwa za kuleta maendeleo tunafufua viwanda siyo kwamba ndio mara ya kwanza tunaingia kwenye mfumo wa viwanda, tunafufua viwanda. Lakini, msingi ni ule ule viwanda ni vile viwanda ambavyo wangefaidi wananchi kwa ujumla.

“Unataka uanzishe viwanda ambavyo kwanza utatengeneza bidhaa ambazo zinahitajiwa na wote, pili ni viwanda ambavyo vitasaidia mali ghafi zitoke kwa wananchi wenyewe. Viwe ni viwanda ambavyo mwelekeo wake uwe ni kutumia malighafi za nchini, lakini kuwainua wakulima,” alisema Jaji Warioba.

Akizungumzia maadui wa maendeleo, umasikini, maradhi, ujinga na dhuluma (rushwa), alisema bado kama taifa halijafanya vizuri kwenye kuondoa umasikini na rushwa.

Jaji Warioba alisema Serikali imefanya jitihada za kupambana na ujinga kwa kujenga shule, vyuo na kutoa elimu bure, pia katika suala la maradhi hospitali zimejengwa na matibabu yako katika hali ya juu.

Hivyo, alisema umasikini bado kuna tatizo na hasa kwa wakulima na watu wa kawaida wanaoishi mijini.

Anasema kama taifa bado kuna tatizo kwenye kilimo na hasa utaratibu wa wataalamu kwa kuangalia mchango wa kilimo kwenye pato la ndani ya taifa (GDP).

Jaji Warioba anasema ukuaji wa kilimo unapaswa kupimwa kwa namna mkulima alivyoinuliwa kutoka kwenye hali duni na kuwa na maisha bora, kwa sababu huko ndiko kwenye umasikini.

“Kuboresha kilimo ni kuinua hali ya masikini waliopo vijijini. Sasa hivi mkulima ana matatizo makubwa sana. Anayo matatizo ya kupata mbegu bora na zikipatikana wakati mwingine hawana uwezo wa kununua hizo mbegu bora. Ana matatizo ya kupata mbolea na pembejeo na zikipatikana wakati mwingine ziko juu ya uwezo wake.

“Mkulima ana matatizo makubwa ya soko, huko nyuma tulijaribu kuwasaidia wakulima kulikuwa na ruzuku wanapata, kwa hiyo walikuwa wanaweza kupata mbegu kwa bei ya uwezo wao pia, mbolea na pembejeo.

Kulikuwa na ruzuku kwenye soko, unanunua mahindi Songea kwa bei kubwa lakini sembe kwenye soko la Dar es Salaam inakuwa bei nafuu kumlinda mkulima,” anasema Jaji Warioba.

Anasema ulipoingia mfumo wa soko huria mkulima bado hajafaidika na hasa kwa utaratibu wa soko, kwa kuwa mazao yanayouzwa nje yanategemea soko la dunia na hapa ndani kama mkulima hasaidiwi hali yake itaendelea kutetereka.

Jaji Warioba anasema kipimo sahihi cha machango wa kilimo ni pale maisha ya mkulima yanapokuwa yamestawi.

Kuhusu maisha ya mjini anasema vijana wengi hawana ajira ila wanafanya biashara ambayo kama wanawafanyia watu wengine kwa kuwa siyo yao.

“Kwa kuwa hawana mtaji anakwenda kuchukua mali ya tajiri anauza ni kama anamfanyia yule kazi,” anasema Jaji Warioba

Advertisement