KALAMU HURU: Kauli za RPC Shanna ni salamu za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020

Wakati mfumo wa vyama vingi unarejeshwa miaka ya 1990, viongozi wa majeshi ya ulinzi na usalama walizuiwa kushiriki shughuli za kisiasa.

Katiba ibara ya 147(3) inasema, “Itakuwa ni marufuku kwa mwanajeshi yeyote kujiunga na chama chochote cha siasa, isipokuwa tu kama atakuwa na haki ya kupiga kura iliyotajwa katika ibara ya 5 ya Katiba hii.”

Ibara ya 147(4) inaeleza maana ya “mwanajeshi” kuwa ni askari aliyeajiriwa kwa masharti ya muda au ya kudumu katika Jeshi la Ulinzi, Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza au Jeshi la Kujenga Taifa.

Lakini karibu miaka 30 sasa tangu mfumo huo urejeshwe, baadhi ya viongozi wa majeshi hayo, hawaoni aibu kuhubiri siasa kwenye mikutano ya chama cha siasa, hususan CCM. Hii ni dalili mbaya kwa mfumo wa demokrasia ya vyama vingi.

Kauli ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Jonathan Shanna alizotoa hivi karibuni akiwa katika mkutano wa ndani wa CCM zimeonyesha anguko kubwa la demokrasia.

Akizungumza katika mkutano huo, Kamanda Shanna aliyesema kuwa amepewa baraka zote na IGP Sirro kuhudhuria mkutano huo, alieleza sababu ya yeye kuwepo pale akisema:

“Kuna hesabu darasa la nne inasema kama A ni sawa na B na B ni sawa na C, kwa hiyo A ni sawa na C. Maana yake A ni chama tawala na B ni Serikali halali na C ni vyombo vya Dola ndiyo sisi. Sasa kama chama tawala, Serikali, vyombo vya Dola, sasa wewe jiulize A kama is equal to C maana yake nini?”

Kwamba sasa RPC Shanna ambaye kitaaluma ni mwanasheria, hajui kwamba Katiba haimruhusu kujihusisha na siasa hivyo, hadi asema maneno yanayomaanisha vyombo vya dola ni sawa na chama tawala.

Pengine ni ana sababu zake au kwa vyovyote ni ukiukwaji mkubwa wa Katiba na inashangaza kwa nini hakuchukuliwa hatua.

Hivi Kamanda Shanna anaweza kuingia kwenye mkutano wa Chadema, CUF au ACT-Wazalendo au chama kingine cha upinzani na kuzungumza yale aliyozungumza pale, japo akawahakikishia wajumbe kuwa Jeshi la Polisi litawalinda?

Mbali na Shanna, tumesikia na kuona baadhi ya makamanda wengine wa polisi wa mikoa wakionyesha upendeleo katika maamuzi.

Kwa mfano katika kufanya mikutano ya hadhara na maandamano ambayo ni haki ya vyama vya siasa, utashangaa kuona hawa wakiruhusiwa kufanya mikutano lakini wengine wanakataliwa.

Katika baadhi ya maeneo, makada wa CCM wamefanya maandamano wakilindwa na Polisi, lakini wapinzani wanatishwa kwa maneno makali kama, “Wakiandamana watapigwa hadi kuchakaa au watapata taabu sana.”

Hizi ni dalili mbaya kuelekea uchaguzi mkuu wa 2020, kwamba huenda usiwe huru na wa haki kwa kuwa polisi wanaonyesha upande walipo.