Kanuni mpya THRDC zazuia Azaki kufungamana na vyama vya siasa

Wednesday November 20 2019

 

By Mussa Juma, Mwananchi

Tanzania ikijiandaa kwa uchaguzi wa serikali za mitaa Novemba 24 mwaka huu na uchaguzi mkuu mwakani, Asasi zisizo za kiserikali (Azaki) na watetezi wa haki za binaadamu wamekuja na kanuni mpya zinazoweka utaratibu wa ushiriki wao.

Hawa ni wadau muhimu katika chaguzi nchini, kutokana na fursa ambayo wanapata ya kutoa elimu ya mpiga kura na elimu ya uraia.

Pamoja na hayo, viongozi wa asasi wa Asasi hizo wana haki sawa na Watanzania wengine kushiriki katika masuala ya kisiasa.

Haki ya viongozi hawa zinalindwa na Katiba ya Tanzania, Ibara ya 21(1) inayoeleza kwamba,

“…kila raia wa Jamhuri ya Muungano anayo haki ya kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi, ama moja kwa moja au kwa kupitia wawakilishi waliochaguliwa na wananchi kwa hiari yao, kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa na sheria au kwa mujibu wa sheria.”

Katiba inaongeza kuwa, kila raia ana haki na uhuru wa kushiriki kwa ukamilifu katika mchakato wa kufanya maamuzi juu ya masuala yanayoathiri wananchi na ustawi wa taifa.

Advertisement

Kwa hiyo, haki ya kupiga kura na au ya kupigiwa kura ni msingi katika taifa lolote la kidemokrasia na kama hii haki ya msingi ikikiukwa au kubatilishwa, demokrasia katika maana yake ya msingi itaondoshwa.

Azaki na vyama vya siasa

Pamoja na haki hizo, kumekuwepo tuhuma kuwa kuna baadhi za Azaki zinapendelea vyama fulani vya siasa nyakati za uchaguzi kutokana na matendo na kauli zao.

Hali hii imekuwa ikiathiri hadhi baadhi ya viongozi wa Azaki na kufikia hatua ya kutolewa kauli hadharani kuwa ni wanachama wa vyama vya siasa.

Baadhi ya Azaki zimekuwa zikituhumiwa kutumia rasilimali fedha, magari na ushawishi mwingine kwa ajili ya kuunga mkono vyama au viongozi wake kugombea katika siasa.

Suluhisho la tuhuma

Kutokana na hali hiyo, Mtandao wa watetezi wa haki za binadamu (THRDC) wenye wanachama 183 ambao watetezi binafsi na Azaki, umezindua kanuni za mashirika wanachama wa mtandao, juu ya ushiriki wao katika uchaguzi mkuu.

Mratibu wa Mtandao wa THRDC, Onesmo Ole Ngurumwa anasema katika kanuni hizo, wanachama hawapaswi kujihusisha moja kwa moja na chama cha siasa au kuwa wagombea wa cheo cha kisiasa wakati wanafanya kazi za utetezi.

Vilevile, watetezi hao wanapaswa kuwa na matumizi sahihi ya rasilimali walizopewa na wafadhili na kuzitumia kwa madhumuni yaliyokusudiwa na lazima waeleze kwa wadau wote, wakiwamo pamoja na walengwa, ni kwa jinsi gani wametumia rasilimali na matokeo gani wameyapata.

“Wanapaswa kufanya kazi zao kwa uwazi, kutoa taarifa za shughuli zao na mipango yao kwa wadau kwa kuzingatia kanuni za uwazi,” anasema.

Vilevile, watetezi hao wanapaswa kufanya kazi kwa uadilifu na kwa ufasaha nyakati za uchaguzi kwa kuzingatia kanuni za uadilifu.

Kwa mujibu wa Olengurumwa, wanachama wa THRDC na watetezi wanaoshiriki shughuli mbalimbali nyakati za uchaguzi na kwenye michakato ya kidemokrasia, wataongozwa na kanuni bila kupendelea upande wowote na bila kumbagua mgombea yeyote.

Kutumia kanuni

Akizindua kanuni hizo, Dk Judith Odunga, mkurugenzi mstaafu wa WiLDLAF, anawataka wanachama kutumia kanuni hizo kama mwongozo katika utendaji kazi wake.

“Nilipokuwa napitia kanuni hizi nimefurahishwa na eneo ambalo linazungumzia nguzo kuu ya demokrasia kwa kutoa kanuni na kuwapo uwazi bila kufanya vitu kwa vificho,” anasema.

Dk Odunga anasema kanuni hizo zitasaidia kutoa uelewa kwa watetezi na Azaki kuhusu majukumu yao nyakati za uchaguzi.

Anasema kanuni hizo zitasaidia kukuza uelewa juu ya haki na fursa za watetezi katika uchaguzi na mchakato mzima wa kidemokrasia; na kutoa maarifa kuhusu namna ya kushiriki kwa usalama, ufanisi, bila kupendelea upande wowote katika uchaguzi na mchakato wa kidemokrasia.”

Maoni kama hayo yametolewa pia na mkurugenzi wa muungano Azaki Zanzibar (Angoza), Hassan Juma anayesisitiza kuwa kanuni hizo ni muhimu katika utendaji wa Azaki nchini.

Anabainisha kuwa chini ya kanuni hizo, watetezi wa haki za binaadamu ambao wataingia katika siasa wanatakiwa kujitangaza na kujiondoa kuongoza mashirika yao hadi hapo watakapoondoka katika siasa.

Juma ambaye pia ni mjumbe wa bodi ya THRDC, anasema kanuni hizo zimeingizwa katika ya muungano huo ili kuondoa tuhuma za mashirika kuwa na fungamano na vyama vya siasa.

Advertisement