Mutungi, Sirro wana mazito kuhusu mikutano ya siasa

Wednesday July 24 2019

 

By Kelvin Matandiko, Mwananchi [email protected]

Kauli za Simon Sirro, mkuu wa Jeshi la Polisi na Jaji Francis Mutungi, msajili wa vyama vya siasa imezua sintofahamu.

Hii ni ya kuvalia njuga malalamiko ya viongozi wakuu wa vyama vya upinzani kuhusu hujuma wanazodai kufanyiwa na maofisa wa polisi kukwamisha mikutano ya kupanua mtandao wao, jambo wanalodhani linafanyika ili kuipa nafasi zaidi CCM.

Haya yameelezwa huku kukiwa na tukio kama la Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Jonathan Shanna kunukuliwa akieleza uhusiano wa moja kwa moja uliopo kati ya CCM, Serikali na polisi katika utekelezaji wa majukumu yao na wakati mwingine akiwafundisha vijana namna ya kujibu salamu ya chama hicho.

Pamoja na hayo, Jaji Mutungi na Sirro, kwa nyakati tofauti wamenukuliwa na gazeti hili wakiwataka “wanasiasa wanaodai kutotendewa haki katika mikutano yao ndani ya halmashauri wawasilishe madai yao kwa maandishi ili wachukue hatua”.

Wakati viongozi hao wakidai hawana upendeleo kwa chama chochote na wamekuwa wakisikia malalamiko hayo kwenye vyombo vya habari huku chama kikuu cha upinzani, Chadema inapuuza maelezo yao.

Katibu mkuu wa chama hicho, Dk Vincent Mashinji anasema Jaji Mtungi hana uhuru wala uwezo wa kuwa kinyume na matakwa ya anayemteua, ambaye ni mwenyekiti wa CCM, anayenufaika na vikwazo kwa vyama vya upinzani nchini.

Advertisement

Hata wachambuzi wa kisiasa wanahoji kuna haja gani ya viongozi hao kusubiri barua wakati haki hiyo ya kikatiba imeonekana kupokonywa wazi kwa mwaka wa nne sasa.

Wanahoji kwa nini Sirro na Mutungi wasichukue hatua ili kulinda Katiba, badala ya kufuata mfumo wa barua?

Aliyewahi kuwa makamu wa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Godwin Ngwilimi anasema Jeshi la Polisi na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ni taasisi zilizoanzishwa kisheria, zinazopaswa kutekeleza majukumu yake kisheria bila kuathiriwa na changamoto za kimfumo zilizopo kwa sasa.

Ngwilimi anasema wanachotakiwa kufanya si kupuuzia changamoto za kimfumo, bali kufuata sheria kwa kuwa hata majaji wanaotoa haki, wanaathiriwa na mfumo huohuo lakini wamekuwa wakisimamia majukumu yao na kutoa haki hata kwa vyama vya upinzani.

“Kama wapinzani watashindwa kutekeleza majukumu yao kisheria, basi itakuwa ni udhaifu wao binafsi. Mfumo wetu wa kikatiba na sheria ndivyo ulivyo. Wakilalamika kwa mtazamo huo tutawauliza mbona huwa wanakwenda mahakamani kudai haki yao kwa majaji walioteuliwa na rais huyohuyo wa CCM?” anahoji Ngwilimi.

Hata hivyo, Ngwilimi anasema hoja ya mfumo inahusu madai ya mabadiliko katika Katiba tuliyonayo.

Kuhusu hoja ya kuwasilisha malalamiko kwa barua kwa sasa, Ngwilimi anasema wako viongozi wanaofanya kazi kwa kufuata utaratibu rasmi na wako wanaochukua hatua bila kufuata taratibu za mfumo huo wa mawasiliano.

“Lakini wale wanaoathirika kwanini wasiende mahakamani? Kwa mfano, mimi mbunge fulani nimeomba kufanya mkutano katika eneo fulani nikazuiwa. Kwanini nisiende mahakamani kama ninaona kuna haki yangu imepokonywa kwa mujibu wa sheria?” anahoji.

“Ninaomba tamko la mahakama iseme kitendo hicho si halali na kinyume cha sheria za nchi, katika mgogoro wowote wa kisheria kwa nini upinzani wasichukue hatua za kisheria? Tena ni rahisi kabisa na mifano wanayo ya kutosha?”

Hata hivyo, Dk Mashinji anasema vikwazo wanavyowekewa katika mikutano ya kisiasa vimepangwa ili kudhoofisha nguvu yao kwa wananchi, jambo lililosababisha wafikiri mbinu mpya ya kufanya siasa.

“Sisi tutamwandikia barua kama alivyotaka, lakini ziko barua nyingi. Kila tukio unaloliona huwa tunamwandikia barua. Zote tunapeleka kwa dispachi. Je, anataka tuziweke mitandaoni? Hapana, siyo utaratibu wetu,” anasema.

Hoja za Sirro, Mutungi

Katika mahojiano na gazeti hili, awali Jaji Francis Mutungi aliagiza viongozi wa upinzani kulalamika kwa maandishi ofisini kwake badala ya kutumia vyombo vya habari.

“Waambie hao (wapinzani) wafanye iwe tangible, walalamike kwangu, na wao wanajua wakilalamika kwangu ni kwa maandishi. Siku zote tunapenda tupate chanzo. Umenielewa? Sasa wao wenyewe hawalalamiki lakini nyie waandishi mnalalamika. Huoni kama wanaweza wakawaruka,” alisema Jaji Mutungi.

Lakini, Sirro anasema Jeshi la Polisi hutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na halina upendeleo kwa vyama vyote vya siasa na kuwa tangu upinzani waanze kulalamika, hajawahi kupokea barua yoyote kuhusu malalamiko yao.

Anasema OCD anapokataa baada ya kuona kuna uvunjifu wa amani huwa anawaandikia barua (vyama), akitoa mapendekezo yake na ikiwa chama hakijaridhika, kinaweza kukata rufaa ofisi ya IGP au kwa waziri mwenye dhamana.

“Kama kuna chama ambacho kinaona hakitendewi haki na polisi, basi tuandikiwe malalamiko hayo ili tuweze kufuatilia kwanini hiyo wilaya imeshindwa kutoa haki, waniandikie barua. Kama hatueleweki basi waende kwa waziri wa Mambo ya Ndani. Kwa hiyo kuna utaratibu mzuri tu.”

Kuhusu upinzani kuzuiwa mikutano wakati ya CCM ikifanyika bila vikwazo, Sirro anasema hilo lijadiliwe kwa takwimu zinazoonyesha ushahidi.

Advertisement