Mgomo wa daladala Tanga waingia siku ya pili

Muktasari:

  • Mgomo huo wa daladala umetoa fursa kwa wenye bajaji, bodaboda na baiskeli kujiongezea kipato.

Tanga. Mgomo wa daladala jijini Tanga umeingia siku ya pili leo Jumanne, Oktoba 17 huku waendesha bodaboda, bajaji na baiskeli wakitumia fursa hiyo kutoa huduma na kujiongezea kipato.

Mgomo huo pia umesababisha watu wengi kutembea kwa miguu kwenda maeneo mbalimbali jijini Tanga.

Wakizungumza na Mwananchi, baadhi ya abiria wamesema wamelazimika kukodi bodaboda baada ya kukosa huduma ya daladala.

“Nawalaumu wenye daladala kwa kugoma na kusababisha tukose huduma. Nikilinganisha na sababu wanazotoa, naona lilikuwa ni jambo la kufanya mazungumzo na mamlaka husika kwa sababu wameleta

usumbufu mkubwa,” amesema Mariam Said mkazi wa Makorora jijini Tanga.

Amesema mgomo huo wa daladala umesababisha abiria kukodi bajaji na kulipa nauli kwa kuchangia.

Wakati hali ikiwa hivyo, mkazi wa jijini Tanga, Daudi Mohamed amesema wenye bajaji wamekuwa wakiwatoza kati ya Sh400 na Sh500 kwa kila abiria, hivyo mgomo wa daladala utawafanya wazoee kutumia usafiri huo kwa kuwa gharama si kubwa.

Dereva wa bodaboda, Mohamed Mjata amesema mgomo huo umewapa faida akisema jana Jumatatu, Oktoba 16 alipata Sh70,000 tofauti na Sh10,000 ambazo huzipata kwa siku.

Ofisa wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) Mkoa wa Tanga, Dk Walukani Kuhamba amesema wamekuwa na vikao na Jeshi la Polisi, Halmashauri ya Jiji la Tanga, wenye daladala na baraza la watumiaji wa huduma za usafiri

kwa ajili ya kufikia muafaka ili huduma zirejee.

Madereva wa daladala wamesema wamelazimika kufanya mgomo kupinga utozwaji wa faini unaofanywa na askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani kwa makosa ambayo si ya kwao.

Wamesema wanaposhusha abiria vituoni, wamekuwa wakikamatwa na kutozwa faini wakielezwa si vituo halali lakini hawaonyeshi vituo viko wapi.

Madereva hao wamesema Halmashauri ya Jiji la Tanga haijawajengea vituo, hivyo kitendo cha kuwakamata wenye daladala wanaona ni kuwanyanyasa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba amesema jeshi

hilo haliwezi kufumbia macho vitendo vya uvunjifu wa sheria za barabarani na kuwataka wenye daladala kutimiza wajibu wao badala ya kugoma.