Video: Waziri Lugola asema wanaendelea kumtafuta mfanyabiashara Mo Dewji

Muktasari:

Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola leo amezungumzia tukio la kutekwa kwa bilionea, Mohamed Dewji ‘Mo Dewji; akisema vyombo vya dola vinaendelea kumtafuta


Dar es salaam. Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amesema bado Jeshi la Polisi linaendelea na juhudi za kumpata Bilionea Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ aliyetekwa  siku tatu zilizopita.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam, Lugola alisema mpaka sasa kuna watuhumiwa 20 wameshakamatwa na wanaendelea kuhojiwa.

"Na waliohusika na tukio hilo watasakwa mpaka pale watakapopatikana, tunavyozungumza sasa (saa 9 jioni), takribani watu 20 wanashikiliwa na kuhojiwa na Polisi, " alisema.

Hata hivyo, Lugola alisema watuhumiwa ambao hawaonekana hawakuhusika na tukio hilo wataachiliwa huru kabla ya saa 24, jambo ambalo pia alisema halijatekelezwa.

Waziri huyo alisema Jeshi la Polisi linaendelea kuwatafuta wote waliotekwa na kupotea hadi wapatikane.

"Kwa hiyo siyo kwamba limetokea tukio la MO Dewji ndio polisi wanafuatilia hilo tu. Polisi hawataacha kuwatafuta na kuwakamata na wengine waliohusika kwenye matukio mengine ili  kuhakikisha wanapatikana," alisema.

Alisema kuna watu wanadhani polisi inaona MO Dewji ndiyo wa muhimu kumtafuta kuliko watu wengine jambo ambalo siyo sahihi.

"Ondoeni hiyo perception (dhana) kila Mtanzania anayo thamani sawa na mwingine," alisema.

Alisema Rais Magufuli ameapa kulinda uhai wa kila Mtanzania na mali zao, huku akiwataka waandishi wa habari kutoinyooshea kidole Serikali kwa utekaji huo..