Mwinyi: Sina siku nyingi za kuiacha dunia

Rais John Magufuli, akimshukuru Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi ambaye pia ni Mdhamini wa Chama cha Skauti Tanzania baada ya kumaliza kuzungumza wakati wa hafla ya kumuapisha Kamishna Mkuu wa chama hicho, Mwantum Mahiza Ikulu, Dar es Salaam jana. Picha na Anthony Siame

What you need to know:

  • Oktoba 2, Mwinyi alikuwa mkoani Arusha kwenye maadhimisho ya siku ya wazee kitaifa kama mgeni rasmi na kuteuliwa kuwa mlezi wa mabaraza ya wazee nchini. Katika hotuba yake, alikumbushia namna alivyojiuzulu wadhifa wake wa Waziri wa Mambo ya Ndani kutokana na kukithiri kwa mauaji ya vikongwe.
  • Mwinyi alisema hawezi kukwepa jukumu la kuwa mlezi wa wazee kwa sababu yeye pia ni mzee na kwamba atayabeba matatizo yote yanayowakabili wazee na kuyafikisha sehemu husika kwa ajili ya ufumbuzi.
  • Rais huyo mstaafu alimtaka Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kuhakikisha kwamba huduma za afya za uhakika zinapatikana kwa wazee hao ili kuwazidishia umri na kutumia busara zao katika maendeleo ya Taifa ikiwemo uhakika wa dawa hasa kwa magonjwa yanayosumbua wazee.

Dar es Salaam. Hotuba aliyoitoa rais wa zamani, Ali Hassan Mwinyi jana Ikulu jijini Dar es Salam, akidokeza muda wake uliosalia duniani, ilimtoa machozi waziri wa zamani, Mwantumu Mahiza.

Mwinyi, ambaye ni mdhamini wa Skauti, alitoa hotuba hiyo wakati wa hafla ya kuapisha wateule wa Rais, akiwemo Mahiza, ambaye amekuwa Skauti Mkuu.

Ukumbi wa mkutano ulikuwa kimya wakati Mwinyi alipotamka maneno hayo, akionekana kutoa wosia kwa wateule kulinda heshima yake.

“Sina siku nyingi za kuiacha dunia,” alisema rais huyo wa Serikali ya Awamu ya Pili na maneno hayo yalimfanya Mahiza ainamishe kichwa na kuonekana akijifuta machozi.

“Leo nina miaka karibu 94, sina siku nyingi za kuiacha dunia. Sitaki niende huko ninakokwenda na aibu nyuma yangu,” alisema Mwinyi.

Kiongozi huyo mstaafu alitoa mfano wa kisa kimoja cha mtu aliyechora ubavuni mwa nyumba ya mtu kwamba maisha ni binadamu ni hadithi tu hapa ulimwenguni, hivyo aliwataka Skauti nao wawe hadithi nzuri kwa wale watakaosimuliwa habari zake.

Mwinyi alipewa nafasi ya kuzungumza baada ya Rais Magufuli kumuapisha katibu mkuu mpya wa Wizara ya Mambo ya Nje, Faraji Mnyepe na Mahiza ambaye ni Skauti Mkuu.

Katika hotuba yake iliyochukua dakika 15, Mwinyi alizungumzia mambo mbalimbali ikiwamo kuwataka viongozi wa Skauti wafanye kazi kwa kufuata kanuni ili wasimtie aibu yeye na Rais John Magufuli ambaye alimteua kushika nafasi ya mdhamini wa Skauti nchini.

Mwinyi alianza hotuba yake kwa kuomba radhi, akisema ana tatizo lake la kusahau na kwamba hivi karibuni atatafuta mwalimu wa lugha ya Kiswahili kwa sababu kutokana na umri wake anasahau maneno mengi.

Alieleza namna anavyomhusudu Rais Magufuli kwa mambo makubwa ambayo anayafanya kwa maslahi ya Taifa. Alisema naye anatamani angekuwa kama Magufuli.

Kwa upande wake, Rais Magufuli alisema Mwinyi ni moja ya viongozi ambao ni wanyenyekevu tofauti na wengine, hasa waliowahi kushika madaraka makubwa. Alisema atazidi kumuombea aishi zaidi ili aendelee kutumika katika maendeleo ya nchi.

“Ni mzee mmojawapo ambaye ni mnyenyekevu sana. Hana makuu, anajishusha, anatambua kuna kuishi na kuna kufa,” alisema Rais Magufuli ambaye mara kadhaa anapozungumzia viongozi wa zamani hutumia neno “wazee” kumaanisha marais wa zamani.

“Mmemsikia amezungumza mwenyewe; anataka akumbukwe kwa mazuri anayoyafanya. Ni watu wachache sana ambao wanakumbuka haya.”

Alisema watu walioshika nyadhifa kubwa kama Mwinyi hawakumbuki kama maisha ya hapa ulimwengini ni ya muda mfupi. Alisema aliamua kumteua kuwa mdhamini wa Skauti akiamini kwamba ameteua mtu sahihi.

“Chombo hiki cha Skauti ambacho kinafanya kazi nzuri sana katika nchi yetu, kinahitaji mzee mwenye busara kama Mzee Mwinyi, ambaye saa nyingine hata anapoleta maombi ya Skauti, yanakuwa si maombi, inakuwa ni amri, kwa hiyo inabidi uyatekeleze,” alisema Rais Magufuli.

JPM azungumzia ziara za nje

Akizungumzia Wizara ya Mambo ya Nje, Rais Magufuli alisema kutosafiri kwake kunaokoa fedha za Serikali ndiyo maana amekuwa akimtuma waziri wa wizara hiyo, Dk Augustine Mahiga kumuwakilisha.

Kauli hiyo ya Rais Magufuli imekuja ikiwa ni siku chache baada ya Waziri Mahiga kurejea nchini kutoka Marekani alikokwenda kumuwakilisha Rais Magufuli kwenye mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN).

Pia Rais amekuwa akiwakilishwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan au Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Tangu mwaka Novemba 2015 alipoingia madarakani, Rais Magufuli amefanya ziara katika nchi nne tu nje katika nchi za Rwanda, Kenya, Uganda na Ethiopia alikokwenda kuhudhuria mkutano wa Umoja wa Afrika (AU).

Alisema uamuzi huo unaokoa fedha nyingi za Serikali kwa sababu akisafiri hulazimika kwenda na ujumbe mkubwa wa watu. Alimpongeza Waziri Mahiga kwa kumuwakilisha vema.

“Nafikiri ni juzi tu ametoka kwenye mkutano wa UN, kule walihudhuria marais wengi wa nchi nyingi. Mimi sikuhudhuria, alienda yeye tu, kwa hiyo nili-save (okoa) hela,” alisema.

“Kwa sababu ukimtuma mmoja na msaidizi wake ni tofauti na kwenda Rais na wasindikizaji, advanced party na nini, kwa hiyo nime-save. Kwa hiyo nimeipunguzia gharama Serikali.”

Kuhusu utendaji wa wizara hiyo, Rais alisema kuna wakurugenzi wazuri lakini wapo ambao wanafanya kazi kwa mazoea na kumtaka katibu mpya kwenda kuwabadilisha na kuwapeleka kwenye wizara nyingine ambako kuna nafasi.

Skauti ni jeshi dogo

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako alisema Chama cha Skauti Tanzania (TSA) ni jeshi dogo linalomsaidia Rais katika kujenga kizazi chenye maadili.

Alisema majukumu ya chama hicho ni kulea vijana katika misingi ya maadili, uzalendo, kuwajengea uwezo wa kujitambua na kujisimamia, kuwa wabunifu na kujenga uwezo wa kujitolea kufanya kazi.

Profesa Ndalichako alisema jeshi hilo limekuwa likitekeleza majukumu yake kama ya kupiga vita rushwa chini ya klabu mbalimbali kuanzia ngazi ya shule za msingi hadi vyuo vikuu nchini.

“Ni vijana wanaojengewa uzalendo, wanaoweza kukusaidia (Rais Magufuli) katika mambo mengi ikiwamo kampeni za kupiga vita Ukimwi. Wao wanapokea kauli mbiu na kuzihamasisha kwa jamii,” alisema Profesa Ndalichako akizungumzia chama hicho kilichoanzishwa miaka 100 iliyopita hapa nchini.

Kuimarisha skauti vyuoni

Akizungumza katika hafla hiyo, Mahiza alitaja vipaumbele viwili katika kipindi cha utekelezaji wa majukumu yake ndani ya miaka minne ya utumishi wa Chama cha Skauti Tanzania (TSA) ambavyo ni kuwekeza nguvu zaidi ya chama hicho katika ngazi ya vyuo vya kati na vyuo vikuu nchini.

Alisema kwa miaka mingi chama hicho kilijikita zaidi katika ngazi ya shule za msingi na sekondari, lakini ni muda sahihi kwa sasa kuelekeza nguvu katika maeneo hayo ili kuongeza hali ya uzalendo nchini.

Alisema atahakikisha skauti inaenea vyuo hivyo, ili kupata wazalendo wa kweli, na pia kufanikisha ujenzi wa kambi ya kimataifa ya mkoani Dodoma.

“Kwa sasa tuna kambi ndogo ipo Morogoro na imepitwa na wakati,” alisema Mwantumu aliyewahi kuongoza nafasi mbalimbali Serikalini.

Alisema Tanzania imekuwa ni kituo kikubwa cha mataifa mengine kuja kujifunza masuala ya skauti, huku viongozi wa hapa nchini wakishiriki mialiko mikubwa duniani.