Breaking News

GOZI LA NG'OMBE: TFF, kalenda ya Ndayiragije haivutii

Monday October 28 2019

 

By Nicasius Agwanda

Jumatatu moja hapa hapa kwenye kolamu hii ya Gozi la Ng’ombe nilijaribu kuzungumza na ndugu yetu kutokea hapo Burundi bwana Etienne Ndayiragije.

Makala ile ilikuwa inamkumbusha tu kuwa kwa majukumu yake alikuwa anajitanua kupita kiasi kuhakikisha anawaridhisha rafiki zake wote kuwa atakuwepo kwenye sherehe zao huku pia akiwa anatakiwa kula kwenye kila sherehe.

Ilikuwa na matokeo mawili mwisho wa siku kuwa kuna upande lazima angechelewa na pia kuna upande ambao angekula kiasi kidogo cha mlo ulioandaliwa.

Wahenga walioishi zamani walisema huwezi kuwatumikia ‘watu’ wawili kwa namna inayofanana. Lazima kuna upande utakuwa na upendo nao zaidi na upo upande utakaokuwa nao kimkakati.

Kulikuwa na macho manne kwenye nafsi ya Ndayiragije yale ya Azam yaliyokuwa yanasubiri akosee yamtimue na yale ya TFF yaliyokuwa yanasubiri apatie yampatie majukumu. Bahati nzuri amepatia na Azam sasa wamenyoosha mikono huku TFF ikimleta mwanasheria wao na kumpa mkataba wa mwaka mmoja.

Huu ni mkataba wa kukodi, mkataba wa kupima uwezo wa kocha na mkataba wa kutaka kufahamu kama wamepatia au wamekosea. Kwa kifupi ni kuwa Ndayiragije amekodiwa kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Advertisement

Binafsi ni moja ya watu ambao wameamini kwa kipindi kirefu sasa kuwa huu ni mwaka wenye kurunzi la kipekee kwa Tanzania kwenye soka, mwaka ambao tumeona mwanga na giza halitupatii shida tena. Ninapoona kocha anapewa mkataba wa mwaka mmoja nakuwa narudi kwenye fikra za makosa tuliyoyafanya muda mrefu, kujaribu.

Kocha anayepewa mwaka mmoja anakuwa amewekwa kuishi kwa muda mfupi na kwa presha ya ualimu wa soka hakuna namna ambayo anaweza kuwekeza kwenye mipango ya muda mrefu.

Tafsiri pana ni kuwa Ndayiragije ataishia kulipenda boga peke yake, hataangaika na ua lake. Yeye atafanye kazi kupata ushindi wa Taifa Stars na si kuijenga Taifa Stars ya muda mrefu.

Hatakuwa na muda wa kutaka kuona Kelvin John anafanya nini na badala yake atataka John Bocco aendelee kuishi ndani ya timu ya Taifa kwa muda mrefu.

Ndayiragije hatakuwa na muda wa kuleta hamasa ya msingi kwenye timu za vijana kwa sababu ana miezi 12 pekee ya kuhakikisha “CV” yake haiingii dosari. Tunaendelea kutoka kwenye kile ambacho ni muhimu na tunakihitaji ambacho ni mikakati ya muda mrefu.

TFF lazima ifike mahala wajiamini, wafanye mambo ambayo wanaona yana tija kwa Taifa hili na yanayoweza kutusogeza kwenye hatua ya msingi na tuendelee kuwa wababe wa ukanda huu. Ni muhimu kuwe na msingi ambao hautatetereka kwa kipindi kirefu.

Mwaka mmoja ni kama hawamuamini Ndayiragije na kwa kutokumuamini maana yake na yeye atafanya kutokuwaamini na inabidi ahakikishe kinakuwa kipindi cha mavuno ambacho kitampa mkataba mpya au kumpeleka kwenye nyumba mpya yenye “heshima” zaidi.

Mipango ya muda mfupi ya TFF itaambatana na mipango ya muda huohuo ya Ndiyaragije.

Tanzania kwa sasa imeendelea kuwa na kasi nzuri na bahati nzuri ukishakuwa kwenye mtiririko huu hata wachezaji huona ile thamani ya timu ya Taifa na pale wanapoitwa wanaenda kupambana kwa machozi, jasho na damu.

Hili linapokuwa suala la msingi ni lazima pia kama shirikisho tutazame mwaka 2022 tutafanya nini na mwaka 2026 tutakuwa katika hatua gani. Vipindi vyote hivi ndivyo ambavyo vitakuwa na Kelvin John na akina Kibabage waliokomaa.

Unapompa Ndayiragije mwaka mmoja maana yake ni kuwa hata kalenda yake ya ukufunzi itakuwa inakwama mwaka 2020 mwezi Oktoba. Tafsiri ambayo haifai kabisa kwenye maendeleo ya soka. Ukufunzi wake utakuwa unategemea ukomo wa mkataba wake na ni lazima aonyeshe ustadi katika kipindi hicho pamoja na matokeo ili aendelee kuwa anayezungumzika kwa watu.

Kama kalenda ya Ndayiragije ina ukomo wa Oktoba 2020, nani anaweka mipango ya Taifa Stars na timu za vijana kwa ajili ya kuvuna wachezaji watakaosukuma taifa mwaka 2022?

Mimi ni shabiki wa Taifa Stars, mzalendo wa Taifa hili na wapo wengi kama mimi lakini pia ni mwanamahesabu wa mipango kulingana na nyakati.

Soka ni biashara na haina haja ya kumpa ajira Ndayiragije kama shukrani kwa sababu tumefuzu Chan na tunaendelea kupambania kufuzu kwenda Kombe la Dunia.

Kila walichogusa Karia na Kidao mwaka huu kimekuwa dhahabu, basi lazima waamini kuwa dhahabu ya mwaka 2022 inawafaa zaidi Watanzania kuliko wao.

Ikifanikiwa watakuwa mashujaa wakubwa kuliko ilivyokua sasa. Huku tukiwa tunawaombea kheri. Hii Kalenda ya majukumu ya Ndayiragije imepakwa rangi mbaya, haivutii.


Advertisement