Wachezaji Watanzania waliokimbia corona nje

Monday April 13 2020
pic corona

Wakati wanasayansi duniani kote wakihangaika kutafuta tiba ya ugonjwa wa virusi vya corona, Covid-19, serikali za nchi mbalimbali duniani zimeendelea kutoa maelekezo kuhusu namna ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo.

Janga la corona ndilo lililosababisha kusitishwa kwa shughuli mbalimbali za michezo ili kupunguza kasi ya kusambaa kwa virusi hivyo kama si kuvitokomeza kabisa.

Katika eneo hilo la kusitishwa kwa shughuli za michezo, imewabidi wachezaji kadhaa wa Tanzania wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi warejee nyumbani kusubiri hali itakapokuwa shwari.

Kwa nini wamerejea nchini wakati wachezaji wengine wameendelea kuwepo katika mataifa wanayocheza, akiwemo Abdi Banda anayecheza nchini Afrika Kusini, Simon Msuva na Nickson Kibabage waliopo Morocco na Mbwana Samatta ambaye anacheza Aston Villa ya England?

“Nilipewa uhuru wa kufanya uamuzi wa kubaki Msumbiji au kurejea nyumbani,” anasema mshambuliaji Eliuter Mpepo ambaye ni mmoja kati ya wachezaji waliorejea nchini.

Mpepo ni mmoja wa wanasoka waliorejea nyumbani wakati wa mapumziko ya corona.

Advertisement

Habibu Kyombo

Licha ya kutocheza mchezo hata mmoja katika kikosi cha Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kutokana na kuuguza jeraha la goti, Kyombo amerejea nyumbani ili kuwa karibu na familia yake katika kipindi hiki.

Inaelezwa kwamba kuna programu maalumu ambazo Kyombo anaendelea nazo nchini kwa maelekezo ya benchi la ufundi la Mamelodi.

Mchezaji huyo wa zamani wa Mbao na Singida United anatazamwa kama nyota wa baadaye wa klabu hiyo ambayo imekuwa ikitawala soka la Afrika Kusini.

Eliuter Mpepo

Ni mchezaji wa A.D. Sanjoanense ya Ureno lakini akiwa CD Costa do Sol ya Msumbiji kwa mkopo. Klabu hiyo ni mabingwa wa Msumbiji.

Anaamini kuwa nyumbani ni mahali salama zaidi kwake.

“Msumbiji ni ugenini kwangu, kwa hiyo tulivyopewa uhuru wa kuchagua nikaona ni bora nirudi nyumbani kwanza ambako nitakuwa na nafasi pia ya kuwahamasisha vijana wenzangu kuchukua tahadhari,” alisema mshambuliaji huyo wa zamani wa Buildcon ya Zambia.

“ Lakini pamoja na hilo, niliona nitakuwa na muda mwingi wa kufanya mazoezi binafsi na marafiki zangu wachache. Nataka haya mambo yakipita niendelee kuwa katika kiwango changu.”

David Kissu

Kipa wa Gor Mahia, David Kissu anasema ukaribu wa Kenya na Tanzania umechangia kuamua kurejea nyumbani akiwa na rafiki yake katika klabu hiyo, Dickson Ambundo.

“Tuliona turudi na viongozi hawakuona kuwa ni tatizo. Lakini kuna programu za mazoezi ambayo tumekuwa tukifanya kila siku kwa maelekezo ya benchi letu la ufundi,” alisema.

“Mazoezi tumekuwa tukifanya asubuhi, kwa mchana na jioni huwa ni ratiba za mchezaji binafsi. Tumekuwa tukisisitizwa kila mtu kujisimamia ipasavyo,” anasema kipa huyo wa zamani wa Njombe Mji na Singida United za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Dickson Ambundo

Ambundo, ambaye yupo kwa mkopo Gor Mahia akitokea Alliance ya Mwanza, anasema kuwa karibu na familia ni jambo muhimu kwake kipindi hiki ambacho wanapaswa kuchukua tahadhari ya mambukizi ya corona.

“Nashukuru Mungu nilifika salama kwa sababu katika hizi safari wapo wanaopata maambukizi. Mimi na rafiki yangu tulifika salama na tunaendelea na mazoezi binafsi ili kujiweka fiti,” anasema mshambuliaji huyo.

Aman Kyatta

Beki wa Kariobang Shark ya Kenya, Aman Kyatta anasema: “Mazoezi ambayo kwa sasa nafanya nikiwa nyumbani ni kwa ajili ya utimamu wa mwili, lakini hofu yangu ni kwamba huenda wachezaji tusirejee tukiwa katika viwango vyetu kwa sababu ili mchezaji kuwa fiti kiushindani anatakiwa kucheza.”

Corona ni kirusi cha aina gani?

Corona ni jamii kubwa ya virusi vinavyosababisha maradhi kwa wanyama na binadamu.

Kwa binadamu, jamii kadhaa za virusi vya corona vinafahamika kusababisha maambukizi kwenye njia ya hewa na mfumo wa upumuaji.

Maradhi yaliyowahi kusababisha madhara makubwa kutokana na virusi vya corona ni pamoja na MERS na SARS yaliyozuka mwanzoni mwa miaka ya 2000.

Kirusi cha corona kilichogundulika hivi karibuni kinasababisha ugonjwa unaofahamika kama Covid-19 ambao hadi umesababisha maelfu ya watu kufariki na wengine kuambukizwa ingawa habari njema ni kwamba wapo pia wengi wanaopona na kutoka hospitali.

Advertisement