KALAMU HURU: Waliopitishana bila kupingwa nao wanashangaa Sumaye kushindwa

Miongoni mwa mambo yaliyozua mjadala katika uchaguzi wa Chadema unaoendelea ni tukio la kuangushwa kwa Waziri mkuu mstaafu mstaafu, Frederick Sumaye aliyekuwa akitetea nafasi yake ya uenyekiti wa Kanda ya Pwani.

Katika uchaguzi huo uliofanyika Novemba 28, 2019 Kibaha Mkoa wa Pwani, Sumaye aliyekuwa akigombea peke yake alipigiwa kura 48 za hapana, 28 za ndiyo na moja ikaharibika. Matokeo hayo yameiacha kanda hiyo ikijipanga kutafuta mwenyekiti mwingine.

Kumekuwa na maoni mengi kuhusu anguko hilo, ambapo baadhi ya wadau wa siasa wamesema ndivyo demokrasia ya ushindani inavyokuwa, huku wengine wakimwonea huruma wakisema Chadema ingemtafutia Sumaye “namna” ya kulinda heshima yake kama waziri mkuu mstaafu.

Miongoni mwa watu waliochangia maoni yao ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole ambaye aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter akisema, “Alipokuwa CCM tulimpa kwa upendeleo uwaziri mkuu miaka 10. Mzee, nadhani muda umefika huko hakuna watu, mimi na wewe tunajua imetosha. Mwenzio amepumzika na muda wa kulea wajukuu anao!”

Maoni hayo ya Polepole ambayo ameyatoa kwa kejeli, yanabeba ujumbe mzito wa chama anachokiongoza.

Polepole anaposema, Sumaye alipokuwa CCM alipewa upendeleo wa kuwa waziri mkuu kwa miaka 10, inaonyesha kuwa chama hicho hutoa vyeo kwa upendeleo?

Pengine kauli hiyo angeitoa Rais mstaafu Benjamin Mkapa aliyempa wadhifa huo kwa muda wote huo, angekuwa na majibu sahihi, lakini Polepole (sijui wakati huo alikuwa wapi) hakuwa mtu sahihi kueleza vigezo vya Sumaye kupewa cheo hicho kwa muda wote huo.

Kwa ujumla Polepole anaonyesha kuwa Sumaye anapoteza muda wake kuwa upinzani, hivyo anatamani arudi CCM kama alivyofanya mwenzake ambaye, ingawa hakumtaja, inaonekana ni Edward Lowassa, waziri mkuu mwingine mstaafu aliyeondoka Chadema na kurejea chama tawala.

Uchaguzi huo, tangu kwenye kanuni zilizotungwa, usimamizi wake na utekelezaji wake uko kinyume kabisa na misingi ya ushindani bali ni upendeleo.

Ni kinyume cha matakwa ya wananchi na ndiyo maana katika baadhi ya vijiji, viongozi hao wanaanza kukataliwa.

Ndivyo maana kwa Chadema, pamoja na kwamba Sumaye alikuwa peke yake kama mgombea bado alipigiwa kura. Pengine angekuwa CCM angepitishwa bila kupingwa.

Suala la Chadema kumfikiria Sumaye kwa kumpa wadhifa mwingine hayo ni mambo yao ya ndani, lakini maadamu aliingia kwenye ushindani, matokeo ameyapata na hiyo sahihi kwa misingi ya demokrasia.