Makambo: Fundi anayeondoka na rekodi Yanga SC

Monday May 27 2019

 

By Khatimu Naheka, Mwananchi

Wakati Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa imebakiza saa chache kabla ya kumalizika, jina la Heritier Makambo litabaki katika kumbukumbu ya mashabiki wa soka nchini.

Makambo anaingia katika rekodi ya kuwa mmoja wa washambuliaji hodari aliyechochea moto katika mashindano hayo msimu huu.

Bila shaka nyota wa Simba Meddie Kagere, atamuota Makambo kutokana na ushindani wao wa kuwania tuzo ya mfungaji bora wa Ligi Kuu msimu huu.

Kagere anaongoza kwa mabao 23 akifuatiwa na Makambo na Salim Aiyee wa Mwadui ya Shinyanga wenye mabao 17 kila mmoja.

Hakika mashabiki wa Yanga watamisi staili ya ushangiliaji wa nyota huyo raia wa DR Congo anayetarajiwa kwenda kuanza maisha mapya katika Klabu ya Horoya ya Guinea. Mbali na kufunga mabao,

Makambo anaondoka Yanga akiwa mchezaji mwenye nidhamu bora kwani licha ya klabu hiyo kupitia kipindi kigumu cha mtikisiko wa kiuchumi hakuwahi kupaza sauti.

Advertisement

Makambo aliendana na mazingira ya soka ya bongo kwani hakukata tamaa aliendelea kuzingatia nidhamu ndani na nje ya uwanja na matunda yake yameonekana.

Kitendo cha Makambo kutanguliza mbele kazi yake ni funzo tosho kwa wachezaji wa Tanzania kwani wapo waliogoma ndani ya klabu hiyo wakidai malimbikizo ya mshahara na posho.

Makambo anaondoka Yanga akiwa na rekodi ya kufunga mabao yaliyotokana na mpira wa kichwa. Makambo unaweza kumfananisha na nyota wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Abeid Mziba ‘Tekelo’ aliyewika katika miaka ya 1980 akiwa na rekodi ya aina yake ya kufunga mabao ya kichwa katika kipindi chote alichokuwa mchezaji kabla ya kutundika daluga.

Safari ya kutua Yanga

Makambo anaondoka Yanga akiwa shujaa kwa kuwa ataipa fedha ambazo hawakutarajia kwani wakati anatua hakuwa mchezaji mwenye jina kubwa kiasi cha kupigiwa hesabu kama angekuwa nyota tegemeo.

Usajili

Baada ya kufuzu majaribio usajili wa Makambo nusura ugonge mwamba kutokana ukata. Makambo alitaka Dola 20,000 (Sh46 milioni) ili atie saini mkataba wa miaka miwili, lakini Yanga haikuwa na fedha hizo kabla ya kufikia mwafaka baada ya meneja wake kuja nchini kumaliza sakata hilo.

Baada ya kufikia mwafaka Makambo alitia saini mkataba wa miaka miwili wenye thamani ya Dola 15000 (Sh34.2 milioni).

Safari ya Makambo ilianza katika mchezo wa kimataifa wa makundi wa Kombe la Shirikisho ambapo alifunga bao lake la kwanza lililokuwa la ushindi na kuipa Yanga wa mabao 2-1. Bao la kwanza lilifungwa na Deus Kaseke.

Makambo akiwa na msimu wa kwanza Yanga, alipata mafanikio kutokana na kiwango chake cha kufunga mabao katika Ligi Kuu.

Mshambuliaji huyo amefunga jumla ya mabao 21 yakiwemo 17 aliyoweka wavuni katika ligi pia alifunga manne kwenye Kombe la FA.

Rekodi

Katika mabao 17 aliyofunga kwenye ligi 10 amefungwa kwa kichwa, mguu wa kushoto akifunga sita na moja pekee alifunga kwa kiki ya mguu wa kulia.

Makambo hakuwahi kufunga bao la penalti ndani ya dakika 90 katika ligi ingawa aliwahi kukosa dhidi ya Alliance kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Hata hivyo, Makambo alifunga mkwaju wa penalti dhidi ya Biashara United katika mchezo wa Kombe la FA katika uamuzi wa penalti tano tano.

Simba

Mpaka anaondoka Makambo hakuwahi kuonja ushindi kwa timu yake mbele ya watani wao wa jadi Simba na hakuwahi kuifunga timu hiyo katika mechi mbili za miamba hiyo ya jijini Dar es Salaam.

Katika mechi hizo mbili Yanga iligangamala na kulazimisha sare kabla ya kulala bao 1-0 katika mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu.

Horoya

Endapo mpango huo utakamilika kama pande hizo zitafikia mwafaka kama inavyotarajiwa, Yanga inatarajiwa kuvuna Dola 100,000 (Sh228 milioni) kutoka Horoya ambayo ni moja ya klabu maarufu nchini Guinea.

Advertisement