Mazishi ya Bilago yaibua utata

Muktasari:

Utata huo unatokana na siku ya mazishi, upande mmoja unadai atazikwa kesho na mwingine keshokutwa

 


Dodoma. Mvutano umeibuka hasa lini aliyekuwa Mbunge wa Buyungu (Chadema), Kasuku Bilago atazikwa.

Ratiba iliyotolewa jana Bungeni Mei 28, 2018 na Naibu Spika Dk Tulia Ackson alisema Bilago anatarajiwa kuzikwa kesho Mei 30, 2018 mkoani Kigoma.

Lakini, ratiba ya chama chake cha Chadema na familia walisema atazikwa keshokutwa.

Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai alipoulizwa na Mwananchi leo asubuhi Mei 29,2018 amesema, ratiba ya Bunge kama ilivyotoka kwamba watazika kesho.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema,"saa hizi nipo Airport tunaupandisha mwili katika ndege lakini sisi tunazika keshokutwa."

Mbowe ambaye pia ni kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni ameongeza,"labda waulize (Bunge) wanazika kesho wamewasiliana na chama gani na familia gani. Sisi tunazika keshokutwa na tutaondoka baada ya kumaliza kuaga hapo Dodoma."

Mvutano mwingine uliojitokeza ni gari ambalo limeandaliwa na Bunge kuwabeba wabunge lililotarajiwa kuondoka asubuhi kwenda Kigoma, kuwa na utata kama limeondoka.

Mbunge wa Ukonga, (Chadema), Mwita Waitara amesema, "tumegoma kutoka asubuhi, tumekodi basi letu na tutaondoka baada ya kumaliza kuaga."

Waitara amesema,"kama hilo basi limeondoka basi litakuwa limewabeba wabunge wa CCM na watumishi wa Bunge. Sisi tunamzika mwenzetu keshokutwa hilo la kesho wanalijua wao."