GOZI LA NG'OMBE: Messi mfalme mwenye walakini

Monday May 13 2019

 

By Nicasius Agwanda

Inawezekana kabisa kwenye vichwa vya wengi, Mei Mosi ni siku ya kimataifa ya wafanyakazi, siku ambayo ina historia kwenye maisha ya binadamu wengi, siku ambayo inawakumbusha wajibu watendaji wa nafasi mbalimbali kwenye ajira. Wakati katika vitabu vya sheria na taratibu za kidunia ikiwa inahesabika hivyo, kuna binadamu kwake hii ni siku tofauti, siku ya maajabu na siku ambayo ilianzisha maisha yake yenye mafanikio makubwa.

Akiwa amevaa jezi namba 30 na umri wa miaka 17 pembeni kidogo mwa uwanja dhidi ya klabu ya Albacete, kwa mguu wake wa kushoto alikuwa anapiga pasi kwa Ronaldinho kisha anakimbia kwenye kisanduku na kupokea mpira kutoka kwa mfalme wa Camp Nou kipindi hicho na kisha kufunga bao lake la kwanza.

Anaitwa Lionel Messi Lapulga, mchezaji ambaye wapo wanaoweza kuamini kuwa tangu dunia imeumbwa na Mungu kupuliza pumzi kwenye mwili wa Adam hajawahi kupatikana mwanamume mwenye kipaji cha soka kumzidi.

Haya yote yalifanyika ili yaliyokusudiwa yatimie hata kama hayakuwa kwenye maandiko matakatifu. Hiyo ikiwa ni Mei Mosi mwaka 2005, miaka 14 baadaye yaani Mei Mosi 2019, Messi sasa akiwa na ndevu na tuzo zinazomtosheleza kwenye chumba chake, alikuwa anakutana na Liverpool ambayo iliaminika kuwa na chanjo dhidi ya ugonjwa ulioitwa Barcelona kwenye Klabu bingwa Ulaya.

Liverpool ambayo imewastaajabisha wengi kuanzia England mpaka Ulaya, Liverpool yenye mchezaji bora wa mwaka wa England, Liverpool ambayo ilikuwa na wafungaji bora wa wawili wa msimu huu wa England na Liverpool ambayo ilifika fainali hizi msimu uliopita ilikuwa inategemewa kuweka utofauti kwenye mchezo huu uliokuwa Camp Nou.

Haikuwa tofauti na mategemeo ya wengi kwani tofauti na bao la Luiz Suarez, Liverpool ilionekana kuwa timu bora zaidi ndani ya uwanja kwa dakika zaidi ya arobaini mpaka pale ambapo Messi alipotaka kupenyeza kisu chake cha moto kwenye moyo wa Liverpool. Messi alifunga mabao mawili na kufanya afikishe 600 kwenye ngazi ya klabu ikiwa analingana na Cristiano Ronaldo. Akiwa na umri wa miaka 31 ni wazi kuwa kutokana na ukweli kuwa majeruhi ya kumuweka nje muda mrefu haijawahi kuwa jadi yake basi tutegemee kuendelea kuona historia ikiendelea kuandikwa.

Advertisement

Messi ni hadithi ambayo watakaosimuliwa baadaye watatamani wangekuwapo wamshuhudie. Huyu ataandikiwa kitabu ambacho simulizi yake itakuwa inasisimua, kuanzia matatizo ya kukua mpaka kuwa kiumbe cha kutisha ndani ya uwanja. Pamoja na Liverpool kuwaondoa kutokana na udhaifu wa kocha Valverde bado Messi anahesabika kama mwanamume wa shoka uwanjani.

Pengine Arsene Wenger hakuwahi kukosea aliposema Messi wa ndani ya uwanja na Messi wa ‘playstation’ hawana tofauti. Inawezekana haikuwa jambo ambalo tulitakiwa kushangaa kipindi ambacho mzee Fergusson (Sir Alex) akiwa ndani ya Wembley katika mazingira yenye joto alikuwa akitetemeka na mkono wake wa pete kuonekana ukiwa unakosa nguvu yake.

Huyu ni Messi ambaye ameshinda kila kitu isipokuwa Kombe la Dunia na Copa America. Messi ambaye mashindano ya ngazi ya Taifa hayajawa sehemu ya mafanikio yake.

Ufalme wa Messi upo Catalunya kuliko Argentina, historia ya Messi ipo Camp Nou kuliko Estadio Antonio Vespucio Liberti. Wakati akiipa adhabu iliyodumu kwa muda mfupi, Liverpool hili ndilo jambo lililokuwa linakuja kichwani mwangu.

Tatizo langu likawa mtu ataandikaje kitabu cha mchezaji bora kuwahi kutokea duniani anayeitwa Messi kama Kombe la Dunia na Copa America havitakuwepo kwenye hesabu? Utasimuliaje hadithi kuwa mchezaji bora wa muda wote alishindwa katika fainali za kombe la dunia mara moja na kushindwa kwenye fainali za Copa America mara tatu?

Wachezaji wenzake wanaotajwa katika sauti zinazokaribiana au kuimbwa katika beti zinazokaribiana, mashairi yao yana makombe ya kimataifa isipokuwa Messi. Hii inaweza kuwa fimbo itakayomwadhibu, hii itakuwa nyota itakayowekwa pembeni mwa jina lake kwenye historia yake kuweka uwalakini. Endapo hatashinda kombe lolote kutakuwa na sababu kubwa ya watu kutokuamini uwezo wake. Imani itabaki kwa raia wa Hispania na sio nyumbani wapinzani watapata tope la kumpaka hususani wakikumbuka kuwa Diego Maradona aliwahi kuleta Kombe la Dunia kwa mbinu zote mpaka bao la mkono lililobatizwa kuwa ‘goli la mkono wa Mungu’. Messi aondoe alama hii ya nyota na stori yake itakuwa ya kusisimua maradufu.

Asipofanya hili, kazi aliyotumwa duniani itakuwa haijakamilika na kutakuwa na wafalme watakaotajwa kabla yake. Ataitwa mfalme mwenye uwalakini.

Advertisement