Roma amwaga chozi

Msanii wa muziki wa hiphop, Ibrahimu Musa ‘Roma Mkatoliki’ akiwaonyesha jana waandishi wa habari majeraha aliyoyapata baada ya kutekwa jijini Dar es Salaam. Aliyeketi ni mkewe Nancy Mshana. Picha na Said Khamis

Muktasari:

“Watu wanasema tunatumika kisiasa tunataka kuichafua Serikali, wapo wanaosema tunatafuta kiki na kuna wengine wamekwenda mbali zaidi na kudai tumelipwa Dola 5,000 ili tutengeneze habari hii.

Msanii wa Muziki wa kizazi kipya, Roma Mkatoliki amezungumza kwa hisia juu ya wasanii wenzake na watu wengine ambao wanahusisha kutekwa kwao na mchezo wa kiini macho.

“Watu wanasema tunatumika kisiasa tunataka kuichafua Serikali, wapo wanaosema tunatafuta kiki na kuna wengine wamekwenda mbali zaidi na kudai tumelipwa Dola 5,000 ili tutengeneze habari hii.

“Tunaumizwa sana na kauli hizo, nguvu za watu walizotumia kupaza sauti zao halafu watu wanasema tunacheza mchezo, hatuwezi kuhatarisha maisha yetu kwa sababu ya fedha sisi ni watu wa kawaida sana familia zetu ni masikini, lakini hatuwezi kukubali kuumizwa hivi kwa ajili ya fedha.”

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Harrison Mwakyembe amesema anataka kupata majibu ya tukio la utekaji wa Roma Mkatoliki kabla ya kuwasilisha bajeti yake bungeni.

“Mimi nitakuwa kwa wapelelezi, nataka kujua suala hili nipate majibu kabla sijawasilisha bajeti yangu bungeni ili bajeti yangu ipite bila makelele mengi,” amesema.